The chat will start when you send the first message.
1Heri mtu yule anayemjali mnyonge,
Bwana atamwokoa wakati wa shida.
2Bwana atamlinda na kuyahifadhi maisha yake,
atambariki katika nchi
na hatamwacha katika tamaa ya adui zake.
3Bwana atamtegemeza akiwa mgonjwa kitandani,
na atamwinua kutoka kitandani mwake.
4Nilisema, “Ee Bwana nihurumie,
niponye, maana nimekutenda dhambi wewe.”
5Adui zangu wanasema kwa hila,
“Lini atakufa, na jina lake litokomee kabisa.”
6Kila anapokuja mtu kunitazama,
huzungumza uongo,
huku moyo wake ukikusanya masingizio;
kisha huondoka na kuyasambaza.
7Adui zangu wote hunongʼonezana dhidi yangu,
hao huniwazia mabaya sana, wakisema,
8“Ugonjwa mbaya sana umempata,
kamwe hatainuka tena kitandani mwake.”
9Hata rafiki yangu wa karibu niliyemwamini,
yule aliyekula chakula changu
ameniinulia kisigino chake.
10Lakini wewe, Ee Bwana , nihurumie,
ukaniinue tena, ili niweze kuwalipiza kisasi.
11Najua kwamba wapendezwa nami,
kwa kuwa adui yangu hanishindi.
12Katika uadilifu wangu unanitegemeza
na kuniweka kwenye uwepo wako milele.
13Mtukuzeni Bwana , Mungu wa Israeli,
tangu milele na hata milele.