The chat will start when you send the first message.
1Wakati huo, wanafunzi wakamjia Yesu na kumuuliza, “Je, nani aliye mkuu kuliko wote katika ufalme wa mbinguni?”
2Yesu akamwita mtoto mdogo na kumsimamisha katikati yao.
3Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipoongoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika ufalme wa mbinguni.
4Kwa hiyo mtu yeyote anyenyekeaye kama huyu mtoto, ndiye aliye mkuu kuliko wote katika ufalme wa mbinguni.
5“Yeyote amkaribishaye mtoto mdogo kama huyu kwa Jina langu, anikaribisha mimi.
6“Lakini kama mtu yeyote akimsababisha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa katika kilindi cha bahari.
7“Ole kwa ulimwengu kwa sababu ya mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi! Mambo hayo lazima yawepo, lakini ole wake mtu yule ambaye huyasababisha.
8Ikiwa mkono wako au mguu wako unakusababisha utende dhambi, ukate na uutupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa huna mkono mmoja au mguu mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele.
9Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe, ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa katika moto wa Jehanamu.
10“Chungeni ili msimdharau mmoja wa hawa wadogo. Kwa maana nawaambia, malaika wao mbinguni daima wanauona uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [
11Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kuokoa kile kilichopotea.][#18:11 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.]
12“Mwaonaje? Ikiwa mtu ana kondoo mia moja, na mmoja wao akapotea, je, hatawaacha wale tisini na tisa vilimani na kwenda kumtafuta huyo mmoja aliyepotea?
13Naye akishampata, amin, nawaambia, hufurahi zaidi kwa ajili ya huyo kondoo mmoja kuliko wale tisini na tisa ambao hawakupotea.
14Vivyo hivyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmoja wa hawa wadogo apotee.
15“Ndugu yako akikukosea, nenda ukamwoneshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako.
16Lakini asipokusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno ‘lithibitishwe kwa ushahidi wa mashahidi wawili au watatu’.[#18:16 Kum 19:15]
17Akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa. Naye akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi awe kwenu kama mtu asiyeamini au mtoza ushuru.
18“Amin, nawaambia, lolote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.
19“Tena nawaambia, ikiwa wawili wenu watakubaliana duniani kuhusu jambo lolote watakaloomba, watatendewa na Baba yangu aliye mbinguni.
20Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”
21Kisha Petro akamwendea Yesu na kumuuliza, “Bwana, ni mara ngapi nimsamehe ndugu yangu akinikosea? Hadi mara saba?”
22Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.
23“Kwa hiyo ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme aliyetaka kufanya hesabu zake za fedha na watumishi wake.
24Alipoanza kufanya hesabu zake, mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta elfu kumi aliletwa kwake.[#18:24 Talanta moja ni sawa na mshahara wa kibarua wa miaka 15.]
25Kwa kuwa alikuwa hawezi kulipa deni hilo, bwana wake akaamuru kwamba auzwe, yeye, mkewe, watoto wake na vyote alivyokuwa navyo, ili lile deni lipate kulipwa.
26“Yule mtumishi akampigia magoti, akamsihi yule bwana akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’
27Yule bwana wa huyo mtumishi akamwonea huruma, akafuta deni lake lote, akamwacha aende zake.
28“Lakini yule mtumishi alipokuwa anatoka nje, akakutana na mtumishi mwenzake aliyekuwa amemkopesha dinari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akimwambia, ‘Nilipe kile ninachokudai!’[#18:28 Dinari moja ilikuwa kama mshahara wa kibarua wa siku moja.]
29“Yule mtumishi mwenzake akapiga magoti akamsihi akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’
30“Lakini akakataa. Badala yake, alienda akamtupa gerezani hata atakapolipa hilo deni.
31Watumishi wenzake walipoona haya yaliyotukia wakaudhika sana, nao wakaenda na kumwambia bwana wao kila kitu kilichokuwa kimetukia.
32“Yule bwana akamwita yule mtumishi akamwambia, ‘Wewe mtumishi mwovu! Mimi nilikusamehe deni lako lote uliponisihi.
33Je, haikukupasa kumhurumia mtumishi mwenzako kama mimi nilivyokuhurumia wewe?’
34Kwa hasira, yule bwana wake akamtia yule mtumishi mikononi mwa askari wa gereza ili ateswe hadi atakapolipa yote aliyokuwa anadaiwa.
35“Hivi ndivyo Baba yangu wa mbinguni atakavyomfanyia kila mmoja wenu ikiwa hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni mwake.”