The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Musa,
2“Sema na Waisraeli, na ujipatie fimbo kumi na mbili kutoka kwao, moja kutoka kwa kila mmoja wa viongozi wa makabila ya baba zao. Andika jina la kila mtu kwenye fimbo yake.
3Kwenye fimbo ya Lawi andika jina la Haruni, kwa maana ni lazima iwepo fimbo moja kwa kila kiongozi kwa ajili ya kila kabila la baba zao.
4Ziweke hizo fimbo ndani ya Hema la Kukutania mbele ya Sanduku la Ushuhuda, mahali nikutanapo nawe.
5Fimbo ya mtu nitakayemchagua itachipuka, nami mwenyewe nitayakomesha haya manungʼuniko ya mara kwa mara ya Waisraeli dhidi yako.”
6Hivyo Musa akasema na Waisraeli, nao viongozi wao wakampa fimbo kumi na mbili, fimbo moja kwa ajili ya kila kabila la baba zao, nayo fimbo ya Haruni ikiwa miongoni mwa hizo.
7Musa akaziweka hizo fimbo mbele za Bwana ndani ya Hema la Ushuhuda.
8Siku iliyofuata Musa aliingia kwenye Hema la Ushuhuda akaona ile fimbo ya Haruni ambayo iliwakilisha jamaa ya Lawi haikuwa tu imechipuka, bali pia ilikuwa imetoa machipukizi, kuchanua maua na kuzaa malozi.
9Ndipo Musa akaleta zile fimbo zote kwa Waisraeli wote kutoka mbele za Bwana . Wakaziangalia, na kila mtu akaichukua fimbo yake mwenyewe.
10Bwana akamwambia Musa, “Rudisha fimbo ya Haruni mbele ya Sanduku la Ushuhuda, ili ihifadhiwe kama alama kwa waasi. Hili litakomesha manungʼuniko yao dhidi yangu, ili wasife.”
11Musa akafanya kama Bwana alivyomwamuru.
12Waisraeli wakamwambia Musa, “Tutakufa! Tumepotea, sote tumepotea!
13Yeyote akaribiaye Maskani ya Bwana atakufa. Je, sisi sote tutakufa?”