2 Wafalme 24

2 Wafalme 24

Yuda yatawaliwa na adui

1Katika siku zake akakwea Nebukadneza, mfalme wa Babeli, na Yehoyakimu akawa mtumishi wake muda wa miaka mitatu; kisha, akageuka, akamwasi.[#Law 26:25; 2 Fal 17:5; 2 Nya 36:6; Yer 25:1,9; 46:2; Dan 1:1; #24:1 Au, Nebukadreza.]

2Naye BWANA akatuma juu yake vikosi vya Wakaldayo, na vikosi vya Washami, na vikosi vya Wamoabi, na vikosi vya wana wa Amoni, akawatuma juu ya Yuda ili kuiharibu, sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa mkono wa watumishi wake manabii.[#Kum 28:49,50; Yer 25:9; 32:28; Eze 19:8; 2 Fal 20:17; 21:12; 23:27]

3Hakika kwa amri ya BWANA mambo hayo yalimpata Yuda, ili waondoshwe kutoka machoni pake, kwa sababu ya dhambi zake Manase, kadiri ya yote aliyoyafanya;[#2 Fal 21:2,11; 23:26]

4tena kwa ajili ya damu zisizo na hatia alizozimwaga; kwani aliujaza Yerusalemu damu zisizo na hatia; wala BWANA hakukubali kusamehe.[#2 Fal 21:16; Yer 15:1; Omb 3:42]

5Basi mambo yote ya Yehoyakimu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda?

6Yehoyakimu akalala na babaze; na mwanawe Yekonia akatawala mahali pake.[#2 Nya 36:6; #24:6 Au, Yehoyakini.]

7Basi mfalme wa Misri hakuja tena kutoka nchi yake; kwa kuwa mfalme wa Babeli alikuwa amemnyang'anya nchi, tangu kijito cha Misri mpaka mto wa Frati, yote aliyokuwa nayo mfalme wa Misri.[#Yer 37:5; 46:2]

Kutawala na kutekwa kwa Yekonia

8Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa Yerusalemu.[#1 Nya 3:16; Yer 24:1; 22:24]

9Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake.

10Wakati ule watumishi wa Nebukadneza mfalme wa Babeli wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji ukahusuriwa.[#Dan 1:1]

11Na Nebukadneza, mfalme wa Babeli, akaufikia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru.

12Na Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka akamwendea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maofisa wake; mfalme wa Babeli akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake.[#Yer 24:1; 29:1,2; Eze 17:12; Yer 25:1; 2 Fal 25:27; Yer 52:28]

Yerusalemu watekwa

13Akatoa huko hazina zote za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme, akavikatakata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani, mfalme wa Israeli, alivitengeneza katika hekalu la BWANA, kama BWANA alivyosema.[#Isa 39:6; Dan 5:2; 1 Fal 14:15; Yer 20:5]

14Akawachukua mateka watu wa Yerusalemu wote pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu kumi; na mafundi wote, na wafua chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa wanyonge wa watu wa nchi.[#2 Nya 36:9,10; Yer 24:1; 39:10; 40:7; 1 Sam 13:19,22; 2 Fal 25:12]

15Akamchukua Yekonia mpaka Babeli; na mama yake mfalme, na wake zake mfalme, na maofisa wake, na wakuu wa nchi, aliwachukua mateka toka Yerusalemu mpaka Babeli.[#2 Nya 36:10; Est 2:6; Yer 22:24,25; Eze 1:2]

16Na mashujaa wote, watu elfu saba, na mafundi na wafua chuma elfu moja, wote pia wenye nguvu, tayari kwa vita, hao wote mfalme wa Babeli aliwachukua mateka mpaka Babeli.[#Yer 52:28]

Sedekia atawala Yuda

17Mfalme wa Babeli akamtawaza Matania, ndugu ya baba yake, awe mfalme badala yake, akalibadili jina lake, akamwita Sedekia.[#Yer 37:1; 1 Nya 3:15; 2 Nya 36:10,11; 2 Fal 23:34; 2 Nya 36:4]

18Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali, binti Yeremia wa Libna.[#2 Nya 36:11; Yer 37:1; 52:1; 2 Fal 23:31]

19Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyafanya Yehoyakimu.

20Maana kwa sababu ya hasira ya BWANA mambo hayo yalitokea katika Yerusalemu na katika Yuda, hata alipokuwa amewaondosha wasiwe mbele ya uso wake; naye Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli.[#Kum 4:24; 29:27,28; 2 Fal 22:16,17; 23:26,27; Eze 17:15; 2 Nya 36:13]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania