2Petro 3

2Petro 3

Ahadi ya kuja kwa Bwana

1Wapenzi, waraka huu ndio wa pili niwaandikiao ninyi; katika zote mbili naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha,[#2 Pet 1:13]

2mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu.[#Yud 1:17]

3Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,[#Yud 1:18; 1 Tim 4:1]

4na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali hiyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa.[#Isa 5:19; Eze 12:22; Mt 24:48]

5Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;[#Mwa 1:2,6-9; Mt 24:38; Zab 24:2]

6kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.[#Mwa 7:11,21; 2 Pet 2:5]

7Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.

8Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja.[#Zab 90:4]

9Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyodhani anakawia, bali huwavumilia, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikie toba.[#Hab 2:3; 1 Tim 2:4]

10Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.[#Mt 24:29,35,43; Lk 12:39; 1 The 5:2,3; Ufu 16:15; 20:11]

11Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa,

12mkiingojea hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka?[#Isa 34:4; Yud 1:5]

13Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.[#Isa 65:17; 66:22; Ufu 21:1,27]

Wosia wa mwisho na sifa kwa Mungu

14Kwa hiyo, wapenzi, mnapoyangojea mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane mkiwa na amani, bila doa wala dosari mbele yake.[#1 Kor 1:7,8; Yud 1:24]

15Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa;[#Rum 2:4; 1 Kor 3:10]

16akisema juu ya mambo haya kama afanyavyo katika barua zake zote pia, katika barua hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuyaelewa na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wapotoavyo Maandiko mengine, na kujiletea maangamizi wao wenyewe.

17Basi, wapenzi kwa kuwa mmejua hayo, jihadharini msije mkapotoshwa na kosa la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha uthabiti wenu.[#Mk 13:5,9,33]

18Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele.[#Yud 1:25]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania