Zaburi 119

Zaburi 119

Zaburi 119

Sifa za Torati ya Mwenyezi Mungu

1Heri wale walio waadilifu katika njia zao,

wanaoenenda katika Torati ya Mwenyezi Mungu.

2Heri wale wanaozishika shuhuda zake,

wanaomtafuta kwa moyo wao wote.

3Wasiofanya lolote lililo baya,

wanaoenenda katika njia zake.

4Umetoa maagizo yako

ili tuyatii kwa ukamilifu.

5Laiti mwenendo wangu ungekuwa imara

katika kuyatii maagizo yako!

6Hivyo mimi sitaaibishwa

ninapozingatia amri zako zote.

7Nitakusifu kwa moyo mnyofu

ninapojifunza sheria zako za haki.

8Nitayatii maagizo yako;

usiniache kabisa.

9Kijana aisafishe njia yake jinsi gani?

Ni kwa kutii, akilifuata neno lako.

10Ninakutafuta kwa moyo wangu wote,

usiniache niende mbali na amri zako.

11Nimelificha neno lako moyoni mwangu

ili nisikutende dhambi.

12Uhimidiwe, Ee Mwenyezi Mungu;

nifundishe maagizo yako.

13Kwa midomo yangu nitasimulia sheria zote

zinazotoka katika kinywa chako.

14Ninafurahia kufuata sheria zako

kama mtu afurahiaye mali nyingi.

15Ninatafakari maagizo yako

na kuziangalia njia zako.

16Ninafurahia maagizo yako,

wala sitalipuuza neno lako.

17Mtendee mema mtumishi wako, nami nitaishi;

nitalitii neno lako.

18Yafungue macho yangu nipate kuona

mambo ya ajabu katika sheria yako.

19Mimi ni mgeni duniani,

usinifiche amri zako.

20Nafsi yangu inataabika kwa shauku kubwa

kwa sheria zako wakati wote.

21Unawakemea wenye majivuno, waliolaaniwa,

wanaoenda mbali na amri zako.

22Niondolee dharau na dhihaka,

kwa kuwa ninazishika sheria zako.

23Ingawa watawala huketi pamoja na kunisingizia,

mtumishi wako atatafakari juu ya maagizo yako.

24Sheria zako ni furaha yangu,

nazo ni washauri wangu.

25Nimelazwa chini mavumbini,

yahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako.

26Nilikueleza njia zangu ukanijibu,

nifundishe sheria zako.

27Nijulishe mafundisho ya mausia yako,

nami nitatafakari maajabu yako.

28Nafsi yangu imechakazwa kwa huzuni,

uniimarishe sawasawa na neno lako.

29Niepushe na njia za udanganyifu,

kwa neema unifundishe sheria zako.

30Nimechagua njia ya kweli,

nimekaza moyo wangu katika sheria zako.

31Nimeng’ang’ania sheria zako, Ee Mwenyezi Mungu,

usiniache niaibishwe.

32Nakimbilia katika njia ya maagizo yako,

kwa kuwa umeuweka moyo wangu huru.

33Ee Mwenyezi Mungu, nifundishe kuyafuata maagizo yako,

nami nitayashika hadi mwisho.

34Nipe ufahamu, nami nitaishika sheria yako

na kuitii kwa moyo wangu wote.

35Niongoze kwenye njia ya amri zako,

kwa kuwa huko napata furaha.

36Ugeuze moyo wangu kuelekea sheria zako,

na siyo kwenye mambo ya ubinafsi.

37Geuza macho yangu kutoka mambo yasiyofaa,

uyahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako.

38Mtimizie mtumishi wako ahadi yako,

ili upate kuogopwa.

39Niondolee aibu ninayoiogopa,

kwa kuwa sheria zako ni njema.

40Tazama jinsi ninavyoonea shauku mausia yako!

Hifadhi maisha yangu katika haki yako.

41Ee Mwenyezi Mungu, upendo wako usiokoma unijie,

wokovu wako sawasawa na ahadi yako,

42ndipo nitakapomjibu anayenidhihaki,

kwa kuwa ninalitumainia neno lako.

43Usilinyakue neno la kweli kutoka kinywani mwangu,

kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika amri zako.

44Nitaitii amri yako daima,

naam, milele na milele.

45Nitatembea huru,

kwa kuwa nimejifunza mausia yako.

46Nitasema sheria zako mbele za wafalme

wala sitaaibishwa,

47kwa kuwa ninazifurahia amri zako

kwa sababu ninazipenda.

