The chat will start when you send the first message.
1Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, jemadari wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,[#Mt 8:5; Mdo 27:1]
2mtu mtauwa, mcha Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima.
3Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio![#Mdo 3:1]
4Akamkodolea macho, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.
5Sasa basi, tuma watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro.
6Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda.[#Mdo 9:43]
7Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa kati ya wale waliomhudumia daima;
8na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa.
9Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana;
10akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia,
11akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inateremshwa kwa pembe zake nne hadi chini;[#Mdo 11:5-17]
12ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani.
13Kisha sauti ikamjia, kusema, Inuka, Petro, uchinje ule.
14Lakini Petro akasema, La, hasha! Bwana, kwa maana sijawahi kula kitu kilicho kichafu au najisi.[#Eze 4:14; Law 11:1-47]
15Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi.[#Mt 15:11; Mk 7:15,19]
16Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni.
17Wakati Petro alipokuwa akisumbuka ndani ya nafsi yake, juu ya maana ya maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakatokeza. Walikuwa kukiulizia nyumba ya Simoni, wakiwa wamesimama mbele ya lango,
18wakaita; wakauliza kama Simoni aitwaye Petro anakaa humo.
19Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta.[#Mdo 13:2; 15:28]
20Basi inuka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma.
21Petro akawashukia wale watu, akanena, Mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani?
22Wakasema, Kornelio jemadari, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, ili asikilize kile utakachosema.
23Akawakaribisha wawe wageni wake.[#Mdo 11:12]
Hata siku ya pili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu waliokaa Yafa wakafuatana naye.
24Kesho yake wakaingia Kaisaria. Na Kornelio alikuwa akiwangojea, akiwa amekusanya jamaa zake na rafiki zake.
25Petro alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguuni mwake, akamsujudia.
26Lakini Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu.[#Mdo 14:15; Ufu 19:10]
27Na katika kusema naye akaingia ndani, akaona watu wengi wamekusanyika.
28Akawaambia, Ninyi mnajua ya kuwa si halali kwa mtu aliye Myahudi ashirikiane na mtu wa taifa lingine wala kumtembelea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu yeyote mchafu wala najisi.
29Kwa sababu hiyo nilikuja nilipoitwa, nisikatae; basi nawauliza, ni neno gani mliloniitia?
30Kornelio akasema, Siku tatu zilizopita, katika saa ii hii, yaani saa tisa, nilikuwa nikisali nyumbani mwangu; nikamwona mtu amesimama mbele yangu, akiwa amevaa nguo zinazong'aa,
31akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za Mungu.
32Basi, tuma watu kwenda Yafa, ukamwite Simoni aitwaye Petro, anakaa katika nyumba ya Simoni, mtengenezaji wa ngozi, karibu na pwani; naye akija atasema nawe.
33Mara nikatuma watu kwako, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tupo hapa mbele za Mungu, tupate kuyasikiliza maneno yote uliyoamriwa na Bwana.
34Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo;[#Kum 10:17; 1 Sam 16:7; Rum 2:11]
35bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.[#Yn 9:31; 10:16]
36Neno lile alilowapelekea wana wa Israeli akihubiri Habari Njema ya amani kwa Yesu Kristo (ndiye Bwana wa wote),[#Zab 107:20; 147:18; Isa 52:7; Nah 1:15; Mt 28:18]
37jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea kote katika Yudea likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliouhubiri Yohana;[#Mt 4:12-17]
38habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huku na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.[#Isa 61:1; Mt 3:16]
39Nasi tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini.[#Kum 21:22]
40Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika,[#1 Kor 15:4-7]
41si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndio sisi, tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu.[#Yn 14:19,22; 15:27; Mdo 1:4]
42Akatuagiza tuwahubirie watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu.[#Mdo 17:31; Rum 14:9,10; 1 Pet 4:5; 2 Tim 4:1]
43Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.[#Isa 33:24; 53:5,6; Yer 31:34; Eze 34:16; Dan 9:24]
44Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.
45Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.
46Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,[#Mdo 2:4; 19:6; Mk 16:17]
47Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?
48Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadhaa.[#Yn 4:40]