Kumbukumbu la Torati 1

Kumbukumbu la Torati 1

Kumbukumbu ya yaliyotokea Horebu

1Haya ndiyo maneno Musa aliyowaambia Israeli wote ng'ambo ya Yordani nyikani, katika jangwa la Araba lililoelekea Sufu, kati ya Parani, na Tofeli, na Labani, na Hazerothi, na Dizahabu.[#Hes 32:6,20,29; Yos 9:1; 22:4,7]

2Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka Horebu kwa njia ya mlima wa Seiri mpaka Kadesh-barnea.[#Hes 13:26; Kum 9:23]

3Ikawa mwaka wa arobaini, mwezi wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, Musa akawaambia wana wa Israeli kama yote aliyopewa na BWANA ya kuwaamuru;[#Hes 33:38]

4alipokwisha kumpiga Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, aliyekuwa akikaa Ashtarothi iliyo katika Edrei;[#Hes 21:21-35; Neh 9:22; Zab 135:11; 139:19]

5ni ng'ambo ya Yordani katika nchi ya Moabu, alipoanza Musa kufunua torati hii, akisema,

6BWANA, Mungu wetu, alituambia huko Horebu, akasema, Mmekaa katika mlima huu vya kutosha;[#Kut 3:11; 9:1; Hes 10:11]

7geukeni mshike safari yenu mwende nchi ya milima ya Waamori, na mahali pote palipo karibu ya hapo, katika hiyo Araba, na nchi ya vilima vilima, na huko Shefela, na Negebu, na pwani pwani, nchi ya Wakanaani, na Lebanoni, mpaka mto huo mkubwa, mto wa Frati.

8Angalieni, nimewawekea nchi mbele yenu, ingieni mkaimiliki nchi BWANA aliyowaapia baba zenu, Abrahamu, na Isaka, na Yakobo, kwamba atawapa na uzao wao baada yao.[#Mwa 12:7; 15:18; 28:13]

Viongozi wa makabila wateuliwa

9Nami wakati ule niliwaambia, nikasema, Mimi siwezi kuwachukua peke yangu.[#Kut 18:18; Hes 11:14]

10BWANA, Mungu wenu, amewafanya kuwa wengi, nanyi, angalieni, mmekuwa leo mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi.[#Mwa 15:5; 22:17; 28:14; Kut 32:13; Kum 10:22; 28:62; 1 Nya 27:23]

11BWANA, Mungu wa baba zenu, na awafanye kuwa wengi mara elfu kuliko mlivyo, na kuwabariki, kama alivyowaahidi.[#Mwa 22:17; 26:4; Kut 32:13]

12Nitachukuaje peke yangu mimi mwenyewe udhia wenu, na mzigo wenu, na ugomvi wenu?[#1 Fal 3:8; 2 Kor 11:28]

13Jitwalieni watu wenye akili na fahamu, watu wanaojulikana, kwa kadiri ya makabila yenu, nami nitawafanya wawe vichwa juu yenu.

14Nanyi mkanijibu, mkaniambia, Jambo ulilolisema ni jema la kufanya.

15Basi nikatwaa vichwa vya makabila yenu wenye akili, waliojulikana, nikawafanya wawe vichwa juu yenu, makamanda wa maelfu, na makamanda wa mamia, na makamanda wa hamsini hamsini, na makamanda wa kumi kumi, na wenye amri, kwa kadiri ya makabila yenu.

16Nikawaagiza wakati ule waamuzi wenu, nikawaambia, Sikilizeni ninyi maneno kati ya ndugu zenu, mkaamue kwa haki kati ya mtu na nduguye, na mgeni aliye pamoja naye.[#Kut 23:2-8; Yn 7:24; Law 24:22]

17Msitazame nafsi za watu katika hukumu; muwasikize wadogo na wakubwa sawasawa; msiogope uso wa mtu yeyote; kwa kuwa hukumu ni ya Mungu; na lile neno liwashindalo mniletee mimi, nami nitalisikiza.[#1 Sam 16:7; Mit 24:23; Yak 2:1; Mit 28:21; 29:4,25; 2 Nya 19:6; Kut 18:22,26]

18Nikawaamuru wakati huo mambo yote yaliyowapasa ninyi kuyafanya.

Waisraeli wakataa kuingia katika nchi

19Tukasafiri kutoka Horebu, tukapita katikati ya jangwa lile kubwa la kutisha mliloliona, njia ile ya kuiendea nchi ya vilima vya Waamori, kama BWANA, Mungu wetu, alivyotuamuru, tukafika Kadesh-barnea.[#Hes 10:12; Kum 8:15; Yer 2:6; Hes 13:26]

20Nami nikawaambia, Mmefika nchi ya vilima ya Waamori, anayotupa sisi BWANA, Mungu wetu.

21Tazama, BWANA, Mungu wako, ameiweka nchi mbele yako; haya panda, itamalaki, kama BWANA, Mungu wa baba zako, alivyokuambia; usiogope wala usifadhaike.[#Hes 13:30; 14:8,9; Yos 1:9; Zab 27:1-3; 46:1,7,11; Isa 41:10; 43:1,2; Lk 12:32; Ebr 13:6]

22Nanyi mkanikaribia kila mmoja wenu, mkasema, Na tutume watu mbele yetu, ili watupelelezee nchi na kutuletea habari za njia itupasayo kuipandia, na za miji tutakayoifikia.

