2 Mambo ya Nyakati 18

2 Mambo ya Nyakati 18

Mikaya awatabiria kushindwa

1Basi, Yehoshafati alikuwa na mali na heshima tele, tena alifanya maridhiano ya ndoa na Ahabu.[#Kum 8:10,18; 1 Sam 2:7,30; 1 Fal 3:13; 1 Nya 29:11,12; 2 Nya 17:5; Zab 112:2-9; Mit 3:13,16; 4:5-8; Mhu 5:19; 1 Tim 4:8; Mwa 6:2; 2 Fal 8:18; 2 Kor 6:14]

2Hata baada ya miaka kadhaa akamshukia Ahabu huko Samaria. Ahabu akamchinjia kondoo na ng'ombe tele, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, akamshawishi ili apande pamoja naye waende Ramoth-gileadi.[#1 Fal 22:2; 2 Nya 19:2]

3Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwambia Yehoshafati, mfalme wa Yuda, Je! Utakwenda nami mpaka Ramoth-gileadi? Akamjibu, Mimi ni kama wewe, na watu wangu kama watu wako; nasi tutakuwa pamoja nawe vitani.

4Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, lakini kwanza umwulize BWANA ushauri.[#1 Sam 23:2-9; 2 Sam 2:1; 1 Fal 22:5,6; 2 Nya 34:26; Yer 21:2; Eze 20:3]

5Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya manabii, watu mia nne; akawaambia, Je! Tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Wakasema, Kwea; kwa kuwa Mungu atautia mkononi mwa mfalme.[#Yer 23:17; Eze 13:3; Mt 23:16-19]

6Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii mwingine wa BWANA, ili tumwulize yeye?

7Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza ya BWANA; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema kamwe, ila siku zote mabaya; naye ndiye Mikaya mwana wa Imla. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivyo.

8Ndipo mfalme wa Israeli akamwita kamanda mmoja, akasema, Mlete hima Mikaya mwana wa Imla.

9Basi, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wamekaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, wakikaa penye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la Samaria; nao manabii wote wakafanya unabii mbele yao.

10Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, BWANA asema hivi, Kwa hizi utawasukuma Washami, hata watakapoangamia.

11Na manabii wote wakatoa unabii huo, wakisema, Kwea Ramoth-gileadi, ukafanikiwe, kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme.

12Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia, maneno ya manabii kwa kupatana yasema mema kwa mfalme; neno lako basi na liwe kama mojawapo lao, ukaseme mema.

13Mikaya akasema, Kama aishivyo BWANA, neno lile atakalolinena Mungu wangu, ndilo nitakalolinena.[#Hes 22:18,20,35; 23:12,26; 24:13; 1 Fal 22:14; Yer 23:8; 42:4; Eze 2:7; Mik 2:6,7; Mdo 20:27; 1 Kor 11:23; 1 The 2:4]

14Na alipokuja kwa mfalme, mfalme akamwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Akasema, Kweeni, mkafanikiwe; nao watatiwa mikononi mwenu.[#1 Fal 18:27; Amo 4:4]

15Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe, usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la BWANA?

16Akasema, Niliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji; BWANA akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.

17Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?

18Mikaya akasema, Sikieni basi neno la BWANA; Nilimwona BWANA ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kulia na wa kushoto.[#Zab 103:20; Dan 7:9]

19BWANA akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.

20Akatoka pepo, akasimama mbele za BWANA, akasema, Mimi nitamdanganya. BWANA akamwambia, Jinsi gani?[#Ayu 1:6; 2 The 2:9]

21Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kufanikiwa pia; ondoka, ukafanye hivyo.[#1 Fal 22:21,22; Hos 4:12; Zek 13:2; Yn 8:44]

22Basi sasa, angalia, BWANA ametia pepo wa uongo vinywani mwa manabii wako hawa; naye BWANA amenena mabaya juu yako.[#Ayu 12:16; Isa 19:14; Eze 14:9; Mt 24:24,25; 2 The 2:9-11; Yak 1:13]

23Ndipo akakaribia Zedekia mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Alitokaje kwangu Roho ya BWANA ili aseme na wewe?[#Yer 20:2; Mk 14:65; Mdo 23:2]

24Mikaya akasema, Angalia utaona siku ile, utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche.

25Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme;

26mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni huyu gerezani, mkamlishe chakula cha shida, na maji ya shida, hadi nitakaporudi kwa amani.[#1 Sam 25:21; 2 Nya 16:10; Lk 23:2]

27Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, BWANA hakusema kupitia kwangu. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.

Kushindwa kwa Ahabu na kifo chake

28Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-gileadi.

29Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha; nao wakaingia vitani.[#1 Sam 28:8; Mit 10:24]

30Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru makamanda wa magari yake, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake.

31Ikawa makamanda wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Mfalme wa Israeli ni huyu. Basi wakamgeukia ili wapigane naye; lakini Yehoshafati akalia, na BWANA akamsaidia; Mungu akawaondoa kwake.[#Mit 13:20; Zab 46:1]

32Ikawa, makamanda wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate.

33Na mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari, Geuza gari, uniondoe katika vita; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.

34Pigano likazidi siku ile; lakini mfalme wa Israeli akajitegemeza garini juu ya Washami hata jioni; akafa kama wakati wa kuchwa kwa jua.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania