2 Wafalme 4

2 Wafalme 4

Elisha amsaidia mjane

1Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha BWANA; na aliyemdai amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.[#1 Fal 20:35; 2 Fal 2:3-7; Kut 21:2; Law 25:39; Kum 15:12-18; Neh 5:1-13; Yer 34:8-18; Mt 18:25]

2Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta.[#1 Fal 17:12]

3Akasema, Nenda, ukaazime vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usiazime vichache.[#2 Fal 3:16]

4Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge.

5Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina.

6Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma.[#Mt 14:20]

7Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Nenda ukayauze mafuta haya, ulipe deni lako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.[#Rum 13:8]

Elisha amfufua mtoto wa Mshunami

8Hata ikawa siku moja, Elisha alikwenda Shunemu; na huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo; naye akamshurutisha aje ale chakula. Ikawa kila alipopita njia ile, huingia kula chakula.[#Yos 19:18; 1 Sam 28:4]

9Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu.[#Mit 31:10,11]

10Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo.[#Mt 10:41,42; 25:40; Rum 12:13; Ebr 13:2]

11Ikawa siku moja akafika huko, akaingia katika chumba kile akalala.

12Akamwambia Gehazi mtumishi wake, Mwite yule Mshunami. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mbele yake.

13Akamwambia, Sema naye sasa, Tazama, wewe umetutunza sana namna hii; utendewe nini basi? Je! Uombewe neno kwa mfalme, au kwa kamanda wa jeshi? Yule mwanamke akamjibu, Mimi ninakaa katika watu wangu mwenyewe.

14Akasema, Basi, atendewe nini? Gehazi akajibu, Hakika hana mwana, na mumewe ni mzee.

15Akamwambia, Kamwite. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mlangoni.

16Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa Mungu, usiniambie mimi mjakazi wako uongo.[#Mwa 18:10,14]

17Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto wa kiume wakati huo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia.

18Hata yule mtoto alipokua, ikawa siku moja alitoka kwenda kwa baba yake kwa wavunao.

19Akamwambia baba yake, Kichwa changu! Kichwa changu! Naye akamwambia mtumishi wake, Mchukue kwa mama yake.

20Akamchukua, akampeleka kwa mama yake, naye akakaa magotini mwake hata adhuhuri, kisha akafa.

21Mamaye akapanda juu, akamlaza juu ya kitanda cha yule mtu wa Mungu, akamfungia mlango, akatoka.

22Kisha akamwita mumewe, akasema, Tafadhali, uniletee mtu mmoja wa watumishi, na punda mmoja, ili nimwendee yule mtu wa Mungu kwa haraka, na kurudi tena.

23Akasema, Kwa nini kumwendea leo? Sio mwandamo wa mwezi, wala sabato. Akasema, Si neno.

24Akatandika punda, akamwambia mtumishi wake, Mwendeshe, twendelee mbele. Usinipunguzie mwendo, nisipokuambia.

25Basi akaenda, akafika kwa yule mtu wa Mungu, katika mlima wa Karmeli. Ikawa, yule mtu wa Mungu alipomwona kwa mbali, akamwambia Gehazi mtumishi wake, Tazama, Mshunami yule kule.[#2 Fal 2:25]

26Tafadhali piga mbio sasa kwenda kumlaki, ukamwambie, Hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto hajambo? Akajibu, Hawajambo.

27Naye alipofika kwa yule mtu wa Mungu kilimani, alimshika miguu. Gehazi akakaribia amwondoe; lakini mtu wa Mungu akamwambia, Mwache; maana roho yake ndani yake ina uchungu; na BWANA amenificha, wala hakuniambia.[#Mt 15:23; 1 Sam 1:10]

28Yule mwanamke akasema, Je! Niliomba mwana kwa bwana wangu? Mimi sikusema, Usinidanganye?

