1 Mambo ya Nyakati 21

1 Mambo ya Nyakati 21

Hesabu na tauni

1Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Waisraeli.[#2 Sam 24:1; 1 Fal 22:20-22; Ayu 1:6; Zek 3:1; Mt 4:3; Lk 22:31; Yn 13:2; Mdo 5:3; Ufu 12:9]

2Basi Daudi akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni mkawahesabu Israeli toka Beer-sheba mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao.[#1 Nya 27:23]

3Naye Yoabu akasema, BWANA na awaongeze watu wake mara mia hesabu yao ilivyo; lakini, bwana wangu mfalme, si wote watumishi wa bwana wangu? Mbona basi bwana wangu analitaka neno hili? Mbona alete hatia kwa Israeli?

4Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akaenda zake, akapita kati ya Israeli wote, akafika Yerusalemu.[#Mit 29:25; Mhu 8:4; Mdo 4:19; 5:29]

5Naye Yoabu akamtolea Daudi jumla ya hesabu ya watu. Na hao wote wa Israeli walikuwa watu milioni moja na laki moja, wenye kufuta panga; na wa Yuda watu elfu mia nne sabini (470,000), wenye kufuta panga.

6Lakini Lawi na Benyamini hakuwahesabu miongoni mwao; kwa sababu neno la mfalme limemchukiza Yoabu.[#Hes 1:47-49; 1 Nya 27:24]

7Neno hilo likawa baya machoni pa Mungu; kwa hiyo akawapiga Israeli.

8Naye Daudi akamwambia Mungu, Nimekosa sana, kwa kuwa nimelifanya jambo hili; lakini sasa uuondolee mbali, nakusihi, uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.[#2 Sam 12:13; 24:10; Ayu 42:2,6; Zab 25:11; 51:1-3; Mit 28:13,14; 2 Kor 7:10; Hos 14:2]

9Naye BWANA akanena na Gadi, mwonaji wake Daudi, akisema,[#1 Sam 9:9]

10Nenda ukanene na Daudi, ukisema, BWANA asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya ujichagulie moja, nikutendee hilo.

11Basi Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, BWANA asema hivi, Jichagulie upendavyo;

12miaka mitatu ya njaa; au miezi mitatu kuangamia mbele ya adui zako, ukipatwa na upanga wa watesi wako; au siku tatu upanga wa BWANA, yaani tauni katika nchi, na malaika wa BWANA akiharibu kati ya mipaka yote ya Israeli. Haya basi ufikiri ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.[#2 Sam 24:13]

13Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na nianguke katika mkono wa BWANA; kwa kuwa rehema zake ni nyingi sana; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.[#Neh 9:17; Zab 100:5; 145:9; Omb 3:22; Yoe 2:13]

14Basi BWANA akawaletea Israeli tauni; nao wakaanguka wa Israeli watu elfu sabini.

15Naye Mungu akatuma malaika aende Yerusalemu ili auangamize; naye alipokuwa tayari kuangamiza, BWANA akatazama, akaghairi katika mabaya, akamwambia malaika aharibuye, Basi yatosha; sasa ulegeze mkono wako. Naye malaika wa BWANA akasimama karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi.[#2 Sam 24:16; Yer 26:18; Mt 23:37,38; Mwa 6:6; Amu 2:18; #21:15 Au, Ornani.]

16Daudi akainua macho yake, akamwona huyo malaika wa BWANA amesimama kati ya nchi na mbingu, naye alikuwa na upanga wazi mkononi, umenyoshwa juu ya Yerusalemu. Ndipo Daudi na wazee wakaanguka kifudifudi, nao wamevaa nguo za magunia.[#2 Nya 3:1]

17Daudi akamwambia Mungu, Je! Si mimi niliyeamuru watu wahesabiwe? Naam, mimi ndimi niliyekosa, na kufanya yaliyo maovu sana; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako, nakusihi, Ee BWANA, Mungu wangu, na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya babangu; wala si juu ya watu wako, hata wao wapigwe.

Madhabahu ya Daudi na sadaka yake

18Ndipo huyo malaika wa BWANA akamwamuru Gadi kwamba amwambie Daudi, ya kuwa Daudi akwee, akamwinulie BWANA madhabahu katika kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi.

19Basi Daudi akakwea kulingana na neno la Gadi, alilolinena kwa jina la BWANA.

20Arauna alipogeuka, na kumwona yule malaika, ndipo yeye na wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha. Naye Arauna alikuwa akipura ngano.

21Basi Daudi alipokuwa akimjia Arauna, Arauna akatazama, akamwona Daudi, akatoka katika kile kiwanja, akamsujudia Daudi kifudifudi hadi chini.

22Ndipo Daudi akamwambia Arauna, Unipe mahali pa kiwanja hiki, ili kwamba nimjengee BWANA madhabahu hapa; kwa thamani yake kamili utanipa; ili kwamba tauni izuiliwe katika watu.[#Hes 16:48; 25:8]

23Arauna akamwambia Daudi, Ujitwalie, na bwana wangu mfalme na afanye yaliyo mema machoni pake; tazama, ng'ombe kwa sadaka za kuteketezwa, na vyombo vya kupuria kwa kuni, na ngano kwa sadaka ya unga, nazitoa; zote nazitoa.

24Mfalme Daudi akamwambia Arauna, La, sivyo, lakini kweli nitazinunua kwa thamani yake kamili; kwani sitamtwalia BWANA kilicho chako, wala kutoa sadaka ya kuteketezwa isiyo na gharama.

25Basi Daudi akampimia Arauna thamani ya mahali pale shekeli mia sita za dhahabu kwa uzani[#2 Sam 24:24]

26Kisha Daudi akamjengea BWANA madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, akamlingana BWANA; naye akamwitikia kutoka mbinguni kwa moto juu ya madhabahu hiyo ya sadaka ya kuteketezwa.[#Law 9:24; 2 Nya 3:1; 7:1]

27BWANA naye akamwamuru malaika; naye akaurudisha upanga wake alani mwake tena.

Mahali pa kujenga hekalu pachaguliwa

28Wakati huo, Daudi alipoona ya kwamba BWANA amemwitikia katika kiwanja cha Arauna, Myebusi, ndipo alipotoa dhabihu huko.

29Kwa maana ile maskani ya BWANA, aliyoifanya Musa jangwani, na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, vilikuwapo wakati huo mahali pa juu pa Gibeoni.[#1 Nya 16:39; 1 Fal 3:4; 2 Nya 1:3]

30Wala Daudi hakuweza kwenda mbele yake ili kumwuliza Mungu; kwa sababu aliona hofu kwa ajili ya upanga wa yule malaika wa BWANA.[#2 Sam 6:9; 1 Nya 13:12; Ayu 13:21; 21:6; Zab 119:120]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania