Marko 7

Marko 7

Mapokeo ya wazee

(Mt 15:1‑20)

1Mafarisayo na baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu wakakusanyika mbele ya Yesu.

2Wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula kwa mikono iliyo najisi, yaani bila kunawa kama ilivyotakiwa na sheria ya dini ya Wayahudi.

3(Kwa kuwa Mafarisayo na Wayahudi wote hawali chakula pasipo kunawa kwa kufuata desturi za wazee wao.

4Wanapotoka sokoni hawawezi kula pasipo kunawa. Pia kuna desturi zingine nyingi wanazofuata kama vile jinsi ya kuosha vikombe, vyungu na vyombo vya shaba.)

5Hivyo, wale Mafarisayo na walimu wa sheria wakamuuliza Yesu, “Mbona wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, na badala yake wanakula kwa mikono najisi?”

6Yesu akawajibu, “Nabii Isaya alisema ukweli alipotabiri juu yenu, ninyi wanafiki. Kama ilivyoandikwa:

“ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,

lakini mioyo yao iko mbali nami.

7Huniabudu bure,

nayo mafundisho yao ni maagizo ya wanadamu tu.’

8Ninyi mmeziacha amri za Mungu na kushika desturi za watu.”

9Naye akawaambia, “Ninyi mnayo njia nzuri ya kukataa amri za Mungu ili mpate kuyashika mapokeo yenu!

10Kwa mfano, Musa alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Yeyote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’[#7:10 Kut 20:12; Kum 5:16; #7:10 Kut 21:17; Law 20:9]

11Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia ni Korbani’ (yaani kimewekwa wakfu kwa Mungu),

12basi hawajibiki tena kumsaidia baba yake au mama yake.

13Kwa njia hiyo ninyi mnabatilisha neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyojiwekea. Nanyi mnafanya mambo mengi ya aina hiyo.”

Vitu vinavyomnajisi mtu

(Mt 15:10‑20)

14Yesu akaita tena umati ule wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni nyote, na mwelewe jambo hili.

15Hakuna kitu kinachomwingia mtu kimtiacho unajisi, lakini kile kimtokacho ndicho kimtiacho unajisi. [

16Kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia na asikie.]”[#7:16 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.]

17Baada ya Yesu kuacha ule umati wa watu na kuingia ndani, wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano ule.

18Akawajibu, “Je, hata nanyi hamwelewi? Je, hamfahamu kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi?

19Mtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni, na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Yesu alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni safi.)

20Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi.

21Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi,

22tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu.

23Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”

Imani ya mwanamke Myunani

(Mt 15:21‑28)

24Ndipo Yesu akaondoka hapo akaenda sehemu za Tiro. Akaingia katika nyumba moja, naye hakutaka mtu yeyote ajue kwamba yuko humo. Lakini hakuweza kujificha.

25Mara mwanamke mmoja, ambaye binti yake mdogo alikuwa na pepo mchafu, akaja na kumpigia magoti miguuni pake.

26Basi huyo mwanamke alikuwa Myunani, aliyezaliwa Foinike ya Siria. Akamsihi Yesu amtoe binti yake huyo pepo mchafu.

27Yesu akamwambia, “Waache watoto washibe kwanza, kwa maana si vyema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”

28Lakini yule mwanamke akamjibu, “Bwana, hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya chakula cha watoto.”

29Ndipo Yesu akamjibu, “Kwa sababu ya jibu lako, nenda zako nyumbani; yule pepo mchafu amemtoka binti yako.”

30Akaenda zake nyumbani akamkuta binti yake amelala kitandani, yule pepo mchafu akiwa amemtoka.

Yesu amponya mtu aliyekuwa kiziwi na bubu

31Kisha Yesu akaondoka sehemu za Tiro, akapita katikati ya Sidoni, hadi Bahari ya Galilaya na kuingia eneo la Dekapoli.

32Huko, watu wakamletea Yesu mtu mmoja kiziwi, ambaye pia alikuwa na kigugumizi, wakamwomba aweke mkono wake juu ya huyo mtu.

33Yesu akampeleka yule kiziwi kando, mbali na watu, akatia vidole vyake masikioni mwa yule mtu. Kisha akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu.

34Ndipo Yesu akatazama mbinguni, akashusha pumzi kwa nguvu, akamwambia, “Efatha!” (yaani, “Funguka!”)

35Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukaachiliwa, akaanza kuongea sawasawa.

36Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hizi. Lakini kadiri alivyowakanya, ndivyo walivyozidi kutangaza kwa bidii.

37Walistaajabu mno. Wakasema, “Amefanya mambo yote vizuri mno! Amewawezesha viziwi wasikie na bubu waseme!”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.