The chat will start when you send the first message.
1Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia;[#Rum 15:26]
2maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao.
3Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao;
4wakituomba sana pamoja na kutusihi kuhusu neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu.[#2 Kor 9:1; Mdo 11:29]
5Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu.
6Hata tukamwonya Tito kuwatimilizia neema hii kwenu kama vile yeye alivyotangulia kuianzisha.
7Lakini kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia.[#1 Kor 1:5; 16:1,2]
8Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu.
9Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.[#Mt 8:20]
10Nami katika neno hili natoa ushauri wangu; maana neno hili lawafaa ninyi mliotangulia, yapata mwaka, sio tu kutenda bali hata kutamani kutenda pia.
11Lakini sasa timizeni kule kutenda nako, ili kama vile mlivyokuwa tayari kutamani kutenda, vivyo hivyo mkawe tayari na kutimiza, kwa kadiri ya mlivyo navyo.
12Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo.[#Mit 3:27,28; Mk 12:43]
13Maana sisemi hayo, ili wengine wapate raha nanyi mpate dhiki;
14bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe sawasawa.[#2 Kor 9:12]
15Kama ilivyoandikwa, Aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa.[#Kut 16:18]
16Lakini ahimidiwe Mungu atiaye bidii ile ile kwa ajili yenu katika moyo wa Tito.
17Maana aliyapokea kweli yale maonyo; tena, huku akizidi kuwa na bidii, alisafiri kwenda kwenu kwa hiari yake mwenyewe.
18Na pamoja naye tukamtuma ndugu yule ambaye sifa zake katika Injili zimeenea makanisani kote.
19Wala si hivyo tu, bali alichaguliwa na makanisa asafiri pamoja nasi katika jambo la neema hii, tunayoitumikia, ili Bwana atukuzwe, ukadhihirike utayari wetu.[#Gal 2:10]
20Tukijiepusha na neno hili, mtu asije akatulaumu kuhusu karama hii tunayoitumikia;
21tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu, ila na mbele ya wanadamu.[#Mit 3:4]
22Nasi pamoja nao tumemtuma ndugu yetu tuliyemwona mara nyingi kuwa ana bidii katika mambo mengi, na sasa ana bidii zaidi sana kwa sababu ya tumaini kuu alilo nalo kwenu.
23Basi mtu akitaka habari za Tito, yeye ni mshirika wangu, na mtenda kazi pamoja nami kwa ajili yenu; tena akitaka habari za ndugu zetu, wao ni Mitume wa makanisa, na utukufu wa Kristo.[#2 Kor 7:13; 12:18; Rum 16:7]
24Basi waonyesheni mbele ya makanisa hakika ya upendo wenu, na sababu ya kujisifu kwetu kwa ajili yenu.[#2 Kor 7:14]