48Ninaziinulia amri zako ambazo ninazipenda mikono yangu,

nami ninatafakari juu ya maagizo yako.

49Kumbuka neno lako kwa mtumishi wako,

kwa sababu umenipa tumaini.

50Faraja yangu katika mateso yangu ni hii:

Ahadi yako inahifadhi maisha yangu.

51Wenye majivuno wamenisimanga bila kuchoka,

hata hivyo sitaiacha sheria yako.

52Ee Mwenyezi Mungu, ninazikumbuka sheria zako za zamani,

nazo zinanifariji.

53Nimeshikwa sana na ghadhabu kwa ajili ya waovu,

ambao wameacha sheria yako.

54Maagizo yako ni kiini cha nyimbo zangu

popote ninapoishi.

55Ee Mwenyezi Mungu, wakati wa usiku ninalikumbuka jina lako,

nami nitatii sheria yako.

56Hili limekuwa zoezi langu:

nami ninayatii mausia yako.

57Ee Mwenyezi Mungu, wewe ni fungu langu,

nimeahidi kuyatii maneno yako.

58Nimetafuta uso wako kwa moyo wangu wote,

nihurumie sawasawa na ahadi yako.

59Nimezifikiri njia zangu

na nimeelekeza hatua zangu katika mausia yako.

60Nitafanya haraka bila kuchelewa

kuzitii amri zako.

61Hata waovu wanifunge kwa kamba,

sitasahau sheria yako.

62Usiku wa manane ninaamka kukushukuru

kwa sababu ya sheria zako za haki.

63Mimi ni rafiki kwa wale wote wanaokucha,

kwa wote wanaofuata mausia yako.

64Ee Mwenyezi Mungu, dunia imejaa upendo wako,

nifundishe maagizo yako.

65Mtendee wema mtumishi wako

Ee Mwenyezi Mungu, sawasawa na neno lako.

66Nifundishe maarifa na uamuzi mzuri,

kwa kuwa ninaamini amri zako.

67Kabla sijapata shida nilipotea njia,

lakini sasa ninalitii neno lako.

68Wewe ni mwema, unalotenda ni jema,

nifundishe maagizo yako.

69Ingawa wenye majivuno wamenisingizia uongo,

nitafuata mausia yako kwa moyo wangu wote.

70Mioyo yao ni katili na migumu,

bali mimi napendezwa na sheria yako.

71Ilikuwa vyema mimi kupata shida

ili nipate kujifunza maagizo yako.

72Sheria inayotoka kinywani mwako ina thamani kubwa kwangu

kuliko maelfu ya vipande vya fedha na dhahabu.

73Mikono yako iliniumba na kunitengeneza,

nipe ufahamu niweze kujifunza amri zako.

74Wale wanaokucha na wafurahie wanaponiona,

kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika neno lako.

75Ee Mwenyezi Mungu, ninajua kwamba sheria zako ni za haki,

katika uaminifu wako umeniadhibu.

76Upendo wako usiokoma uwe faraja yangu,

sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako.

77Huruma yako na inijie ili nipate kuishi,

kwa kuwa naifurahia sheria yako.

78Wenye majivuno na waaibishwe kwa kunikosea mimi bila sababu,

lakini mimi nitatafakari juu ya mausia yako.

79Wale wanaokucha na wanigeukie mimi,

hao ambao wanazielewa sheria zako.

80Moyo wangu usiwe na lawama katika kutii maagizo yako,

ili nisiaibishwe.

81Nafsi yangu inazimia kwa kutamani wokovu wako,

lakini nimeweka tumaini langu katika neno lako.

82Macho yangu yamefifia, nikingoja ahadi yako;

ninasema, “Utanifariji lini?”

83Ingawa nimekuwa kama kiriba kwenye moshi,

bado sijasahau maagizo yako.

84Mtumishi wako itampasa angoje hadi lini?

Ni lini utawaadhibu washtaki wangu?

85Wenye majivuno wananichimbia mashimo,

kinyume na sheria yako.

86Amri zako zote ni za kuaminika;

unisaidie, kwa sababu watu wananishtaki bila sababu.

87Walikaribia kabisa kunifuta kutoka uso wa dunia,

lakini sijaacha mausia yako.

88Yahifadhi maisha yangu sawasawa na upendo wako,

nami nitatii sheria za kinywa chako.

89Ee Mwenyezi Mungu, neno lako ni la milele,

linasimama imara mbinguni.