29Ndipo Elisha akamwambia Gehazi, Jikaze viuno, ukachukue fimbo yangu mkononi mwako, ukaende zako; ukikutana na mtu, usimsalimu; na mtu akikusalimu, usimjibu; ukaweke fimbo yangu juu ya uso wa mtoto.[#1 Fal 18:46; 2 Fal 9:1; Lk 10:4; Kut 7:19; 14:16; 2 Fal 2:8,14; Mdo 19:12]

30Na mama yake yule mtoto akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Basi akaondoka, akamfuata.[#2 Fal 2:2]

31Na Gehazi akawatangulia, akaiweka ile fimbo juu ya uso wa mtoto; lakini hapakuwa na sauti, wala majibu. Basi akarudi ili kumlaki, akamwambia, akisema, Mtoto hakuamka.[#Yn 11:11]

32Basi Elisha alipofika nyumbani, tazama, mtoto amekwisha kufa, amelazwa kitandani pake.

33Basi akaingia ndani, akajifungia mlango, yeye na yule mtoto wote wawili, akamwomba BWANA.[#Mt 6:6; 1 Fal 17:20; Yak 5:16]

34Akapanda juu ya kitanda, akajilaza juu ya mtoto, akaweka kinywa chake juu ya kinywa chake, na macho yake juu ya macho yake, na mikono yake juu ya mikono yake; akajinyosha juu yake; mwili wake yule mtoto ukaanza kupata moto.[#Mdo 20:10]

35Kisha akarudi, akatembea nyumbani, huku na huko mara moja; akapanda, akajinyosha juu yake; na yule mtoto akapiga chafya mara saba, na mtoto akafumbua macho yake.[#1 Fal 17:21; 2 Fal 8:1]

36Akamwita Gehazi, akasema, Mwite yule Mshunami. Basi akamwita. Na alipofika kwake, Elisha akasema, Haya! Mchukue mwanao.

37Ndipo akaingia, akamwangukia miguuni akainama mpaka chini; kisha akamchukua mwanawe, akatoka.[#Ebr 11:35]

Elisha atakasa sufuria la matango

38Elisha akafika Gilgali tena; na kulikuwa na njaa katika nchi; na hao wana wa manabii walikuwa wakikaa mbele yake. Akamwambia mtumishi wake, Teleka sufuria kubwa, uwapikie wana wa manabii.[#Lk 10:39; Mdo 22:3]

39Na mmoja wao akaenda nje kondeni ili kuchuma mboga, akaona mtangomwitu, akayachuma matangomwitu, hata nguo yake ikawa imejaa, akaja akayapasuapasua sufuriani; kwa maana hawakuyajua.[#Mt 7:16]

40Basi wakawapakulia hao watu ili wale. Ikawa, walipokuwa katika kula chakula, wakapiga kelele, wakasema, Mauti imo sufuriani, Ee mtu wa Mungu. Wala hawakuweza kula.[#Kut 10:17]

41Lakini yeye akasema, Leteni unga. Naye akautupa ndani ya sufuria; akasema, Wapakulie watu, ili wale. Wala hakikuwamo kitu kibaya sufuriani.[#Kut 15:25; 2 Fal 2:21; 5:10; Yn 9:6]

Elisha alisha watu mia moja

42Tena, akaja mtu kutoka Baal-shalisha, akamletea mtu wa Mungu chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano guniani. Akasema, Uwape watu, ili wale.[#1 Sam 9:4; 1 Kor 9:11; Gal 6:6]

43Na mtumishi wake akasema, Je! Niwaandalie hiki watu mia moja? Lakini akasema, Uwape watu, ili wale; kwa kuwa BWANA asema hivi, Watakula na kusaza.[#Lk 9:13; Yn 6:9]

44Basi akawaandalia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la BWANA.[#Mt 14:20; 15:37; Yn 6:13; Mwa 18:14; Yer 32:17; Zek 8:6; Mt 19:26; Lk 1:37]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania