The chat will start when you send the first message.
1Ee Mungu, mbona umetukataa milele?
Mbona hasira yako inatoka moshi
juu ya kondoo wa malisho yako?
2Kumbuka watu uliowanunua zamani,
kabila la urithi wako, ambao uliwakomboa:
Mlima Sayuni, ambamo uliishi.
3Geuza hatua zako kuelekea magofu haya ya kudumu,
uharibifu wote huu ambao adui ameuleta pale patakatifu.
4Adui zako wamenguruma pale ulipokutana nasi,
wanaweka bendera zao kama alama.
5Walifanya kama watu wanaotumia mashoka
kukata kichaka cha miti.
6Walivunjavunja milango yote iliyonakshiwa
kwa mashoka na vishoka vyao.
7Waliteketeza kabisa mahali pako patakatifu,
wakayanajisi makao ya Jina lako.
8Walisema mioyoni mwao,
“Tutawaponda kabisa!”
Walichoma kila mahali Mungu
alipoabudiwa katika nchi.
9Hatukupewa ishara za miujiza;
hakuna manabii waliobaki,
hakuna yeyote kati yetu ajuaye
hali hii itachukua muda gani.
10Ee Mungu, mtesi atakudhihaki hadi lini?
Je, adui watalitukana jina lako milele?
11Kwa nini unazuia mkono wako,
mkono wako wa kuume?
Uutoe kutoka makunjo ya vazi lako
na uwaangamize!
12Lakini wewe, Ee Mungu, ni mfalme wangu tangu zamani,
unaleta wokovu duniani.
13Ni wewe uliyeigawanya bahari kwa uweza wako;
ulivunja vichwa vya mnyama mkubwa wa baharini.
14Ni wewe uliyeponda vichwa vya Lewiathani,[#74:14 Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa.]
nawe ukamtoa kama chakula kwa viumbe vya jangwani.
15Ni wewe uliyefungua chemchemi na vijito,
ulikausha mito iliyokuwa ikitiririka daima.
16Mchana ni wako, na usiku ni wako pia;
uliziweka jua na mwezi.
17Ni wewe uliyeiweka mipaka yote ya dunia,
ulifanya kiangazi na masika.
18Ee Bwana , kumbuka jinsi mtesi alivyokudhihaki,
jinsi watu wapumbavu walivyolitukana jina lako.
19Usiukabidhi uhai wa njiwa wako kwa wanyama mwitu;
usisahau kabisa uhai wa watu wako wanaoteseka milele.
20Likumbuke agano lako,
maana mara kwa mara mambo ya jeuri
yamejaa katika sehemu za giza nchini.
21Usiruhusu waliodhulumiwa warudi nyuma kwa aibu;
maskini na wahitaji hebu walisifu jina lako.
22Inuka, Ee Mungu, ujitetee;
kumbuka jinsi wapumbavu
wanavyokudhihaki mchana kutwa.
23Usipuuze makelele ya watesi wako,
ghasia za adui zako, zinazoinuka mfululizo.