The chat will start when you send the first message.
1Neno la unabii kuhusu Ninawi. Kitabu cha maono cha Nahumu Mwelkoshi.
2Bwana ni mwenye wivu na Mungu mlipiza kisasi;
Bwana hulipiza kisasi na amejaa ghadhabu.
Bwana hulipiza kisasi juu ya watesi wake,
naye anadumisha ghadhabu yake dhidi ya adui zake.
3Bwana si mwepesi wa hasira naye ni mwenye nguvu,
Bwana hataacha kuadhibu wenye hatia.
Njia yake ipo katika kisulisuli na tufani,
na mawingu ni vumbi la miguu yake.
4Anakemea bahari na kuikausha,
anafanya mito yote kukauka.
Bashani na Karmeli zinanyauka
na maua ya Lebanoni hukauka.
5Milima hutikisika mbele yake
na vilima huyeyuka.
Nchi hutetemeka mbele yake,
dunia na wote wanaoishi ndani yake.
6Ni nani awezaye kuzuia hasira yake yenye uchungu?
Nani awezaye kuvumilia hasira yake kali?
Ghadhabu yake imemiminwa kama moto,
na miamba inapasuka mbele zake.
7Bwana ni Mwema,
kimbilio wakati wa taabu.
Huwatunza wale wanaomtegemea,
8lakini kwa mafuriko makubwa,
ataangamiza Ninawi;
atafuatilia adui zake hadi gizani.
9Kila njama wanayopanga dhidi ya Bwana
yeye atalikomesha;
taabu haitatokea mara ya pili.
10Watasongwa katikati ya miiba
na kulewa kwa mvinyo wao.
Watateketezwa kama mabua makavu.
11Ee Ninawi, kutoka kwako amejitokeza mmoja,
ambaye anapanga njama
dhidi ya Bwana
na kushauri uovu.
12Hili ndilo asemalo Bwana :
“Ingawa wana muungano nao ni wengi sana,
watakatiliwa mbali na kuangamia.
Ingawa nimekutesa wewe, ee Yuda,
sitakutesa tena.
13Sasa nitavunja nira zao kutoka shingo yako,
nami nitazivunjilia mbali pingu zako.”
14Hii ndiyo amri Bwana aliyoitoa kukuhusu wewe, Ninawi:
“Hutakuwa na wazao
watakaoendeleza jina lako.
Nitaharibu sanamu za kuchonga na sanamu za kusubu
zilizopo katika hekalu la miungu yenu.
Nitaandaa kaburi lako,
kwa maana wewe ni mwovu kabisa.”
15Tazama, huko juu milimani,
miguu ya huyo mmoja aletaye habari njema,
ambaye anatangaza amani!
Ee Yuda, sherehekea sikukuu zako,
nawe utimize nadhiri zako.
Waovu hawatakuvamia tena;
wataangamizwa kabisa.