1 Mambo ya Nyakati 29

1 Mambo ya Nyakati 29

Matoleo kwa ujenzi wa hekalu

1Kisha mfalme Daudi akawaambia kusanyiko lote, Sulemani mwanangu, ambaye Mungu amemchagua peke yake, angali ni mchanga bado na hana uzoefu, nayo kazi hii ni kubwa; kwani nyumba hii ya enzi si kwa mwanadamu, ila kwa BWANA, Mungu.[#1 Fal 3:7; 1 Nya 22:5; Mit 4:3]

2Basi kwa uwezo wangu wote nimeiwekea akiba nyumba ya Mungu wangu, dhahabu kwa vitu vya dhahabu, na fedha kwa vitu vya fedha, na shaba kwa vitu vya shaba, na chuma kwa vitu vya chuma, na miti kwa vitu vya miti; vito vya shohamu, na vya kujazia, vito vya njumu, na vya rangi mbalimbali, na mawe ya thamani ya kila namna, na marumaru tele.[#Kut 28:9; Isa 54:11,12; Ufu 21:18]

3Nami tena kwa kuwa nimeiwekea nyumba ya Mungu wangu shauku yangu, nami ninayo hazina yangu mwenyewe ya dhahabu na fedha, ninaitoa kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, zaidi ya hiyo akiba niliyoiwekea tayari nyumba takatifu;[#Zab 26:8; 27:4; 84:1; Mit 3:9]

4yaani, talanta elfu tatu za dhahabu, za dhahabu ya Ofiri, na talanta elfu saba za fedha iliyosafika, ya kuzifunikiza kuta za nyumba;[#1 Fal 9:28; 2 Nya 8:18; Ayu 22:24]

5ya dhahabu, kwa vitu vya dhahabu, na ya fedha kwa vitu vya fedha, na kwa kazi za kila namna zitakazofanywa kwa mikono ya mafundi. Ni nani basi ajitoaye kwa moyo ili ajiweke wakfu leo kwa BWANA?

6Ndipo wakuu wa koo za mababa, na wakuu wa makabila ya Israeli, na makamanda wa maelfu na wa mamia, pamoja na wasimamizi wa kazi ya mfalme, wakajitoa kwa hiari yao;[#1 Nya 27:1,25]

7nao wakatoa, kwa ajili ya utumishi wa nyumba ya Mungu, dhahabu talanta elfu tano, na darkoni elfu kumi, na fedha talanta elfu kumi, na shaba talanta elfu kumi na nane, na chuma talanta elfu mia moja.[#29:7 Darkoni, ni sarafu, thamani yake ni kama shilingi 21.]

8Na wale walioonekana kuwa na vito vya thamani wakavitoa vitiwe katika hazina ya nyumba ya BWANA, chini ya mkono wa Yehieli, Mgershoni.[#1 Nya 26:21]

9Ndipo hao watu wakafurahi, kwa sababu wametoa kwa hiari yao wenyewe, kwa moyo wao wote, kwa hiari yao wenyewe, wamemtolea BWANA; mfalme Daudi naye akafurahi sana.[#1 Fal 8:61; 2 Kor 9:7]

Daudi amshukuru Mungu

10Kwa hiyo Daudi akamhimidi BWANA, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele.[#1 Fal 8:15,16; 2 Nya 6:4; Zab 72:18; Eze 3:12]

11Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na ushindi, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote.[#Dan 4:34,35; Mt 6:13; 1 Tim 1:17; Ufu 5:13]

12Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote.[#Kum 8:18; 1 Sam 2:7,8; Zab 75:6; Mit 10:22; Rum 11:36; Yak 1:17]

13Basi sasa, Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu.

14Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea.

15Kwani sisi tu wageni na wapitaji mbele zako, kama walivyokuwa baba zetu wote; siku zetu duniani ni kama kivuli, na hakuna tumaini la kuishi.[#Mwa 47:9; Zab 39:12; Ebr 11:13; 1 Pet 2:11; Ayu 14:2; Zab 90:9; 102:11; 144:4]

16Ee BWANA, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yote inatoka mkononi mwako, na yote ni yako wewe.

