Amosi 3

Amosi 3

Dhambi ya Israeli na adhabu yake

1Lisikieni neno hili alilolisema BWANA juu yenu, enyi wana wa Israeli, juu ya jamaa yote niliowapandisha kutoka nchi ya Misri, nikisema,

2Ni ninyi tu niliowajua katika jamaa zote zilizo duniani; kwa sababu hiyo nitawapatiliza ninyi maovu yenu yote.[#Eze 9:6; Dan 9:12; Mt 11:22; Lk 12:47; Rum 2:9; 1 Pet 4:17]

3Je! Watu wawili wanaweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?

4Je! Simba atanguruma mwituni, asipokuwa na mawindo? Mwanasimba atalia pangoni mwake, ikiwa hakupata kitu?

5Je! Ndege ataanguka mtegoni juu ya nchi, mahali asipotegewa tanzi? Mtego utafyatuka juu ya nchi, bila kunasa kitu chochote?

6Je! Tarumbeta itapigwa mjini, watu wasiogope? Mji utapatikana na hali mbaya, asiyoileta BWANA?[#Eze 33:3]

7Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.[#Mwa 6:13; Mit 3:32; Dan 9:22-27; Yn 15:15; Ufu 1:1,19]

8Simba amekwisha kunguruma, ni nani asiyeogopa? Bwana MUNGU amenena, ni nani awezaye neno ila kutabiri?[#1 Kor 9:16]

9Tangazeni habari katika majumba ya Ashdodi, na katika majumba ya nchi ya Misri, mkaseme, Kusanyikeni juu ya milima ya Samaria, katazameni, ni mishindo mikubwa kama nini iliyomo humo, na udhalimu mwingi kama nini uliomo ndani yake.

10Kwa maana hawajui kutenda haki, asema BWANA, hao wawekao akiba ya jeuri na unyang'anyi katika majumba yao.

11Basi, haya ndiyo asemayo Bwana MUNGU; Atakuwako adui, kuizunguka nchi pande zote; naye atazishusha chini nguvu zako zikutoke; na majumba yako yatatekwa nyara.[#2 Fal 17:6]

12Haya ndiyo asemayo BWANA; Kama vile mchungaji apokonyavyo kinywani mwa simba miguu miwili, au kipande cha sikio; ndivyo watakavyopokonywa wana wa Israeli, wakaao Samaria katika pembe ya kochi, na juu ya mito ya hariri ya kitanda.[#3:12 Katika Kiebrania maana si dhahiri.]

13Sikieni, mkashuhudu juu ya nyumba ya Yakobo, asema Bwana, MUNGU wa majeshi.

14Kwani katika siku ile nitakapompatiliza Israeli makosa yake, nitazipatiliza pia madhabahu za Betheli, na pembe za madhabahu zitakatiliwa mbali, na kuanguka chini.[#2 Fal 23:15]

15Nami nitaipiga nyumba ya wakati wa baridi pamoja na nyumba ya wakati wa joto; na hizo nyumba za pembe zitaangamia, nazo nyumba kubwa zitakuwa na mwisho, asema BWANA.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania