The chat will start when you send the first message.
1Sikieni haya, enyi mataifa yote,
sikilizeni, ninyi wote mnaoishi dunia hii.
2Wakubwa kwa wadogo,
matajiri na maskini pamoja:
3Kinywa changu kitasema maneno ya hekima,
usemi wa moyo wangu utatoa ufahamu.
4Nitatega sikio langu nisikilize mithali,
nitafafanua kitendawili kwa zeze:
5Kwa nini niogope siku mbaya zinapokuja,
wakati wadanganyifu waovu wanaponizunguka,
6wale wanaotegemea mali yao
na kujivunia utajiri wao mwingi?
7Hakuna mwanadamu yeyote
awezaye kuukomboa uhai wa mwingine,
au kumpa Mungu fidia kwa ajili yake.
8Fidia ya uhai ni gharama kubwa,
hakuna malipo yoyote yanayotosha,
9ili aishi milele
na asione uharibifu.
10Wote wanaona kwamba watu wenye hekima hufa;
wajinga na wapumbavu vivyo hivyo huangamia
na kuwaachia wengine mali yao.
11Makaburi yao yatabaki kuwa nyumba zao za milele,
makao yao vizazi vyote;
ingawa walikuwa na mashamba
na kuyaita kwa majina yao.
12Lakini mwanadamu, licha ya utajiri wake, hadumu;
anafanana na mnyama aangamiaye.
13Hii ndiyo hatima ya wale wanaojitumainia wenyewe,
pia ya wafuasi wao, waliothibitisha misemo yao.
14Kama kondoo, wamewekewa kwenda kaburini,[#49:14 Kaburini hapa ina maana ya Sheol kwa Kiebrania, yaani Kuzimu.]
nacho kifo kitawala.
Wanyofu watawatawala asubuhi,
maumbile yao yataozea kaburini,
mbali na majumba yao makubwa ya fahari.
15Lakini Mungu atakomboa uhai wangu dhidi ya kaburi;[#49:15 au nafsi]
hakika atanichukua kwake.
16Usitishwe mtu anapotajirika,
fahari ya nyumba yake inapoongezeka,
17kwa maana hatachukua chochote atakapokufa,
fahari yake haitashuka pamoja naye.
18Ingawa alipokuwa akiishi alijihesabu kuwa heri,
na wanadamu wanakusifu unapofanikiwa,
19atajiunga na kizazi cha baba zake,
ambao hawataona kamwe nuru ya uzima.
20Wanadamu wenye utajiri bila ufahamu
ni kama wanyama wanaoangamia.