The chat will start when you send the first message.
1Hizi ndizo amri na hukumu mtakazozifuata kuzifanya katika nchi aliyokupa BWANA, Mungu wa baba zako, uimiliki, siku zote mtakazoishi juu ya nchi.[#Kum 4:10; 1 Fal 8:40; Gal 6:9]
2Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi;[#Kut 34:33; 2 Fal 16:4; 17:10,11; Yer 3:6]
3nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo.[#Kum 7:5; Hes 33:52; Amu 2:2; Kut 23:13; Zab 16:4; Zek 13:2]
4Wala msimfanyie hivyo BWANA, Mungu wenu.
5Lakini mahali atakapochagua BWANA, Mungu wenu, katika makabila yenu yote, apaweke jina lake, maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe uende huko;[#Kum 26:2; Yos 9:27; 1 Fal 8:29; 2 Nya 7:12; Zab 78:68]
6pelekeni huko sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng'ombe na ya kondoo;[#Law 17:3; Kum 14:22]
7na huko mtakula mbele za BWANA, Mungu wenu, nanyi furahini katika yote mtakayotia mikono yenu, ninyi na wa nyumbani mwenu, aliyokubarikia BWANA, Mungu wako.[#Kum 14:26; Law 23:40; Mhu 3:12; 5:18]
8Msifanye kwa kufuata mambo yote tuyafanyayo hapa leo, kila mtu kama apendavyo;
9kwani hamjafikia bado katika raha na urithi akupao BWANA, Mungu wako.
10Lakini mtakapovuka Yordani na kukaa katika nchi anayowarithisha BWANA, Mungu wenu, akawapeni raha, akiwaokoa na adui zenu pande zote, mkakaa salama;
11wakati huo itakuwa kwamba mahali pale atakapopachagua BWANA, Mungu wenu, alikalishe jina lake, hapo ndipo mtakapoleta kila kitu ninachowaamuru; sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu zote teule mtakazoweka kwa BWANA.[#Kum 14:23; 15:20; 16:2; Yos 18:1; 1 Fal 8:29; Zab 78:68; 87:2]
12Nanyi mtafurahi mbele za BWANA, Mungu wenu, ninyi, na wana wenu, na binti zenu, na watumishi wenu wa kiume na wa kike, na Mlawi aliyemo malangoni mwenu; kwa kuwa hana sehemu wala urithi kwenu.[#Kum 10:9; 14:29]
13Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo;[#Law 17:4]
14bali katika mahali atakapopachagua BWANA katika kabila zako mojawapo, ndipo utakapotoa sadaka zako za kuteketezwa, ndipo utakapotenda yote ninayokuamuru.
15Pamoja na haya, waweza kuchinja nyama na kula ndani ya malango yako yote, kwa kufuata yote yanayotamaniwa na roho yako, kulingana na baraka ya BWANA, Mungu wako, aliyokupa; aliye tohara na asiye tohara ana ruhusa kula katika nyama hiyo, kama ya paa na ya kulungu.[#Mwa 9:3; Kum 14:5; 15:22]
16Lakini msiile damu; imwageni juu ya nchi kama maji.[#Mwa 9:4; Law 7:26-27; 17:10-14; 19:26; Kum 15:23; 1 Sam 14:33,34; Mdo 15:20,29]
17Usile ndani ya makazi yako zaka ya nafaka zako, wala ya divai yako, wala ya mafuta yako, wala wazaliwa wa kwanza wa makundi yako, ya ng'ombe wala ya kondoo, wala nadhiri zako uwekazo zozote, wala sadaka zako za hiari, wala sadaka ya kuinuliwa ya mkono wako;
18lakini hivyo mtakula mbele za BWANA, Mungu wako, mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, wewe, na mwanao wa kiume na wa kike, na mtumwa wako wa kiume na wa kike, na Mlawi aliye ndani ya malango yako; nawe furahi mbele za BWANA, Mungu wako, katika yote utakayotia mkono wako.[#Kum 14:23; Mhu 3:12,13; 5:18-20]
19Jilinde nafsi yako usimpuuze Mlawi siku zote utakazoishi katika nchi yako.[#Kum 14:27]
20BWANA, Mungu wako, atakapoongeza mpaka wako, kama alivyokuahidi, nawe utakaposema, Nataka kula nyama, kwa kuwa roho yako yatamani kula nyama; waweza kula nyama, kwa kufuata yote inayotamani roho yako.[#Mwa 15:18; 28:14; Kut 34:24; Kum 11:24; 19:8]
21Na mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apaweke jina lake, pakiwa mbali nawe mno, ndipo utakapochinja katika kundi lako la ng'ombe na kondoo alilokupa BWANA kama nilivyokuagiza, nawe utakula ndani ya malango yako, kwa kufuata yote inayotamani roho yako.
22Kama vile anavyoliwa paa na kulungu, ndivyo utakavyoila nyama hii; asiyekuwa tohara na aliye tohara wataila pia.
23Ila ujihadhari kwamba usile damu, kwani ile damu ndiyo uhai; na uhai usile pamoja na nyama.[#Law 17:10-14; Mwa 9:4]
24Usiile; imwage juu ya nchi kama maji.
25Usiile; ili upate kufanikiwa, na watoto wako baada yako utakapofanya yaliyoelekea machoni pa BWANA.[#Kum 4:40; Isa 3:10; Kut 15:26; Kum 13:18; 1 Fal 11:38]
26Ila vitu vyako vitakatifu ulivyo navyo, na nadhiri zako, uvitwae uende mahali atakapochagua BWANA;[#Hes 5:9,10; 18:19; 1 Nya 21:22,24]
27nawe zisongeze sadaka zako za kuteketezwa, nyama na damu, juu ya madhabahu ya BWANA, Mungu wako; na damu ya dhabihu zako uimwage juu ya madhabahu ya BWANA, Mungu wako, nawe utakula nyama yake.[#Law 1:5-13; 17:11]
28Maneno haya ninayokuagiza yote yatunze na kuyasikiza, ili upate kufanikiwa na watoto wako baada yako milele, hapo unapoyafanya yaliyo mema na kuelekea machoni pa BWANA, Mungu wako.[#Zab 25:12,13; Mit 1:33; 3:1-4; Mhu 8:12]
29BWANA, Mungu wako, atakapoyaondolea mbali hayo mataifa mbele yako, huko uingiako kuyamiliki, nawe ukawatwaa, na kuishi katika nchi yao;[#Kut 23:23; Yos 23:4; Zab 78:55]
30ujiangalie, usije ukanaswa ukawafuata, wakiisha kuangamizwa mbele yako; wala usije ukauliza habari za miungu yao, ukisema, Mataifa haya waitumikiaje miungu yao? Nami nifanye hivyo.
31Usimtende kama haya BWANA, Mungu wako; kwani kila yaliyo machukizo kwa BWANA, ayachukiayo yeye, wameifanyia miungu yao; kwa maana hata wana wao na binti zao huiteketezea hiyo miungu yao ndani ya moto.[#Law 18:3,26-30; 2 Fal 17:15; 2 Nya 33:2; 36:14; Yer 32:35]
32Neno lolote ninalowaagiza lizingatieni, usilizidishe, wala usilipunguze.[#Kum 4:2; Ufu 22:18-19; Yos 1:7; Mit 30:6]