Zaburi 65

Zaburi 65

Zaburi 65

Kusifu na kushukuru

1Ee Mungu, sifa zakungojea katika Sayuni;

kwako wewe nadhiri zetu zitatimizwa.

2Ewe usikiaye maombi,

watu wote watakuja kwako wewe.

3Tulipokuwa tumefunikwa kabisa na dhambi,

wewe ulisamehe makosa yetu.

4Heri wale uliowachagua

na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako!

Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako,

mema ya Hekalu lako takatifu.

5Unatujibu kwa matendo ya kushangaza ya haki,

Ee Mungu Mwokozi wetu,

tumaini la miisho yote ya duniani

na la bahari zilizo mbali sana,

6uliyeumba milima kwa uwezo wako,

ukiwa umejivika nguvu,

7uliyenyamazisha dhoruba za bahari,

ngurumo za mawimbi yake,

na ghasia za mataifa.

8Wale wanaoishi mbali sana

wanaogopa maajabu yako,

kule asubuhi ipambazukiapo

na kule jioni inakofifilia

umeziita nyimbo za furaha.

9Waitunza nchi na kuinyeshea,

waitajirisha kwa wingi.

Vijito vya Mungu vimejaa maji

ili kuwapa watu nafaka,

kwa maana wewe umeviamuru.

10Umeilowesha mifereji yake

na kusawazisha kingo zake;

umeilainisha kwa manyunyu

na kuibariki mimea yake.

11Umeuvika mwaka taji la baraka,

magari yako yanafurika kwa wingi.

12Mbuga za majani za jangwani umezineemesha;

vilima vimevikwa furaha.

13Malisho yamejaa makundi ya wanyama,

na mabonde yamepambwa kwa mavuno;

vyote vinashangilia kwa furaha na kuimba.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.