Marko 10

Marko 10

Safari ya kwenda Yerusalemu na matukio mjini

Yesu afundisha kuhusu talaka

(Mt 19:1‑12; Lk 16:18)

1Yesu akaondoka huko, akavuka Mto Yordani, akaenda sehemu za Yudea. Umati mkubwa wa watu wakaenda kwake tena, naye akawafundisha, kama ilivyokuwa desturi yake.

2Baadhi ya Mafarisayo wakaja ili kumjaribu kwa kumuuliza, “Je, ni halali mtu kumwacha mke wake?”

3Yesu akawajibu, “Je, Musa aliwaamuru nini?”

4Wakajibu, “Musa aliruhusu kwamba mume anaweza kumwandikia mkewe hati ya talaka na kumwacha.”

5Yesu akawaambia, “Musa aliwaandikia sheria hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu.

6Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke’.[#10:6 Mwa 1:27]

7‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe,

8na hao wawili watakuwa mwili mmoja.’ Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena, bali mwili mmoja.[#10:8 Mwa 2:24]

9Basi, alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”

10Walipokuwa tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza kuhusu jambo hili.

11Akawajibu, “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kuoa mke mwingine, anazini naye.

12Naye mwanamke amwachaye mumewe na kuolewa na mume mwingine, anazini.”

Yesu awabariki watoto wadogo

(Mt 19:13‑15; Lk 18:15‑17)

13Watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wake wakawakemea.

14Yesu alipoona yaliyokuwa yakitukia, akachukizwa. Akawaambia wanafunzi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa.

15Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”

16Akawachukua watoto mikononi mwake, akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.

Kijana tajiri

(Mt 19:16‑30; Lk 18:18‑30)

17Yesu alipokuwa anaondoka, mtu mmoja akamkimbilia, akapiga magoti mbele yake, akamuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

18Yesu akamwambia, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake.

19Unazijua amri: ‘Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.’”[#10:19 Kut 20:12‑16; Kum 5:16‑20]

20Akamjibu, “Mwalimu, amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”

21Yesu akamtazama na kumpenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

22Yule mtu aliposikia hayo, akasikitika sana. Akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

23Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Itakuwa vigumu sana kwa wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!”

24Wanafunzi wake wakashangazwa sana na maneno hayo. Lakini Yesu akawaambia tena, “Wanangu, tazama jinsi ilivyo vigumu kwa wale wanaotumainia mali kuingia katika ufalme wa Mungu.

25Ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”

26Wanafunzi wake wakashangaa sana. Wakaulizana wao kwa wao, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”

27Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu sivyo. Mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”

28Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha kila kitu na kukufuata wewe!”

29Yesu akasema, “Amin, nawaambia, hakuna mtu yeyote aliyeacha nyumba, ndugu wa kiume au wa kike, au mama au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili,

30ambaye hatalipwa mara mia katika ulimwengu huu: nyumba, ndugu wa kiume na wa kike, mama na baba na watoto, mashamba pamoja na mateso, kisha uzima wa milele katika ulimwengu ujao.

31Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na wa mwisho watakuwa wa kwanza.”

Yesu atabiri tena kifo chake

(Mt 20:17‑19; Lk 18:31‑34)

32Walikuwa njiani wakipanda kwenda Yerusalemu, na Yesu alikuwa amewatangulia. Wanafunzi wake walishangaa, nao watu waliowafuata walijawa na hofu. Yesu akawachukua tena wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia yatakayompata.

33Akasema, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atasalitiwa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Wao watamhukumu kifo na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa,

34ambao watamdhihaki na kumtemea mate, watampiga na kumuua. Siku tatu baadaye atafufuka.”

Ombi la Yakobo na Yohana

(Mt 20:20‑28)

35Kisha Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakaja kwake na kumwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie lolote tutakalokuomba.”

36Naye akawaambia, “Je, mwataka niwafanyie jambo gani?”

37Wakamwambia, “Tupe kukaa mmoja upande wako wa kuume na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wako.”

38Lakini Yesu akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?”

39Wakajibu, “Tunaweza.”

Kisha Yesu akawaambia, “Kikombe nikinyweacho mtakinywea na ubatizo nibatizwao mtabatizwa,

40lakini kuketi mkono wangu wa kuume au wa kushoto si juu yangu mimi kuwapa. Nafasi hizi ni kwa ajili ya wale walioandaliwa.”

41Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana.

42Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa wale wanaodhaniwa kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu, nao wenye vyeo huonesha mamlaka yao.

43Lakini isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu,

44na yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa mtumwa wa wote.

45Kwa kuwa hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

Yesu amponya kipofu Bartimayo

(Mt 20:29‑34; Lk 18:35‑43)

46Kisha wakafika Yeriko. Yesu alipokuwa akiondoka mjini na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu mmoja, jina lake Bartimayo (maana yake “mwana wa Timayo”), alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada.

47Aliposikia kuwa ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita, akaanza kupaza sauti akisema, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!”

48Watu wengi wakamkemea, wakamwambia akae kimya, lakini yeye akazidi kupaza sauti, akisema, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”

49Yesu akasimama na kusema, “Mwiteni.”

Hivyo wakamwita yule mtu kipofu, wakamwambia, “Jipe moyo! Inuka, anakuita.”

50Akiwa analivua lile joho lake, alisimama na kumwendea Yesu.

51Yesu akamuuliza, “Unataka nikufanyie nini?”

Yule kipofu akajibu, “Mwalimu, nataka kuona.”

52Yesu akamwambia, “Nenda zako, imani yako imekuponya.” Mara akapata kuona, akamfuata Yesu njiani.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.