17Nami ninajua, Mungu wangu, ya kuwa wewe wajaribu moyo, nawe wapendezwa na unyofu. Nami katika unyofu wa moyo wangu nimeyatoa haya yote kwa hiari yangu mwenyewe; nami sasa nimeona kwa furaha watu wako, waliopo hapa, wakikutolea kwa hiari yao.[#Kum 8:2; 1 Sam 16:7; Zab 7:9; 1 Nya 28:9; Mit 16:2; 21:2; Yer 17:10; Ebr 4:13; Zab 11:7; Mit 11:20]

18Ee BWANA, Mungu wa Abrahamu, na wa Isaka, na wa Israeli, baba zetu, ulidumishe jambo hili milele katika fikira za mawazo ya mioyo ya watu wako, ukaiongoze mioyo yao kwako;[#Zab 10:17; Yer 10:23]

19naye Sulemani mwanangu, umjalie ili kwa moyo wote, azishike amri zako, na shuhuda zako, na maagizo yako, akayatende hayo yote na kuijenga nyumba hii ya enzi, niliyoiwekea akiba.[#Zab 72:1; 1 Nya 22:14]

20Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, Haya, mhimidini BWANA, Mungu wenu. Basi kusanyiko lote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao, wakainamisha vichwa vyao, wakamsujudia BWANA, na mfalme naye.

Sulemani atawazwa kuwa mfalme

21Siku ya pili yake, wakamtolea BWANA dhabihu, wakamchinjia BWANA sadaka ya kuteketezwa, yaani, ng'ombe elfu moja, na kondoo dume elfu moja, na wana-kondoo elfu moja, pamoja na sadaka zao za vinywaji, na dhabihu nyingi kwa ajili ya Israeli wote;

22wakala na kunywa mbele za BWANA siku ile, kwa furaha kuu. Wakamtawaza Sulemani, mwana wa Daudi, mara ya pili, wakamtia mafuta mbele za BWANA, awe mkuu, na Sadoki awe kuhani.

23Ndipo Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha BWANA, awe mfalme badala ya Daudi babaye, akafanikiwa; nao Israeli wote wakamtii.

24Nao wakuu wote, na mashujaa, na wana wote wa mfalme Daudi nao, wakaahidi kuwa watiifu kwa mfalme Sulemani.[#Mwa 24:2; 47:29; 2 Nya 30:8; Eze 17:18]

25Naye BWANA akamtukuza Sulemani mno machoni pa Israeli wote, akampa fahari ya kifalme ya kumpita mfalme awaye yote aliyekuwa kabla yake katika Israeli.[#1 Fal 3:13; 2 Nya 1:12; Mhu 2:9; Dan 5:18,19; Ebr 2:9]

Muhtasari wa utawala wa Daudi

26Basi Daudi, mwana wa Yese, akawa mfalme juu ya Israeli wote.

27Na wakati aliotawala juu ya Israeli, ulikuwa miaka arobaini; miaka saba alitawala Hebroni, na miaka thelathini na mitatu akatawala Yerusalemu.[#2 Sam 5:4,5; 1 Fal 2:11]

28Akafa akiwa mzee sana, mwenye maisha marefu, mali na heshima; naye Sulemani mwanawe akatawala badala yake.[#Mwa 15:15; 25:8; Hes 23:10; 1 Nya 23:1; Ayu 5:26; Mdo 13:36]

29Basi habari za mfalme Daudi, mwanzo hadi mwisho, angalia, zimeandikwa katika kumbukumbu za Samweli, mwonaji, na katika kumbukumbu za Nathani, nabii, na katika kumbukumbu za Gadi, mwonaji;

30zikisimulia kuhusu kutawala kwake kote na nguvu zake, na mambo yote yaliyompata yeye, na Israeli, na falme zote za nchi.[#Dan 2:21]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania