2 Wakorintho 12

2 Wakorintho 12

Maono na mafunuo ya Paulo

1Sina budi kujisifu, ijapokuwa haipendezi; lakini nitafikia maono na mafunuo ya Bwana.

2Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu.

3Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua);

4ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haistahili mwanadamu ayaseme.[#Lk 23:43; Ufu 2:7]

5Kuhusu mtu kama huyo nitajisifu; lakini kwa ajili ya nafsi yangu sitajisifu, isipokuwa kuhusu udhaifu wangu.[#2 Kor 11:30]

6Maana kama ningetaka kujisifu singekuwa mpumbavu, kwa sababu nitasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu asinihesabie zaidi ya hayo ayaonayo kwangu au kuyasikia kwangu.[#2 Kor 10:8; 11:16]

7Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nilipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi.[#Ayu 2:6]

8Kwa ajili ya kitu hicho nilimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke.

9Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.

10Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na matusi, na matatizo, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.[#Flp 4:13]

Shauku ya Paulo kwa kanisa la Korintho

11Nimekuwa mpumbavu, ninyi mmenilazimisha. Maana ilinipasa nisifiwe na ninyi; kwa sababu sikuwa duni ya mitume walio wakuu kwa lolote, nijapokuwa si kitu.[#2 Kor 11:5]

12Kweli ishara za mtume zilitendwa katikati yenu katika subira yote, kwa ishara na maajabu na miujiza.[#Rum 15:19]

13Maana ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila kwa kuwa mimi sikuwalemea? Mnisamehe kosa hili.[#2 Kor 11:19]

14Tazama, hii ni mara ya tatu ya mimi kuwa tayari kuja kwenu, wala sitawalemea. Maana sivitafuti vitu vyenu, bali nawatafuta ninyi; maana haiwapasi watoto kuweka akiba kwa wazazi, bali wazazi kwa watoto.[#2 Kor 13:1]

15Nami nitakuwa radhi kutumia na kutumiwa kwa ajili yenu. Je! Kadiri nizidivyo kuwapenda sana, ninapungukiwa kupendwa?[#Flp 2:17]

16Lakini na iwe hivyo, mimi sikuwalemea; bali kwa kuwa mwerevu niliwapata kwa hila.

17Je! Mtu yeyote niliyemtuma kwenu, kwa mtu huyo niliwatoza kitu?

18Nilimwonya Tito, nikamtuma ndugu yule pamoja naye. Je! Tito aliwatoza kitu? Je! Hatukuenenda kwa Roho yeye yule na katika nyayo zile zile?[#2 Kor 8:6,16-18]

19Mnadhani hata sasa ya kuwa najitetea kwenu! Mbele za Mungu twanena katika Kristo. Na hayo yote, wapenzi, ni kwa ajili ya kuwajenga ninyi.

20Maana nachelea, nisije nikawakuta si kama vile nitakavyo kuwakuta, nikaonekana kwenu si kama vile mtakavyo; nisije nikakuta labda fitina na wivu, na ghadhabu, na ugomvi, na masingizio, na manong'onezo, na majivuno, na ghasia;[#2 Kor 10:2; 1 Kor 4:6]

21nami nitakapokuja tena, Mungu wangu asije akanidhili kwenu, nami nikawasikitikia wengi waliokosa tangu hapo, wasiutubie uchafu, na uasherati, na uovu walioufanya.[#2 Kor 2:1; 13:2]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania