The chat will start when you send the first message.
1Msifuni Mwenyezi Mungu.[#111:1 kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.]
Nitamtukuza Mwenyezi Mungu kwa moyo wangu wote,
katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko.
2Kazi za Mwenyezi Mungu ni kuu,
wote wanaopendezwa nazo huzitafakari.
3Kazi zake zimejaa fahari na utukufu,
haki yake hudumu daima.
4Amefanya maajabu yake yakumbukwe,
Mwenyezi Mungu ni mwenye neema na huruma.
5Huwapa chakula wale wanaomcha,
hulikumbuka agano lake milele.
6Amewaonesha watu wake uwezo wa kazi zake,
akiwapa nchi za mataifa mengine.
7Kazi za mikono yake ni za uaminifu na haki,
mausia yake yote ni ya kuaminika.
8Zinadumu milele na milele,
zikifanyika kwa uaminifu na unyofu.
9Aliwapa watu wake ukombozi,
aliamuru agano lake milele:
jina lake ni takatifu na la kuogopwa.
10Kumcha Mwenyezi Mungu ndicho chanzo cha hekima,
wote wanaozifuata amri zake wana busara.
Sifa zake zadumu milele.