90Uaminifu wako unaendelea kwa vizazi vyote,

umeiumba dunia, nayo inadumu.

91Sheria zako zinadumu hadi leo,

kwa kuwa vitu vyote vinakutumikia.

92Kama nisingefurahia sheria yako,

ningeangamia katika taabu zangu.

93Sitasahau mausia yako kamwe,

kwa maana kwayo umehifadhi maisha yangu.

94Uniokoe, kwa maana mimi ni wako,

kwa kuwa nimetafuta mausia yako.

95Waovu wanangojea kuniangamiza,

bali mimi ninatafakari sheria zako.

96Katika ukamilifu wote ninaona mna kikomo,

lakini amri zako hazina mwisho.

97Aha! Tazama, sheria yako naipenda mno ajabu.

Ninaitafakari mchana kutwa.

98Amri zako zimenipa hekima kuliko adui zangu,

kwa kuwa nimezishika daima.

99Nina akili kuliko walimu wangu wote,

kwa kuwa ninatafakari kuhusu sheria zako.

100Nina ufahamu kuliko wazee,

kwa kuwa ninayatii mausia yako.

101Nimezuia miguu yangu isiende kwenye kila njia mbaya,

ili niweze kutii neno lako.

102Sijaziacha sheria zako,

kwa kuwa umenifundisha wewe mwenyewe.

103Tazama jinsi maneno yako yalivyo matamu kwangu,

matamu kuliko asali katika kinywa changu!

104Ninapata ufahamu kutoka mausia yako,

kwa hiyo ninachukia kila njia ya upotovu.

105Neno lako ni taa ya miguu yangu

na mwanga katika njia yangu.

106Nimeapa na nimethibitisha,

kwamba nitafuata sheria zako za haki.

107Nimeteseka sana, uhifadhi maisha yangu, Ee Mwenyezi Mungu,

sawasawa na neno lako.

108Ee Mwenyezi Mungu, pokea sifa za hiari za kinywa changu,

nifundishe sheria zako.

109Ingawa maisha yangu yako hatarini siku zote,

sitasahau sheria yako.

110Waovu wamenitegea mtego,

lakini sijayakiuka maagizo yako.

111Sheria zako ni urithi wangu milele,

naam ni furaha ya moyo wangu.

112Nimekusudia moyoni mwangu

kuyafuata maagizo yako hadi mwisho.

113Ninachukia watu wa nia mbili,

lakini ninapenda sheria yako.

114Wewe ni kimbilio langu na ngao yangu,

nimeweka tumaini langu katika neno lako.

115Ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu,

ili niweze kushika amri za Mungu wangu!

116Nihifadhi sawasawa na ahadi yako, nami nitaishi;

usiache matumaini yangu yakavunjwa.

117Nitegemeze, nami nitaokolewa,

nami daima nitayaheshimu maagizo yako.

118Unawakataa wote wanaoyaasi maagizo yako,

kwa maana udanganyifu wao ni bure.

119Waovu wa nchi unawatupa kama takataka,

kwa hivyo nazipenda sheria zako.

120Mwili wangu unatetemeka kwa kukuogopa wewe,

ninaziogopa sheria zako.

121Nimetenda yaliyo haki na sawa,

usiniache mikononi mwa watesi wangu.

122Mhakikishie mtumishi wako usalama,

usiache wenye kiburi wanidhulumu.

123Macho yangu yamefifia, yakitazamia wokovu wako,

na kuitazamia ahadi yako ya kweli.

124Mtendee mtumishi wako kulingana na upendo wako

na unifundishe maagizo yako.

125Mimi ni mtumishi wako; nipe busara

ili niweze kuelewa sheria zako.

126Ee Mwenyezi Mungu, wakati wako wa kutenda umewadia,

kwa kuwa sheria yako inavunjwa.

127Kwa sababu nazipenda amri zako zaidi ya dhahabu,

naam, zaidi ya dhahabu safi,

128na kwa sababu naona maagizo yako yote ni adili,

nachukia kila njia potovu.

129Sheria zako ni za ajabu,

hivyo ninazitii.

130Kuingia kwa maneno yako kunaleta nuru,

kunampa mjinga ufahamu.

131Nimefungua kinywa changu na kuhema,

nikitamani amri zako.

132Nigeukie na unihurumie, kama uwafanyiavyo siku zote

wale wanaolipenda jina lako.

133Ongoza hatua zangu kulingana na neno lako,

usiache dhambi yoyote initawale.

