The chat will start when you send the first message.
1Wakashuka watu waliotoka Yudea wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamuwezi kuokoka.[#Law 12:3; Gal 5:2]
2Basi baada ya Paulo na Barnaba kushindana na watu hawa na kuhojiana nao sana, ndugu wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande kwenda Yerusalemu kwa mitume na wazee ili kuzungumza juu ya suala hilo.[#Mdo 11:30; Gal 2:1]
3Basi, wakisafirishwa na kanisa, wakapita kati ya nchi ya Foinike na Samaria, wakitangaza habari za kuongoka kwao Mataifa; wakawafurahisha ndugu sana.
4Walipofika Yerusalemu wakakaribishwa na kanisa na mitume na wazee, nao wakawaeleza mambo yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao.[#Mdo 14:27]
5Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika Torati ya Musa.
6Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulitafakari neno hilo.
7Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini.[#Mdo 10:1-43; 11:15]
8Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia, akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi;[#Mdo 2:4; 10:44]
9wala hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani.[#Mdo 10:34]
10Basi sasa mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulibeba.[#Gal 3:10; 5:1; Mt 11:30]
11Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao.[#Gal 2:16; Efe 2:4-10]
12Basi mkutano wote wakanyamaza, wakawasikiliza Barnaba na Paulo wakiwapasha habari za ishara na maajabu, ambayo Mungu aliyafanya kwa ujumbe wao katika Mataifa.
13Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni.[#Mdo 21:18; Gal 2:9]
14Simeoni ametueleza jinsi Mungu hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya jina lake.[#Mdo 15:7-9; Lk 1:68]
15Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa,[#Amo 9:11,12]
16Baada ya mambo haya nitarejea,[#Amo 9:11-12; Yer 12:15]
Nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka.
Nitajenga tena maanguko yake,
Nami nitaisimamisha;
17Ili wanadamu waliobakia wamtafute Bwana,
Na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao;
18Asema Bwana, ajulishaye hayo tangu milele.[#Isa 45:21]
19Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa;
20bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu.[#Kut 34:15-17; Law 3:17; 5:2; 17:10-16; 18:6-23; Mwa 9:4]
21Kwa maana tangu zamani za kale Musa anao watu wahubirio mambo yake; katika kila mji husomwa kila sabato katika masinagogi.[#Mdo 13:15]
22Basi ikawapendeza mitume na wazee na kanisa lote kuwachagua watu miongoni mwao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa Barsaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu katika ndugu. Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao,
23Mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa; Salamu.
24Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza;[#Mdo 15:1]
25sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,
26watu waliohatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
27Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao.
28Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima,[#Mt 23:4]
29yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu.
30Hata hao wakiisha kupewa ruhusa wakateremka kwenda Antiokia; na baada ya kuwakusanya jamii yote wakawapa ile barua.
31Nao walipokwisha kuisoma wakafurahi kwa ajili ya faraja ile.
32Tena Yuda na Sila, kwa kuwa wao wenyewe ni manabii, wakawausia ndugu kwa maneno mengi, wakawathibitisha.[#Mdo 11:27; 13:1]
33Na wakiisha kukaa huko muda, wakaruhusiwa na ndugu waende kwa amani kwa hao waliowatuma.
[
34Lakini Sila akaona vema kukaa huko.]
35Na Paulo na Barnaba wakakaa huko Antiokia, wakifundisha na kulihubiri neno la Bwana, pamoja na watu wengine wengi.
36Baada ya siku kadhaa Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Turejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wako hali gani.[#1 The 3:5]
37Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.[#Mdo 12:12,25]
38Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini.[#Mdo 13:13; Kol 4:10]
39Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akaabiri kwenda Kipro.[#Mdo 4:36; 13:4]
40Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe neema ya Bwana.
41Akapita katika Shamu na Kilikia akiyaimarisha makanisa.