23Neno hili likanipendeza sana; nikatwaa watu kumi na wawili, mtu mmoja kutoka kila kabila.[#Hes 13:3]

24Nao wakageuka, wakapanda mlimani wakafika katika bonde la Eshkoli, wakalipeleleza.

25Wakachuma baadhi ya matunda ya nchi ile mikononi mwao, wakatuletea huku chini, wakatuletea habari tena, wakasema, Nchi hii anayotupa BWANA, Mungu wetu, ni nchi njema.

26Lakini hamkukubali kukwea huko, mliasi neno la BWANA, Mungu wenu;[#Kum 9:23; Ebr 3:16; Hes 14:1-4; Zab 106:24]

27mkanung'unika hemani mwenu, mkasema, Ni kwa sababu BWANA ametuchukia, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili kutuangamiza.[#Kum 9:28]

28Twakwea kwenda wapi? Ndugu zetu wameiyeyusha mioyo yetu, wakituambia, Wale watu ni wengi, ni warefu kuliko sisi; miji nayo ni mikubwa, imejengewa kuta hata mbinguni; na zaidi ya hayo huko tumewaona Waanaki.[#Hes 13:28-33; Kum 9:1,2]

29Ndipo nikawaambia msiwaogope.

30BWANA, Mungu wenu, anayetangulia mbele yenu, ndiye atakayewapigania, kwa mfano wa yote aliyowafanyia huko Misri mbele ya macho yenu;[#Kut 14:14; Neh 4:20]

31na huko jangwani, ulipoona alivyokuchukua BWANA, Mungu wako, kama mtu amchukuavyo mwanawe, njia yote mliyoiendea, hata mkafika mahali hapa.[#Mdo 13:18; Kut 19:4; Kum 32:11; Isa 46:3,4; 63:9; Hos 11:3]

32Lakini katika jambo hili hamkumwamini BWANA, Mungu wenu,[#Ebr 3:19; Zab 106:24; Yud 1:5]

33aliyewatangulia njiani, usiku kwa moto, kuwaonesha njia mtakayoiendea, na mchana kwa hilo wingu, ili apate kuwatafutia mahali pa kusimamisha hema zenu.[#Kut 13:21; Zab 78:14; Hes 10:33; Eze 20:6]

Adhabu kwa ajili ya uasi wa Israeli

34BWANA akaisikia sauti ya maneno yenu, akaghadhibika, akaapa, akasema,[#Ebr 3:18; Kum 2:14]

35Hakika yangu hapana mmoja miongoni mwa watu hawa wa kizazi hiki kibaya atakayeiona nchi hiyo nzuri, niliyowaapia baba zenu kuwapa,[#Hes 14:22; Zab 95:11]

36isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, huyo ataiona; nami nitampa yeye na watoto wake nchi hiyo aliyoikanyaga; kwa kuwa amemfuata BWANA kwa kila neno.

37Na BWANA alinikasirikia mimi kwa ajili yenu, akasema, Wala wewe hutaingia humo;[#Hes 27:14; Kum 3:26; 4:21; 34:4; Zab 106:32]

38Yoshua mwana wa Nuni asimamaye mbele yako ndiye atakayeingia; mtie moyo; kwa kuwa yeye atawarithisha Israeli.[#Kut 24:13; 33:11; 1 Sam 16:22; Kum 31:7,23]

39Tena, wadogo wenu, mliosema watakuwa mateka, na wana wenu, wasiokuwa leo na maarifa ya mabaya wala mema, ndio watakaoingia, nao ndio nitakaowapa, nao wataimiliki.[#Isa 7:15,16; Eze 18:20]

40Na ninyi basi geukeni, mshike safari yenu, mwende jangwani kwa njia ya Bahari ya Shamu.

41Ndipo mkanijibu, mkaniambia, Sisi tumefanya dhambi juu ya BWANA, tutakwea kupigana kwa mfano wa yote tuliyoamriwa na BWANA. Mkajihami kila mtu na silaha zake za vita, mkafanya wepesi kukwea mlimani.

42BWANA akaniambia, Waambie, Msiende, wala msipigane; kwani mimi siko kati yenu; msije mkapigwa mbele ya adui zenu.

43Hata ingawa niliwaambia, hamkunisikiliza, bali mliasi amri ya Bwana, mkajiamini na kulewa mlimani.[#Hes 14:44,45]

44Na Waamori waliokuwa wakikaa katika mlima huo, waliwatokea juu yenu, wakawafukuza, kama wafukuzwao na nyuki, wakawapigia Seiri mpaka Horma.[#Kum 28:25; 32:30; Zab 118:12; Isa 7:18]

45Mkarudi mkalia mbele za BWANA; BWANA asiisikize sauti yenu, wala hakuelekeza masikio yake kwenu.[#Ayu 27:9; Zab 66:18; Mit 1:24; Isa 1:15; Yer 11:7-14; Zek 7:11; Yn 9:31]

Maisha ya jangwani

46Ndipo mkakaa Kadeshi siku nyingi, kwa kadiri ya hizo siku mlizokaa.[#Hes 13:25; 20:1,22; Amu 11:17]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania