1 Mambo ya Nyakati 15

1 Mambo ya Nyakati 15

Sanduku la Agano laletwa Yerusalemu

1Basi Daudi akajijengea nyumba katika mji wa Daudi; akatayarisha mahali kwa ajili ya sanduku la Mungu, akalipigia hema.[#1 Nya 16:1; 17:1-5; Zab 132:2-5; Mdo 7:46]

2Ndipo Daudi akasema, Haimpasi mtu awaye yote kulichukua sanduku la Mungu, isipokuwa Walawi peke yao; kwa kuwa hao ndio aliowachagua BWANA, ili walichukue sanduku la Mungu, na kumtumikia daima.[#Hes 4:2,15; Kum 10:8; 31:9; Yos 3:3]

3Basi Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu, ili kulipandisha sanduku la BWANA, mpaka mahali pake alipoliwekea tayari.[#1 Fal 8:1; 1 Nya 13:5]

4Daudi akawakutanisha wana wa Haruni, na Walawi;

5wa wana wa Kohathi; Urieli mkuu wao, na nduguze mia moja na ishirini;[#Kut 6:16-18]

6wa wana wa Merari; Asaya mkuu wao, na nduguze mia mbili na ishirini;

7wa wana wa Gershoni; Yoeli mkuu wao, na nduguze mia moja na thelathini;

8wa wana wa Elsafani; Shemaya mkuu wao, na nduguze mia mbili;[#Kut 6:22]

9wa wana wa Hebroni; Elieli mkuu wao, na nduguze themanini;[#Kut 6:18; Hes 26:58]

10wa wana wa Uzieli; Aminadabu mkuu wao, na nduguze mia moja kumi na wawili.

11Tena, Daudi akawaita Sadoki na Abiathari makuhani, na hao Walawi, Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli, na Aminadabu,

12akawaambia, Ninyi ni vichwa vya koo za baba za Walawi; jitakaseni, ninyi na ndugu zenu, ili mlipandishe sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli, mpaka mahali pale nilipolitayarishia.[#Kut 19:10,22; Law 10:3; 1 Sam 7:1; 2 Nya 5:11; 29:5,15; Eze 48:11; Yn 17:17; Rum 12:1,2]

13Kwa kuwa ninyi hamkulichukua safari ya kwanza, BWANA, Mungu wetu, alitufurikia, kwa maana hatukumtafuta kulingana na sheria.[#2 Sam 6:3; 1 Nya 13:7,10,11]

14Basi makuhani na Walawi wakajitakasa, ili wapate kulipandisha sanduku la BWANA, Mungu wa Israeli.

15Na wana wa Walawi wakalichukua sanduku la Mungu mabegani mwao kwa miti yake, kama vile Musa alivyoamuru, kulingana na neno la BWANA.[#Kut 25:14; Hes 4:15; 7:9]

16Kisha Daudi akamwambia mkuu wa Walawi, kwamba awaagize ndugu zao waimbaji, pamoja na vyombo vyao vya kupigia ngoma, vinanda, na vinubi, na matoazi, wavipige na kupaza sauti kwa furaha.[#1 Nya 6:31; 13:8; Zab 33:2; 68:25]

17Basi Walawi wakamwagiza Hemani mwana wa Yoeli; na wa nduguze, Asafu mwana wa Berekia; na wa wana wa Merari ndugu zao, Ethani mwana wa Kishi;[#1 Nya 6:33,39,44]

18na pamoja nao ndugu zao kwa cheo cha pili, Zekaria, na Yaasieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Uni, na Eliabu; na Benaya, na Maaseya, na Matithia, na Elifelehu, na Mikneya, na Obed-edomu, na Yeieli, mabawabu.

19Hivyo hao waimbaji, Hemani, Asafu, na Ethani, wakaagizwa kupiga matoazi yao ya shaba kwa sauti kuu;

20na Zekaria, na Yaasieli na Shemiramothi, na Yehieli, na Uni, na Eliabu, na Maaseya, na Benaya, wenye vinanda vya sauti ya Alamothi;

21na Metithia, na Elifelehu, na Mikneya, na Obed-edomu, na Yeieli, na Azazia, wenye vinubi vya sauti ya Sheminithi,

22waongoze. Na Kenania, mkuu wa Walawi katika uimbaji, asimamie uimbaji, kwa sababu alikuwa stadi.

23Na Berekia na Elkana walikuwa mabawabu kwa ajili ya sanduku.

24Na Shebania, na Yoshafati, na Nethaneli, na Amasai, na Zekaria, na Benaya, na Eliezeri, makuhani, wakapiga baragumu mbele ya sanduku la Mungu; na Obed-edomu na Yehia walikuwa mabawabu kwa ajili ya sanduku.[#Hes 10:8; Zab 81:3]

25Basi Daudi, na wazee wa Israeli, na makamanda wa maelfu, wakaenda, ili kulipandisha sanduku la Agano la BWANA kutoka nyumbani mwa Obed-edomu kwa furaha kuu;[#2 Sam 6:12,13; 1 Fal 1:8; Kum 12:7,18; Ezr 6:16]

26hata ikawa, Mungu alipowajalia Walawi waliolichukua sanduku la Agano la BWANA, wakachinja ng'ombe saba, na kondoo dume saba.[#Hes 23:1; Ayu 42:8]

27Naye Daudi alikuwa amevaa joho la kitani safi, na Walawi wote waliolichukua sanduku, na waimbaji, na Kenania msimamizi wa uchukuzi, na waimbaji; naye Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani.

28Ndivyo Israeli wote walivyolipandisha sanduku la Agano la BWANA kwa shangwe na kwa sauti ya tarumbeta, na kwa baragumu, na kwa matoazi, wakipiga sauti kuu kwa vinanda na vinubi.[#1 Nya 13:8]

29Hata ikawa, sanduku la Agano la BWANA lilipofika mjini kwa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi, akicheza na kushangilia; akamdharau moyoni mwake.[#2 Sam 6:16; Mdo 2:13]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania