The chat will start when you send the first message.
1Wimbo ulio bora wa Sulemani.
2Unibusu kwa busu la kinywa chako,
kwa maana upendo wako unafurahisha kuliko divai.
3Manukato yako yananukia vizuri,
jina lako ni kama manukato yaliyomiminwa.
Ndiyo sababu wanawali wanakupenda!
4Nichukue twende nawe, na tufanye haraka!
Mfalme na anilete ndani ya vyumba vyake.
Tunakushangilia na kukufurahia,
tutasifu upendo wako kuliko divai.
Tazama jinsi ilivyo bora wakupende!
5Mimi ni mweusi, lakini napendeza,
enyi binti za Yerusalemu,
mweusi kama mahema ya Kedari,
kama mapazia ya hema la Sulemani.
6Usinikazie macho kwa sababu mimi ni mweusi,
kwa sababu nimefanywa mweusi na jua.
Wana wa mama yangu walinikasirikia
na kunifanya niwe mtunza mashamba ya mizabibu.
Shamba langu mwenyewe la mizabibu nimeliacha.
7Niambie, wewe ninayekupenda,
unalisha wapi kundi lako la kondoo
na ni wapi unapowapumzisha kondoo wako adhuhuri.
Kwa nini niwe kama mwanamke aliyefunikwa shela
karibu na makundi ya rafiki zako?
8Kama hujui, ewe mwanamke mzuri kuliko wote,
fuata nyayo za kondoo,
na kulisha wana-mbuzi wako
karibu na mahema ya wachungaji.
9Mpendwa wangu, ninakufananisha na farasi jike
aliyefungwa katika mojawapo ya magari ya vita ya Farao.
10Mashavu yako yanapendeza yakiwa na vipuli,
shingo yako ikiwa na mikufu ya vito.
11Tutakufanyia vipuli vya dhahabu,
vyenye kupambwa kwa fedha.
12Mfalme alipokuwa mezani pake,
manukato yangu yalisambaza harufu yake nzuri.
13Mpenzi wangu kwangu mimi ni kifuko cha manemane
kati ya matiti yangu.
14Mpenzi wangu kwangu mimi ni kama kishada cha maua ya mhina
kutoka mashamba ya mizabibu ya En-Gedi.
15Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpendwa wangu!
Tazama jinsi ulivyo mzuri!
Macho yako ni kama ya hua.
16Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!
Ee, tazama jinsi unavyopendeza!
Na kitanda chetu ni cha majani mazuri.
17Nguzo za nyumba yetu ni mierezi,
na mapao yetu ni miberoshi.