The chat will start when you send the first message.
1Baada ya Yesu kumaliza kusema haya yote kwa watu waliokuwa wanamsikiliza, akaingia Kapernaumu.
2Mtumishi wa jemadari mmoja Mrumi, ambaye bwana wake alimthamini sana, alikuwa mgonjwa sana karibu na kufa.
3Jemadari huyo aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee wa Wayahudi kwake, wakamwomba aje kumponya mtumishi wa huyo jemadari.
4Wale wazee walipofika kwa Yesu, wakamsihi sana amsaidie yule jemadari wakisema, “Mtu huyu anastahili wewe umfanyie jambo hili,
5kwa sababu analipenda taifa letu tena ametujengea sinagogi.”
6Hivyo Yesu akaongozana nao.
Lakini alipokuwa hayuko mbali na nyumbani, yule jemadari akatuma rafiki zake kumwambia Yesu, “Bwana, usijisumbue, kwani mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu.
7Ndiyo maana sikujiona hata ninastahili kuja kwako wewe. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona.
8Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”
9Yesu aliposikia maneno haya, alishangazwa naye sana. Akageukia umati ule wa watu waliokuwa wanamfuata, akawaambia, “Sijaona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.”
10Nao wale watu waliokuwa wametumwa kwa Yesu waliporudi nyumbani walimkuta yule mtumishi amepona.
11Baadaye kidogo, Yesu alienda katika mji mmoja ulioitwa Naini. Nao wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu walienda pamoja naye.
12Alipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule walikuwa pamoja na huyo mwanamke.
13Bwana Yesu alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.”
14Kisha akalikaribia jeneza, akaligusa. Nao wale waliokuwa wamelibeba wakasimama. Akasema, “Kijana, nakuambia, inuka.”
15Yule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Yesu akamkabidhi kwa mama yake.
16Watu wote wakajawa na hofu ya Mungu, nao wakamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea miongoni mwetu. Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.”
17Habari hizi za mambo aliyoyafanya Yesu zikaenea Yudea yote na sehemu zote za jirani.
18Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji wakamweleza Yohana mambo haya yote. Hivyo Yohana akawaita wanafunzi wake wawili
19na kuwatuma kwa Bwana ili kumuuliza, “Wewe ndiwe yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”
20Wale watu walipofika kwa Yesu wakamwambia, “Yohana Mbatizaji ametutuma tukuulize, ‘Wewe ndiwe yule aliyekuwa aje, au tumtazamie mwingine?’ ”
21Wakati huo huo, Yesu aliwaponya wengi waliokuwa na magonjwa, maradhi na pepo wachafu, na pia akawafungua vipofu wengi macho wakapata kuona.
22Hivyo akawajibu wale wajumbe, “Rudini mkamwambie Yohana yote mnayoyaona na kuyasikia: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema.
23Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”
24Wajumbe wa Yohana walipoondoka, Yesu akaanza kusema na umati wa watu kuhusu Yohana Mbatizaji. Akawauliza, “Mlipoenda kule nyikani, mlienda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo?
25Kama sivyo, mlienda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya kifahari? La hasha! Watu wanaovaa mavazi ya kifahari na kuishi maisha ya anasa wako katika majumba ya kifalme.
26Lakini mlienda kuona nini? Mlienda kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii.
27Huyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa:
“ ‘Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,
atakayetengeneza njia mbele yako.’
28Nawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake, hakuna aliye mkuu kuliko Yohana. Lakini yeye aliye mdogo kabisa katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana.”
29(Watu wote, hata watoza ushuru, waliposikia maneno ya Yesu, walikubali kwamba mpango wa Mungu ni haki, maana walikuwa wamebatizwa na Yohana.
30Lakini Mafarisayo na wataalamu wa sheria walikataa mpango wa Mungu kwao kwa kutokubali kubatizwa na Yohana.)
31Yesu akawauliza, “Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Wanafanana na nini?
32Wao ni kama watoto waliokaa sokoni wakiitana wao kwa wao, wakisema:
“ ‘Tuliwapigia filimbi,
lakini hamkucheza;
tuliwaimbia nyimbo za maombolezo,
lakini hamkulia.’
33Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuja, alikuwa hali mkate wala hanywi divai, nanyi mkasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’
34Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nanyi mnasema: ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’
35Lakini hekima huthibitishwa kuwa kweli na watoto wake wote.”
36Basi Farisayo mmoja alimwalika Yesu kwake ale chakula. Hivyo Yesu akaenda nyumbani mwa yule Farisayo na kuketi mezani.
37Palikuwa na mwanamke mmoja katika mji ule aliyekuwa mwenye dhambi. Alipopata habari kwamba Yesu alikuwa akila chakula nyumbani mwa yule Farisayo, akaleta chupa ya marhamu yenye manukato.
38Yule mwanamke akasimama nyuma ya miguu ya Yesu akilia. Akailowanisha miguu yake kwa machozi yake, kisha akaifuta kwa nywele zake, akaibusu na kuimiminia manukato.
39Yule Farisayo aliyemwalika Yesu alipoona yanayotendeka, akawaza moyoni mwake, “Kama huyu mtu angekuwa nabii, angejua kwamba ni nani anayemgusa, na kwamba yeye ni mwanamke wa namna gani, na ya kuwa huyu mwanamke ni mwenye dhambi.”
40Yesu akamjibu, “Simoni, nina jambo la kukuambia.”
Simoni akajibu, “Mwalimu, sema.”
41“Palikuwa na mtu mmoja aliyewakopesha watu wawili fedha: Mmoja alidaiwa dinari mia tano na mwingine dinari hamsini.[#7:41 Dinari 500 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku mia tano.]
42Wote wawili walipokuwa hawawezi kulipa, aliyafuta madeni yao wote wawili. Sasa ni yupi kati yao atakayempenda zaidi yule aliyewasamehe?”
43Simoni akajibu, “Nadhani ni yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi.”
Naye Yesu akamwambia, “Umehukumu kwa usahihi.”
44Kisha akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, “Je, unamwona mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako, hukunipa maji ya kunawa miguu yangu, lakini huyu ameninawisha miguu kwa machozi yake, na kunifuta kwa nywele zake.
45Hukunisalimu kwa busu, lakini huyu mwanamke hajaacha kuibusu miguu yangu tangu nilipoingia.
46Hukunipaka mafuta kichwani mwangu, lakini yeye ameipaka miguu yangu manukato.
47Kwa hiyo, nakuambia, dhambi zake zilizokuwa nyingi zimesamehewa, kwani ameonesha upendo mwingi. Lakini yule aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo.”
48Kisha akamwambia yule mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.”
49Lakini wale waliokuwa wameketi pamoja naye chakulani wakaanza kusemezana wao kwa wao, “Huyu ni nani ambaye hata anasamehe dhambi?”
50Yesu akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”