The chat will start when you send the first message.
1Wakati ule BWANA akaniambia, Chonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza, kisha uje kwangu huku mlimani, ukajifanyie na sanduku la mti.[#Kut 34:1,2; 25:10]
2Nami nitaandika juu ya hizo mbao maneno hayo yaliyokuwa juu ya mbao za kwanza, ulizozivunja, nawe uzitie ndani ya hilo sanduku.
3Basi nikafanya sanduku la mti wa mshita, nikachonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza, nikakwea mle mlimani, na zile mbao mbili mkononi mwangu.[#Kut 25:5; 37:1]
4Naye akaandika juu ya mbao mfano wa maandiko ya kwanza, zile amri kumi, alizowaambia BWANA huko mlimani kutoka kati ya moto siku ya mkutano; BWANA akanipa.[#Kut 34:28; Yer 31:33; Kut 20:1; 19:17; Kum 9:10; 18:16; #10:4 au maneno kumi.]
5Basi nikageuka nikashuka kutoka mlimani, nikazitia mbao ndani ya sanduku nililofanya; nazo zimo humo kama alivyoniamuru BWANA.[#Kut 34:29; 40:20; 1 Fal 8:9]
6(Wana wa Israeli wakasafiri kutoka visima vya Bene-yaakani kwenda Mosera; Haruni akafa huko, akazikwa huko; na Eleazari mwanawe akahudumu kama kuhani badala yake.[#Hes 20:28; 33:31,38]
7Wakasafiri kutoka huko kwenda Gudgoda; wakatoka Gudgoda wakaenda Yotbatha, nayo ni nchi ya vijito vya maji.
8Na wakati huo BWANA alilitenga kabila la Lawi ili walichukue lile sanduku la Agano la BWANA, wasimame mbele za BWANA kwa kumtumikia, na kuwabarikia watu kwa jina lake, hata hivi leo.[#Hes 3:5-8; Law 9:22; Hes 6:23; Kum 21:5]
9Ndipo asiwe na fungu Lawi, wala urithi pamoja na nduguze; BWANA ndiye urithi wake, kwa mfano wa vile alivyomwambia BWANA, Mungu wako.)[#Hes 18:20,24; Kum 18:1,2; Eze 44:28]
10Nikakaa mle mlimani kama hapo kwanza, siku arobaini usiku na mchana; BWANA akanisikiliza wakati huo nao; BWANA asitake kukuangamiza.[#Kut 34:28]
11BWANA akaniambia, Ondoka, uendelee na safari yako ukiwaongoza watu; nao wataingia waimiliki nchi, niliyowaapia baba zao ya kuwa nitawapa.
12Na sasa, Israeli, BWANA, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche BWANA, Mungu wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote;[#Mik 6:8; Yer 7:23; Mt 22:37; 1 Tim 1:5]
13kuzifuata amri za BWANA na sheria zake, ninazokuamuru leo, upate uheri?
14Tazama, mbingu ni mali ya BWANA, Mungu wako, na mbingu za mbingu, na nchi, na vitu vyote vilivyomo.[#1 Fal 8:27; Zab 115:16; Mwa 14:19; Zab 24:1]
15Tena, BWANA aliwafurahia baba zako, na kuwapenda, akawachagua wazao wao baada yao, naam, na ninyi zaidi ya mataifa yote kama hivi leo.
16Basi, zitahirini govi za mioyo yenu, wala msiwe na shingo ngumu.[#Law 26:41; Yer 4:4; Rum 2:28; Efe 4:21; Kol 2:11]
17Kwa maana BWANA, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea watu, wala kukubali rushwa.[#1 Tim 6:15; Ufu 17:14; 19:16; Mdo 10:34; Rum 2:11; Zab 136:2; Dan 2:47; 2 Nya 19:7; Ayu 34:19; Gal 2:6; Efe 6:9; Kol 3:25; 1 Pet 1:17]
18Huwafanyia yatima na mjane hukumu ya haki, naye humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi.[#Zab 68:5; 146:9]
19Basi, mpendeni mgeni, kwa sababu ninyi wenyewe mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.
20Mche BWANA, Mungu wako, umtumikie yeye; ambatana naye, na kuapa kwa jina lake.[#Mt 4:10; Zab 63:11]
21Yeye ndiye fahari yako, na yeye ndiye Mungu wako, aliyekutendea mambo haya makubwa, ya kutisha, uliyoyaona kwa macho yako.[#Zab 22:3; Yer 17:14]
22Baba zako walienda Misri wakiwa watu sabini; na sasa BWANA, Mungu wako, amekufanya kama nyota za mbinguni kwa wingi.[#Mwa 15:5; 22:17; 46:27]