The chat will start when you send the first message.
1Ee Bwana wa majeshi,
makao yako yapendeza kama nini!
2Nafsi yangu inatamani sana,
naam, hata kuona shauku,
kwa ajili ya nyua za Bwana ;
moyo wangu na mwili wangu
vinamlilia Mungu Aliye Hai.
3Hata shomoro amejipatia makao,
mbayuwayu amejipatia kiota
mahali awezapo kuweka makinda yake:
mahali karibu na madhabahu yako,
Ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu.
4Heri wale wanaokaa nyumbani mwako,
wanaokusifu wewe daima.
5Heri wale ambao nguvu zao ziko kwako,
na njia ziendazo Sayuni zimo mioyoni mwao.
6Wanapopita katika Bonde la Baka,[#84:6 maana yake Bonde la Vilio]
hulifanya mahali pa chemchemi,
pia mvua za vuli hulijaza kwa madimbwi.
7Huendelea toka nguvu hadi nguvu,
hadi kila mmoja afikapo
mbele za Mungu huko Sayuni.
8Ee Bwana Mungu wa majeshi, sikia maombi yangu;
nisikilize, Ee Mungu wa Yakobo.
9Ee Mungu, uitazame ngao yetu,
mtazame kwa wema mpakwa mafuta wako.
10Siku moja katika nyua zako ni bora
kuliko siku elfu mahali pengine;
afadhali ningekuwa bawabu katika nyumba ya Mungu wangu
kuliko kukaa katika mahema ya waovu.
11Kwa kuwa Bwana Mungu ni jua na ngao;
Bwana hutoa wema na heshima;
hakuna kitu chema anachowanyima
wale ambao hawana hatia.
12Ee Bwana wa majeshi,
heri mtu anayekutumaini wewe.