The chat will start when you send the first message.
1Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.
2Tupeni nafasi mioyoni mwenu. Hatukumdhulumu mtu yeyote, wala kumharibu mtu, wala kumkosea mtu.[#2 Kor 12:17; Mdo 20:33]
3Sisemi neno hilo ili niwahukumu ninyi kuwa na hatia; kwa maana nimetangulia kusema, ya kwamba ninyi mmo mioyoni mwetu hata kwa kufa pamoja, na kuishi pamoja.[#2 Kor 6:11-13]
4Ninao ujasiri mwingi kwenu; naona fahari kuu juu yenu. Nimejaa faraja, katika dhiki yetu yote nimejaa furaha ya kupita kiasi.
5Kwa maana hata tulipokuwa tumefika Makedonia miili yetu haikupata nafuu; bali tuliteseka kotekote; nje palikuwa na vita, ndani hofu.[#2 Kor 2:13; Mdo 20:1,2]
6Lakini Mungu, mwenye kuwafariji wanyonge, alitufariji kwa kuja kwake Tito.[#2 Kor 1:3,4; 2:13; Zab 113:6; 138:6; Isa 66:2]
7Wala si kwa kuja kwake tu, bali kwa zile faraja nazo alizofarijiwa kwenu, akituarifu habari ya shauku yenu, na maombolezo yenu, na bidii yenu kwa ajili yangu, hata nikazidi kufurahi.
8Kwa sababu, ijapokuwa niliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nilijuta, naona ya kwamba barua ile iliwahuzunisha, ingawa ni kwa muda tu.[#2 Kor 2:4]
9Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lolote.
10Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba iletayo wokovu isiyo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.[#Mt 27:3-5; Ebr 12:17]
11Maana, angalieni, kuhuzunishwa huko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii gani ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo.
12Basi, ijapokuwa niliwaandikia, sikuandika kwa ajili yake yeye aliyedhulumu, wala si kwa ajili yake yeye aliyedhulumiwa, bali ili bidii yenu kwa ajili yetu ipate kudhihirishwa kwenu mbele za Mungu.
13Kwa hiyo tulifarijiwa. Tena katika kufarijiwa kwetu tulifurahi sana kupita kiasi kwa sababu ya furaha ya Tito; maana roho yake imeburudishwa na ninyi nyote.
14Kwa maana, ikiwa nimejisifu mbele yake katika neno lolote kwa ajili yenu, sikutahayarishwa; bali, kama tulivyowaambia mambo yote kwa kweli, vivyo hivyo na kujisifu kwetu kwa Tito kulikuwa kweli.
15Na mapenzi yake kwenu yamekuwa mengi kupita kiasi, akumbukapo kutii kwenu ninyi nyote, jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu na kutetemeka.[#2 Kor 2:9]
16Nafurahi, kwa sababu katika kila neno nina moyo mkuu kwa ajili yenu.