The chat will start when you send the first message.
1Ee Bwana , nimekukimbilia wewe,
usiache nikaaibika kamwe.
2Kwa haki yako uniponye na kuniokoa,
unitegee sikio lako uniokoe.
3Uwe kwangu mwamba wa kimbilio,
mahali nitakapokimbilia kila wakati;
toa amri ya kuniokoa, kwa kuwa wewe
ni mwamba wangu na ngome yangu.
4Ee Mungu wangu uniokoe kutoka mkono wa mwovu,
kutoka makucha ya watu wapotovu na wakatili.
5Kwa kuwa umekuwa tumaini langu, Ee Bwana Mwenyezi,
tegemeo langu tangu ujana wangu.
6Tangu kuzaliwa nimekutegemea wewe,
ulinitoa tumboni mwa mama yangu.
Nitakusifu wewe daima.
7Nimekuwa ishara mbaya kwa wengi,
lakini wewe ni kimbilio langu imara.
8Kinywa changu kimejazwa sifa zako,
nikitangaza utukufu wako mchana kutwa.
9Usinitupe wakati wa uzee,
wala usiniache nguvu zangu zinapopungua.
10Kwa maana adui zangu wananisengenya,
wale wanaotaka kuniua wanapanga njama.
11Wanasema, “Mungu amemwacha,
mkimbilieni mkamkamate,
kwani hakuna wa kumwokoa.”
12Ee Mungu, usiwe mbali nami,
njoo haraka kunisaidia, Ee Mungu wangu.
13Washtaki wangu na waangamie kwa aibu,
wale wanaotaka kunidhuru
na wafunikwe kwa dharau na fedheha.
14Lakini mimi nitatumaini siku zote;
nitakusifu zaidi na zaidi.
15Kinywa changu kitasimulia haki yako,
wokovu wako mchana kutwa,
ingawa sifahamu kipimo chake.
16Ee Bwana Mwenyezi, nitakuja
na kutangaza matendo yako makuu,
nitatangaza haki yako, yako peke yako.
17Ee Mungu, umenifundisha tangu ujana wangu,
hadi leo ninatangaza matendo yako ya ajabu.
18Ee Mungu, usiniache,
hata nikiwa mzee wa mvi,
hadi nitangaze uwezo wako kwa kizazi kijacho,
nguvu zako kwa wote watakaokuja baadaye.
19Ee Mungu, haki yako imefika juu Lakini mimi mbingu,
wewe ambaye umefanya mambo makuu.
Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe?
20Ingawa umenifanya nipate taabu nyingi na chungu,
utanihuisha tena,
kutoka vilindi vya dunia
utaniinua tena.
21Utaongeza heshima yangu
na kunifariji tena.
22Ee Mungu wangu, nitakusifu kwa kinubi
kwa ajili ya uaminifu wako;
Ee Uliye Mtakatifu wa Israeli,
nitakuimbia sifa kwa zeze.
23Midomo yangu itapaza sauti kwa furaha
ninapokuimbia sifa,
mimi, ambaye umenikomboa.
24Ulimi wangu utasimulia matendo yako ya haki
mchana kutwa,
kwa maana wale waliotaka kunidhuru,
wameaibishwa na kufadhaishwa.