The chat will start when you send the first message.
1Katika Yuda, Mungu anajulikana,
jina lake ni kuu katika Israeli.
2Hema lake liko Salemu,
makao yake katika Sayuni.
3Huko alivunja mishale iliyowaka,
ngao na panga, silaha za vita.
4Wewe unangʼaa kwa mwanga,
mwenye fahari zaidi ya milima yenye utajiri wa wanyama pori.
5Mashujaa hulala wametekwa nyara,
hulala usingizi wao wa mwisho;
hakuna hata mmoja wa watu wa vita
anayeweza kuinua mikono yake.
6Kwa kukemea kwako, Ee Mungu wa Yakobo,
farasi na gari la vita vilikaa kimya.
7Wewe peke yako ndiye wa kuogopwa.
Ni nani awezaye kusimama mbele yako unapokasirika?
8Ulitamka hukumu kutoka mbinguni,
nayo nchi ikaogopa, ikawa kimya:
9wakati wewe, Ee Mungu, ulipoinuka kuhukumu,
kuwaokoa wote walioonewa katika nchi.
10Hakika ghadhabu yako dhidi ya wanadamu inakuletea sifa,
na masalia ya ghadhabu yako unajifunga mshipi.
11Wekeni nadhiri kwa Bwana Mungu wenu na kuzitimiza;
nchi zote za jirani na walete zawadi
kwa Yule astahiliye kuogopwa.
12Huvunja roho za watawala;
anaogopwa na wafalme wa dunia.