134Niokoe na uonevu wa wanadamu,

ili niweze kutii mausia yako.

135Mwangazie mtumishi wako uso wako

na unifundishe amri zako.

136Chemchemi za machozi zinatiririka machoni yangu,

kwa kuwa sheria yako haifuatwi.

137Ee Mwenyezi Mungu, wewe ni mwenye haki,

sheria zako ni sahihi.

138Sheria ulizoziweka ni za haki,

ni za kuaminika kikamilifu.

139Jitihada yangu imenidhoofisha, kwa kuwa adui zangu

wanayapuuza maneno yako.

140Ahadi zako zimejaribiwa kikamilifu,

mtumishi wako anazipenda.

141Ingawa ni mdogo na ninadharauliwa,

sisahau mausia yako.

142Haki yako ni ya milele,

na sheria yako ni kweli.

143Shida na dhiki zimenipata,

lakini amri zako ni furaha yangu.

144Sheria zako ni sahihi milele,

hunipa ufahamu ili nipate kuishi.

145Ee Mwenyezi Mungu, ninakuita kwa moyo wangu wote,

nami nitayatii maagizo yako.

146Ninakuita; niokoe

nami nitazishika sheria zako.

147Ninaamka asubuhi na mapema na kukuomba msaada;

nimeweka tumaini langu katika neno lako.

148Sikufumba macho yangu usiku kucha,

ili niweze kutafakari juu ya ahadi zako.

149Usikie sauti yangu sawasawa na upendo wako,

Ee Mwenyezi Mungu,

uyahifadhi maisha yangu,

sawasawa na sheria zako.

150Wale wanaopanga mipango miovu wako karibu nami,

lakini wako mbali na sheria yako.

151Ee Mwenyezi Mungu, hata hivyo wewe u karibu,

na amri zako zote ni za kweli.

152Tangu zamani nimejifunza kutoka shuhuda zako

kwamba umezithibitisha ili zidumu milele.

153Yaangalie mateso yangu, uniokoe,

kwa kuwa sijasahau sheria yako.

154Nitetee katika hali hii yangu na unikomboe,

uyahifadhi maisha yangu sawasawa na ahadi yako.

155Wokovu uko mbali na waovu,

kwa kuwa hawatafuti maagizo yako.

156Ee Mwenyezi Mungu, huruma zako ni kuu,

uyahifadhi maisha yangu sawasawa na sheria zako.

157Adui wanaonitesa ni wengi,

lakini mimi sitaziacha sheria zako.

158Ninawatazama wasioamini kwa chuki,

kwa kuwa hawalitii neno lako.

159Tazama jinsi ninavyopenda mausia yako;

Ee Mwenyezi Mungu, uyahifadhi maisha yangu,

sawasawa na upendo wako.

160Maneno yako yote ni kweli,

sheria zako zote za haki ni za milele.

161Watawala wamenitesa bila sababu,

lakini moyo wangu unatetemeka kwa neno lako.

162Nafurahia ahadi zako

kama mtu aliyepata mateka mengi.

163Ninachukia na kuchukizwa sana na uongo,

lakini napenda sheria yako.

164Ninakusifu mara saba kwa siku,

kwa ajili ya sheria zako za haki.

165Wanaopenda sheria yako wana amani tele,

wala hakuna kitu kinachoweza kuwakwaza.

166Ee Mwenyezi Mungu, ninangojea wokovu wako,

nami ninafuata amri zako,

167Ninazitii sheria zako,

kwa sababu ninazipenda mno.

168Nimetii mausia yako na sheria zako,

kwa kuwa njia zangu zote zinajulikana kwako.

169Ee Mwenyezi Mungu, kilio changu na kifike mbele zako,

nipe ufahamu sawasawa na neno lako.

170Maombi yangu na yafike mbele zako,

niokoe sawasawa na ahadi yako.

171Midomo yangu na ibubujike sifa,

kwa kuwa unanifundisha maagizo yako.

172Ulimi wangu na uimbe kuhusu neno lako,

kwa kuwa amri zako zote ni za haki.

173Mkono wako uwe tayari kunisaidia,

kwa kuwa nimechagua mausia yako.

174Ee Mwenyezi Mungu, ninatamani wokovu wako,

na sheria yako ni furaha yangu.

175Nijalie kuishi ili nipate kukusifu,

na sheria zako zinitegemeze.

176Nimetangatanga kama kondoo aliyepotea.

Mtafute mtumishi wako,

kwa kuwa sijasahau amri zako.

Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™ Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Scriptures™ Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.