The chat will start when you send the first message.
1Ee Bwana , pingana na wale wanaopingana nami,
upigane na hao wanaopigana nami.
2Chukua ngao na kigao.
Inuka unisaidie.
3Inua mkuki wako na fumo lako[#35:3 Fumo ni sawa na sagai, yaani mkuki mfupi.]
dhidi ya hao wanaonifuatia.
Iambie nafsi yangu,
“Mimi ni wokovu wako.”
4Wafedheheshwe na waaibishwe
wale wanaotafuta uhai wangu.
Wanaofanya shauri kuniangamiza
wafukuzwe mbali kwa bumbuazi.
5Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo,
malaika wa Bwana akiwafukuza.
6Njia yao na iwe giza na ya utelezi,
malaika wa Bwana akiwafuatilia.
7Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu,
na bila sababu wamenichimbia shimo,
8maafa na yawapate ghafula:
wavu walionifichia na uwatege wenyewe,
na waanguke katika shimo hilo,
kwa maangamizi yao.
9Ndipo nafsi yangu itashangilia katika Bwana
na kuufurahia wokovu wake.
10Nitapaza sauti yangu nikisema,
“Ni nani aliye kama wewe, Ee Bwana ?
Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale waliowazidi nguvu,
unawaokoa maskini na wahitaji kutokana na wanaowanyangʼanya!”
11Mashahidi wakatili wanainuka,
wananiuliza mambo nisiyoyajua.
12Wananilipa baya kwa jema
na kuiacha nafsi yangu ukiwa.
13Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa gunia
na nikajinyenyekeza kwa kufunga.
Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa,
14niliendelea kuomboleza
kama vile wao ni rafiki au ndugu.
Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni
kama ninayemwombolezea mama yangu.
15Lakini nilipojikwaa,
walikusanyika kwa shangwe;
washambuliaji walijikusanya dhidi yangu
bila mimi kujua.
Walinisingizia pasipo kukoma.
16Kama watu wasiomcha Mungu, wamenidhihaki,
wamenisagia meno.
17Ee Bwana, utatazama hadi lini?
Niokoe maisha yangu na maangamizi yao,
okoa uhai wangu wa thamani
kutokana na simba hawa.
18Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa,
nitakusifu katikati ya watu wengi.
19Usiwaache wale wanaonisimanga,
wale ambao ni adui zangu bila sababu;
usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu
wakonyeze jicho kwa hila.
20Hawazungumzi kwa amani,
bali wanatunga mashtaka ya uongo
dhidi ya wale wanaoishi
kwa utulivu katika nchi.
21Hunifumbulia vinywa vyao wakisema, “Aha! Aha!
Kwa macho yetu wenyewe tumeliona.”
22Ee Bwana , umeona hili, usiwe kimya.
Usiwe mbali nami, Ee Bwana.
23Amka, inuka unitetee!
Unipiganie Mungu wangu na Bwana wangu.
24Nihukumu kwa haki yako, Ee Bwana Mungu wangu,
sawasawa na haki yako;
usiwaache wakusimange.
25Usiwaache wafikiri, “Aha, hili ndilo tulilotaka!”
Au waseme, “Tumemmeza.”
26Wote wanaofurahia dhiki yangu
waaibishwe na wachanganyikiwe;
hao wanaojiinua dhidi yangu
wavikwe aibu na dharau.
27Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki
wapige kelele za shangwe na furaha;
hebu waseme siku zote, “Bwana atukuzwe,
ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake.”
28Ulimi wangu utanena haki yako
na sifa zako mchana kutwa.