Marko 16

Marko 16

Yesu afufuka

(Mt 28:1‑8; Lk 24:1‑12; Yn 20:1‑10)

1Sabato ilipomalizika, Mariamu Magdalene, Mariamu mama yake Yakobo, na Salome walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu.

2Asubuhi na mapema, siku ya kwanza ya juma, mara tu baada ya kuchomoza jua, walienda kaburini.

3Njiani wakawa wanaulizana wao kwa wao, “Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe kutoka ingilio la kaburi?”

4Lakini walipotazama, wakaona lile jiwe, ambalo lilikuwa kubwa sana, limekwisha kuvingirishwa kutoka pale penye ingilio la kaburi.

5Walipokuwa wakiingia mle kaburini, wakamwona kijana mmoja aliyevaa joho jeupe akiwa ameketi upande wa kuume, nao wakastaajabu.

6Yule malaika akawaambia, “Msistaajabu. Mnamtafuta Yesu, Mnazareti, aliyesulubiwa. Amefufuka! Hayuko hapa. Tazameni mahali walipomlaza.

7Lakini nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro, kwamba, ‘Anawatangulia kwenda Galilaya. Mtamwona huko kama alivyowaambia.’ ”

8Hivyo wakatoka, wakakimbia kutoka mle kaburini wakiwa na hofu kuu na mshangao. Nao hawakumwambia mtu yeyote neno lolote, kwa sababu waliogopa.

Yesu amtokea Mariamu Magdalene

(Mt 28:9‑10; Yn 20:11‑18)

[

9Yesu alipofufuka alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, aliyekuwa amemtoa pepo wachafu saba.[#16:9 Maandiko mengine ya kale hayana sehemu ya Mk 16:9‑20.]

10Mariamu akaenda, naye akawaambia wale waliokuwa wamefuatana na Yesu, waliokuwa wanaomboleza na kulia.

11Lakini waliposikia kwamba Yesu yu hai na kwamba Mariamu alikuwa amemwona, hawakusadiki.

Yesu awatokea wanafunzi wawili

(Lk 24:13‑35)

12Baadaye Yesu akawatokea wawili miongoni mwa wanafunzi wake walipokuwa wakienda shambani akiwa katika sura nyingine.

13Nao wakarudi na kuwaambia wenzao. Lakini hawakuwasadiki wao pia.

Yesu awatuma wanafunzi wake

(Mt 28:16‑20; Lk 24:36‑49; Yn 20:19‑23; Mdo 1:6‑8)

14Baadaye Yesu akawatokea wale wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa wakila chakula. Akawakemea kwa kutoamini kwao na kwa ugumu wa mioyo yao kwa kutosadiki wale waliomwona baada yake kufufuka.

15Akawaambia, “Nendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.

16Yeyote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa.

17Nazo ishara hizi zitafuatana na wanaoamini: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu; watasema kwa lugha mpya;

18watashika nyoka kwa mikono yao; na hata wakinywa kitu chochote cha kuua, hakitawadhuru kamwe; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.”

Yesu apaa mbinguni

(Lk 24:50‑53; Mdo 1:9‑11)

19Baada ya Bwana Yesu kusema nao, alichukuliwa juu mbinguni na kuketi mkono wa kuume wa Mungu.

20Kisha wanafunzi wake wakatoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana akatenda kazi pamoja nao na kulithibitisha neno lake kwa ishara zilizofuatana nalo.]

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.