The chat will start when you send the first message.
1Basi Wareubeni na Wagadi, waliokuwa na makundi makubwa ya ngʼombe, kondoo na mbuzi, waliona kuwa nchi ya Yazeri na nchi ya Gileadi ni nzuri kwa mifugo.
2Hivyo walimjia Musa, na kuhani Eleazari na viongozi wa jumuiya, na kuwaambia,
3“Atarothi, Diboni, Yazeri, Nimra, Heshboni, Eleale, Sebamu, Nebo na Beoni,
4nchi ambayo Bwana ameishinda mbele ya Waisraeli, inafaa kwa mifugo, nao watumishi wako wana mifugo.
5Kama tumepata kibali mbele ya macho yako, nchi hii na ipewe watumishi wako kama milki yetu. Usitufanye tuvuke Yordani.”
6Musa akawaambia Wagadi na Wareubeni, “Je, watu wa nchi yenu wataenda vitani wakati ninyi mmeketi hapa?
7Kwa nini mmewakatisha Waisraeli tamaa wasivuke katika nchi ambayo Bwana amewapa?
8Hivi ndivyo baba zenu walivyofanya wakati nilipowatuma kutoka Kadesh-Barnea kuipeleleza nchi.
9Baada ya kufika kwenye Bonde la Eshkoli na kuitazama nchi, waliwakatisha tamaa Waisraeli wasiingie katika nchi ambayo Bwana alikuwa amewapa.
10Siku ile hasira ya Bwana iliwaka naye akaapa kiapo hiki:
11‘Kwa kuwa hawakunifuata kwa moyo wote, hakuna mtu yeyote mwenye miaka ishirini au zaidi ambaye alikuja kutoka Misri atakayeona nchi niliyoahidi kwa kiapo kwa Abrahamu, Isaka na Yakobo;
12hakuna hata mmoja isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni, kwa sababu walimfuata Bwana kwa moyo wote.’
13Hasira ya Bwana iliwaka dhidi ya Waisraeli na akawafanya watangetange katika jangwa kwa miaka arobaini, hadi kizazi chote cha wale waliofanya maovu mbele yake kimeangamia.
14“Nanyi mko hapa, uzao wa wenye dhambi, mkisimamia mahali pa baba zenu na mkimfanya Bwana kuwakasirikia Waisraeli hata zaidi.
15Mkigeuka na kuacha kumfuata, atawaacha tena watu hawa wote jangwani, na mtakuwa sababu ya maangamizi yao.”
16Ndipo wakamjia Musa na kumwambia, “Tungetaka kujenga mazizi hapa kwa ajili ya mifugo yetu na miji kwa ajili ya wanawake wetu na watoto.
17Lakini sisi tuko tayari kuchukua silaha zetu na kutangulia mbele ya Waisraeli hadi tutakapowaleta mahali pao. Wakati huo wanawake wetu na watoto wataishi katika miji yenye ngome, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya wenyeji wa nchi.
18Hatutarudi nyumbani mwetu hadi kila Mwisraeli apokee urithi wake.
19Hatutapokea urithi wowote pamoja nao ngʼambo ya Yordani, kwa sababu urithi wetu umekuja kwetu upande wa mashariki mwa Yordani.”
20Kisha Musa akawaambia, “Kama mtafanya jambo hili, kama mtajivika silaha mbele za Bwana kwa ajili ya vita,
21na kama ninyi nyote mtaenda mmejivika silaha ngʼambo ya Yordani mbele za Bwana hadi awe amewafukuza adui zake mbele zake,
22hadi wakati nchi itakapokuwa imeshindwa mbele za Bwana , ndipo mtaweza kurudi na kuwa huru kutoka masharti yenu kwa Bwana na Israeli. Nayo nchi hii itakuwa milki yenu mbele za Bwana .
23“Lakini mkishindwa kufanya hili, mtakuwa mnatenda dhambi dhidi ya Bwana ; nanyi kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata.
24Jengeni miji kwa ajili ya wanawake na watoto wenu, na mazizi kwa ajili ya mbuzi na kondoo wenu, lakini fanyeni yale mliyoahidi.”
25Wagadi na Wareubeni wakamwambia Musa, “Sisi watumishi wako tutafanya kama bwana wetu anavyotuagiza.
26Watoto na wake zetu, makundi ya mbuzi na kondoo, na makundi ya ngʼombe wetu, watabaki hapa katika miji ya Gileadi.
27Lakini watumishi wenu, kila mwanaume aliyevaa silaha za vita, watavuka ngʼambo kupigana mbele za Bwana , sawa kama bwana wetu asemavyo.”
28Kisha Musa akatoa amri kuwahusu kwa kuhani Eleazari, na Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa za makabila ya Israeli.
29Musa akawaambia, “Ikiwa Wagadi na Wareubeni, kila mwanaume aliyevaa silaha za vita, atavuka Yordani pamoja nanyi mbele za Bwana , basi mtakapoishinda nchi iliyo mbele yenu, wapeni nchi ya Gileadi kama milki yao.
30Lakini kama hawatavuka pamoja nanyi wakiwa wamevaa silaha za vita, lazima wakubali kupokea milki yao pamoja nanyi katika nchi ya Kanaani.”
31Wagadi na Wareubeni wakajibu, “Watumishi wako watafanya lile Bwana alilosema.
32Tutavuka mbele za Bwana kuingia Kanaani tukiwa tumevaa silaha za vita, lakini mali tutakayoirithi itakuwa ngʼambo hii ya Yordani.”
33Kisha Musa akawapa Wagadi, Wareubeni, na nusu ya kabila la Manase mwana wa Yusufu ufalme wa Sihoni mfalme wa Waamori, na ufalme wa Ogu mfalme wa Bashani, nchi yote pamoja na miji yake, na nchi inayowazunguka.
34Wagadi wakajenga Diboni, Atarothi, Aroeri,
35Atroth-Shofani, Yazeri, Yogbeha,
36Beth-Nimra na Beth-Harani kama miji iliyozungushiwa ngome, tena wakajenga mazizi kwa ajili ya makundi yao ya mbuzi na kondoo.
37Nao Wareubeni wakajenga upya miji ya Heshboni, Eleale na Kiriathaimu,
38pia Nebo na Baal-Meoni (majina ya hiyo miji yalibadilishwa) na Sibma. Miji waliyoijenga upya waliipa majina.
39Wazao wa Makiri mwana wa Manase walienda Gileadi, wakaiteka nchi na kuwafukuza Waamori waliokuwa huko.
40Kwa hiyo Musa akawapa Wamakiri, wazao wa Manase, nchi ya Gileadi, nao wakakaa huko.
41Yairi, mzao wa Manase, akateka makazi yao, akayaita Hawoth-Yairi.
42Naye Noba akateka Kenathi na makazi yaliyoizunguka, akayaita Noba kwa jina lake.