Warumi 8

Warumi 8

Maisha katika Roho

1Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu.[#8:1 Maandiko mengine huongeza maneno ya ms 4 Yesu, ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.]

2Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti.

3Kwa maana kile ambacho sheria haikuwa na uwezo wa kufanya, kwa vile ilivyokuwa dhaifu katika mwili, Mungu kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe kwa mfano wa mwanadamu mwenye mwili ulio wa dhambi na kwa ajili ya dhambi, yeye aliihukumu dhambi katika mwili,

4ili haki ipatikanayo kwa sheria itimizwe ndani yetu sisi, ambao hatuenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.

5Kwa maana wale wanaoishi kwa kuufuata mwili huziweka nia zao katika vitu vya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kufuata Roho, huziweka nia zao katika mambo ya Roho.

6Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani.

7Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.

8Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.

9Lakini ninyi, hamtawaliwi na mwili, bali na Roho, ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu. Mtu ambaye hana Roho wa Kristo, huyo si wa Kristo.

10Lakini kama Kristo anakaa ndani yenu, miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, lakini roho zenu zi hai kwa sababu ya haki.

11Nanyi ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu kutoka kwa wafu ataihuisha pia miili yenu ambayo hufa, kupitia kwa Roho wake akaaye ndani yenu.

12Kwa hiyo ndugu zangu, sisi tu wadeni, si wa mwili, ili tuishi kwa kuufuata mwili,

13kwa maana mkiishi kwa kuufuata mwili, mtakufa, lakini mkiyaua matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.

14Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio watoto wa Mungu.

15Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iletayo hofu tena, bali mlipokea Roho wa kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, Baba.”[#8:15 ni neno la Kiaramu ambalo maana yake ni Baba ; ni mtoto wa kuzaa tu angeweza kulitumia kwa baba yake.]

16Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu kwamba sisi tu watoto wa Mungu.

17Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.

Utukufu ujao

18Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu.

19Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu.

20Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini,

21ili viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.

22Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama uchungu wa mwanamke wakati wa kuzaa.

23Wala si hivyo viumbe peke yao, bali hata sisi ambao ndio matunda ya kwanza ya Roho, kwa ndani tunalia kwa uchungu tukisubiri kwa shauku kufanywa wana wa Mungu, yaani ukombozi wa miili yetu.

24Kwa kuwa tuliokolewa kwa tumaini hili. Lakini kama kinachotumainiwa kikionekana, basi hakiwi tumaini tena. Je, kuna mtu anayetumaini kupata kitu alicho nacho tayari?

25Lakini tunapotumaini kupata kitu ambacho hatuna, basi twakingojea kwa saburi.

26Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa.

27Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.

Tu zaidi ya washindi

28Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wanaompenda, yaani wale walioitwa kwa kusudi lake, ili kuwaletea mema.

29Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.

30Nao wale Mungu aliotangulia kuwachagua, akawaita, wale aliowaita pia akawahesabia haki, nao wale aliowahesabia haki, pia akawatukuza.

Upendo wa Mungu

31Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu?

32Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye?

33Ni nani atakayewashtaki wale ambao Mungu amewateua? Mungu ndiye anayewahesabia haki.

34Ni nani basi atakayewahukumia adhabu? Hakuna! Kristo Yesu aliyekufa, naam, na zaidi ya hayo, akafufuliwa kutoka kwa wafu, yuko mkono wa kuume wa Mungu, naye pia anatuombea.

35Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga?

36Kama ilivyoandikwa:

“Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

37Lakini katika mambo haya yote tu zaidi ya washindi kwa yeye aliyetupenda.

38Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo,

39wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.