Wimbo 2

Wimbo 2

1Mimi ni ua la Sharoni,

yungiyungi ya bondeni.

2Kama yungiyungi kati ya miiba,

ndivyo alivyo mpendwa wangu kati ya wanawali.

3Kama mti wa mtofaa miongoni mwa miti ya msituni,

ndivyo alivyo mpenzi wangu

miongoni mwa wanaume vijana.

Ninafurahia kuketi kivulini mwa mwanaume huyu,

na tunda lake ni tamu kwangu.

4Amenichukua hadi ukumbi wa karamu,

na bendera ya huyu mwanaume

juu yangu ni upendo.

5Nitie nguvu kwa zabibu kavu,

niburudishe kwa matofaa,

kwa maana ninazimia kwa mapenzi.

6Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu,

na mkono wake wa kuume unanikumbatia.

7Binti za Yerusalemu, ninawaagiza

kwa paa na kwa ayala wa shambani:

Msichochee wala kuamsha mapenzi

hata yatakapotaka yenyewe.

8Sikiliza! Mpenzi wangu!

Tazama! Huyu hapa anakuja,

akirukaruka juu milimani

akizunguka juu ya vilima.

9Mpenzi wangu ni kama paa au ayala mchanga.

Tazama! Anasimama nyuma ya ukuta wetu,

akitazama kupitia madirishani,

akichungulia kimiani.

10Mpenzi wangu alizungumza na kuniambia,

“Inuka, mpendwa wangu,

mrembo wangu, tufuatane.

11Tazama! Wakati wa masika umepita,

mvua imekwisha na ikapita.

12Maua yanatokea juu ya nchi;

majira ya kuimba yamewadia,

sauti za njiwa zinasikika

katika nchi yetu.

13Mtini unatunga matunda yake ya mwanzoni,

zabibu zinazochanua zaeneza harufu nzuri.

Inuka, njoo mpenzi wangu.

Mrembo wangu, tufuatane.”

14Hua wangu penye nyufa za majabali,

mafichoni pembezoni mwa mlima,

nioneshe uso wako,

na niisikie sauti yako,

kwa maana sauti yako ni tamu,

na uso wako unapendeza.

15Tukamatie mbweha,

mbweha wale wadogo

wanaoharibu mashamba ya mizabibu,

mashamba yetu ya mizabibu yaliyochanua.

16Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake,

yeye hujilisha kati ya yungiyungi.

17Hadi jua linapochomoza,

na vivuli vikimbie,

rudi, mpenzi wangu,

na uwe kama paa,

au kama ayala mchanga

juu ya vilima vya Betheri.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.