Malaki 2

Malaki 2

Onyo kwa makuhani

1“Sasa onyo hili ni kwa ajili yenu, enyi makuhani.

2Kama hamtasikiliza, na kama hamtaki kuielekeza mioyo yenu kuheshimu Jina langu, nitatuma laana juu yenu, nami nitalaani baraka zenu. Naam, nimekwisha kuzilaani, kwa sababu hamkuielekeza mioyo yenu kuniheshimu mimi,” Asema Bwana wa majeshi.

3“Kwa sababu yenu nitawakatilia mbali wazao wenu. Nitazipaka nyuso zenu kinyesi, hicho kinyesi cha dhabihu zenu. Nanyi mtafukuzwa pamoja nazo mtoke mbele zangu.

4Nanyi mtajua kuwa nimewapelekea onyo hili ili agano langu na Lawi lipate kuendelea,” asema Bwana wa majeshi.

5“Agano langu lilikuwa pamoja naye, agano la uhai na amani, nami nilimpa yote, ili aniche na kuniheshimu, naye akaniheshimu na kusimama akilicha Jina langu.

6Fundisho la kweli lilikuwa kinywani mwake, wala hakuna uongo wowote uliopatikana katika midomo yake. Alitembea nami katika amani na unyofu, naye akawageuza wengi kutoka dhambini.

7“Kwa maana yapasa midomo ya kuhani kuhifadhi maarifa. Tena kutoka kinywani mwake watu wangepaswa kutafuta mafundisho, kwa sababu yeye ni mjumbe wa Bwana wa majeshi.

8Lakini mmegeuka mkaiacha njia, na kwa mafundisho yenu mmesababisha wengi kujikwaa. Mmevunja agano na Lawi,” asema Bwana wa majeshi.

9“Kwa hiyo nimewasababisha ninyi kudharauliwa na kufedheheshwa mbele ya watu wote, kwa sababu hamkufuata njia zangu, bali mmeonesha upendeleo katika mambo ya sheria.”

Yuda si mwaminifu

10Je, sote hatuna Baba mmoja? Hatukuumbwa na Mungu mmoja? Kwa nini basi tunalinajisi agano la baba zetu kwa kukosa uaminifu kila mmoja kwa mwenzake?

11Yuda amevunja uaminifu. Jambo la kuchukiza limetendeka katika Israeli na katika Yerusalemu: Yuda amepanajisi mahali patakatifu apendapo Bwana , kwa kuoa binti ya mungu mgeni.

12Kwa maana kwa mtu yeyote atendaye jambo hili, Bwana na amkatilie mbali kutoka mahema ya Yakobo, hata kama huwa anamletea Bwana wa majeshi sadaka.

13Kitu kingine mnachokifanya: Mnaifurikisha madhabahu ya Bwana kwa machozi. Mnalia na kuugua kwa sababu yeye haziangalii tena sadaka zenu wala hazikubali kwa furaha kutoka mikononi mwenu.

14Mnauliza, “Kwa nini?” Ni kwa sababu Bwana ni shahidi kati yako na mke wa ujana wako, kwa sababu umevunja uaminifu naye, ingawa yeye ni mwenzako, mke wa agano lako la ndoa.

15Je, Bwana hakuwafanya wao kuwa mmoja? Katika mwili na katika roho wao ni wa Mungu. Kwa nini wawe mmoja? Kwa sababu Mungu alikuwa akitafuta mzao mwenye kumcha Mungu. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, mtu asivunje uaminifu kwa mke wa ujana wake.

16“Ninachukia kuachana,” asema Bwana , Mungu wa Israeli, “pia nachukia mtu anayejivika jeuri kama vazi,” asema Bwana wa majeshi.

Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, wala msije mkavunja uaminifu.

Siku ya hukumu

17Mmemchosha Bwana kwa maneno yenu.

Nanyi mnauliza, “Tumemchosha kwa namna gani?”

Mmemchosha kwa kusema, “Wote watendao mabaya ni wema machoni pa Bwana , naye anapendezwa nao” au “Mungu wa haki yuko wapi?”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.