The chat will start when you send the first message.
1Basi Sulemani alipomaliza maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa BWANA ukaijaza nyumba.[#1 Fal 8:54; Isa 65:24; Dan 9:20; Mdo 4:31; 16:25,26; Mwa 15:17; Law 9:23,24; Amu 6:21; 1 Fal 18:38; 1 Nya 21:26; 2 Nya 5:13; Eze 10:3; Ufu 21:23]
2Wala makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa BWANA, kwa kuwa utukufu wa BWANA umeijaza nyumba ya BWANA.[#2 Nya 5:14]
3Wana wa Israeli wote walipoona ule moto ukishuka, utukufu wa BWANA ulipokuwa katika nyumba, wakasujudu kifudifudi mpaka sakafuni, wakaabudu, wakamshukuru BWANA, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele.[#2 Nya 5:13; 20:21; Zab 103:17; 136:1]
4Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za BWANA.[#1 Fal 8:62]
5Mfalme Sulemani akatoa sadaka ya ng'ombe elfu ishirini na mbili, na kondoo elfu mia moja na ishirini. Ndivyo mfalme na watu wote walivyoifanya wakfu nyumba ya Mungu.
6Makuhani wakasimama kwenye nafasi zao walipoagizwa; Walawi nao pamoja na vinanda vya BWANA, alivyovifanya Daudi mfalme, ili kumshukuru BWANA, kwa maana fadhili zake ni za milele, hapo aliposifu Daudi kwa mikono yao; nao makuhani wakapiga panda mbele yao; nao Israeli wote wakasimama.[#1 Nya 15:16; 2 Nya 5:12]
7Tena Sulemani akaitakasa behewa katikati, iliyokuwa mbele ya nyumba ya BWANA; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba aliyoifanya Sulemani haikutosha kuzipokea sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na mafuta.[#Hes 16:37; 1 Fal 8:64; 2 Nya 36:14; Ebr 13:10-12]
8Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, toka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, muda wa siku saba.[#1 Fal 8:65; Mwa 15:18; Yos 13:3]
9Siku ya nane wakaita kusanyiko la makini; kwa maana waliadhimisha kuitakasa madhabahu siku saba, na sikukuu siku saba.
10Akawaruhusu watu waende hemani kwao siku ya ishirini na tatu, ya mwezi wa saba, wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema wote BWANA aliomfanyia Daudi, na Sulemani, na Israeli watu wake.[#1 Fal 8:66]
11Hivyo Sulemani akaimaliza nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme; na yote yaliyomwingia Sulemani moyoni ayafanye nyumbani mwa BWANA, na nyumbani mwake mwenyewe, akayafanikisha.[#1 Fal 9:1]
12BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu.[#Mwa 12:7; Kum 12:5; Zab 78:68,69; 132:13,14]
13Nikizifunga mbingu isiwepo mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwatumia watu wangu tauni;[#2 Nya 6:26]
14ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekeza, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.[#Yak 4:10; 2 Nya 6:27]
15Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.[#2 Nya 6:40]
16Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima.[#2 Nya 6:6]
17Nawe, ukienda mbele yangu kama alivyokwenda Daudi baba yako, ufanye kulingana na yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu;[#1 Fal 9:4]
18ndipo nitakithibitisha kiti cha enzi cha ufalme wako, kama nilivyoagana na Daudi baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kutawala katika Israeli.[#2 Nya 6:16]
19Lakini mkigeuka, na kuziacha sheria zangu na amri zangu nilizoweka mbele yenu, mkienda, na kuitumikia miungu mingine, na kuiabudu;[#Law 26:14; Kum 28:15]
20ndipo nitawang'oa katika nchi yangu niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaiondosha itoke mbele zangu, nami nitaifanya kuwa mithali na tukano katikati ya watu wote.[#Zab 5:5]
21Na nyumba hii, iliyo juu, kila apitaye ataona ushangao, atasema, Mbona BWANA ameitendea hivi nchi hii, na nyumba hii?[#Yer 7:14; 22:8; Omb 2:15; Kum 29:24]
22Nao watajibu, Kwa sababu walimwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine, wakaiabudu, na kuitumikia; kwa hiyo ameyaleta mabaya haya yote juu yao.[#Amu 2:13; 2 Fal 17:18; 2 Nya 36:16; Dan 9:12]