Kumbukumbu la Torati 15

Kumbukumbu la Torati 15

Amri kuhusu mwaka wa Sabato

1Kila miaka saba, mwisho wake, fanya maachilio.[#Kut 23:10; Yer 34:14]

2Na jinsi ya maachilio ni hii, kila mkopeshaji na akiache alichomkopesha mwenziwe, wala asimlipize mwenziwe wala nduguye; kwa kuwa imepigwa mbiu ya maachilio ya BWANA.

3Waweza kumtoza mgeni; lakini kila uwiacho kwa nduguyo mkono wako utamwachilia.[#Kum 23:20]

4Lakini hawatakuwako maskini kwenu; (kwa kuwa BWANA atakubarikia kweli katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, uimiliki, iwe urithi wako;)[#Kum 28:8]

5kwamba utaisikiliza tu kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, uyatunze maagizo haya yote nikuagizayo leo, kuyafanya.

6Kwani BWANA, Mungu wako, atakubarikia, kama alivyokuahidi; nawe utakopesha mataifa mengi, lakini hutakopa; tena utayatawala mataifa mengi, usitawaliwe na wao.[#Mit 22:7]

7Kama akiwapo mtu maskini pamoja nawe, nduguzo mmojawapo, ndani ya malango yako mojawapo, katika nchi yako akupayo BWANA, Mungu wako, usifanye moyo wako kuwa mgumu, wala usimfumbie mkono wako nduguyo maskini;[#Law 25:35; Mt 18:30; 1 Yoh 3:17]

8lakini mfumbulie mkono wako kwa kweli, umkopeshe kwa kweli yatoshayo haja ya mahitaji yake.[#Law 25:35; Mt 5:42; Lk 6:34; Gal 2:10]

9Jitunze, msiwe na neno lisilofaa moyoni mwako, kusema, Umekaribia mwaka wa saba, mwaka wa maachilio; jicho lako likawa ovu juu ya nduguyo usimpe kitu; naye akamlilia BWANA juu yako, ikawa ni dhambi kwako.[#Kum 28:54; Mit 23:6; 28:22; Mt 20:15; Kum 24:15; Ayu 34:28; Zab 12:5; 140:12; Amo 5:11; Yak 5:4; Mt 25:41]

10Mpe kwa kweli, wala moyo wako usisikitike utakapompa; kwa kuwa atakubarikia BWANA, Mungu wako, kwa neno hili katika kazi yako yote, na katika kila utakalotia mkono wako.[#Mt 25:40; Mdo 20:35; Rum 12:8; 2 Kor 9:5; 1 Tim 6:18; 1 Pet 4:11; Kum 14:29; Zab 41:1; Mit 22:9; 29:7]

11Kwa maana maskini hawatakoma katika nchi milele; ndipo ninakuamuru na kukuambia, Mfumbulie kwa kweli mkono wako nduguyo, mhitaji wako, maskini wako, katika nchi yako.[#Mt 26:11; Mk 14:7; Yn 12:8]

Jinsi ya Kuwatendea watumwa

12Ikiwa nduguyo, mwanaume wa Kiebrania, au mwanamke wa Kiebrania, akiuzwa kwako, naye amekutumikia miaka sita; basi mwaka wa saba mwache huru aondoke kwako.[#Law 25:39-46; Kut 21:2; Yer 34:14]

13Nawe utakapomwacha huru aondoke kwako, usimwache aende zake mikono mitupu;

14umwangalie kwa wema katika kundi lako, na sakafu yako ya nafaka, na kinu chako cha divai; mpe kama alivyokubarikia BWANA, Mungu wako.[#Mit 10:22]

15Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, akakukomboa BWANA, Mungu wako; kwa hiyo mimi nakuamuru neno hili hivi leo.

16Hata itakuwa, akikuambia, Siondoki kwako; kwa sababu akupenda wewe na nyumba yako, kwa kuwa yu hali njema kwako;[#Kut 21:5,6]

17ndipo utwae uma, uupenyeze katika sikio lake uingie katika ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako milele. Na kijakazi wako naye mfanye vivyo hivyo.

18Wala usione ugumu, utakapomwacha huru kuondoka kwako; kwani amekutumikia miaka sita kwa ujira mara mbili wa mwajiriwa; na BWANA, Mungu wako, atakubarikia kwa yote utakayofanya.[#Isa 16:14; 21:16]

Wazaliwa wa kwanza wa wanyama wafugwao

19Wazaliwa wa kwanza wa kiume wote wazaliwao katika kundi lako la ng'ombe na la kondoo, uwatakase kwa BWANA, Mungu wako; usifanye kazi kwa mzaliwa wa kwanza wa ng'ombe wako, wala usimkate manyoya mzaliwa wa kwanza wa kundi lako la kondoo.[#Kut 13:2]

20Utamla mbele za BWANA, Mungu wako, mwaka hata mwaka mahali atakapochagua BWANA, wewe na nyumba yako.[#Kum 12:5; 14:23; 16:11]

21Lakini akiwa na kilema, akichechemea, au akiwa kipofu, au mwenye kilema kibaya chochote, usimsongezee BWANA, Mungu wako, sadaka.[#Law 22:20; Kum 17:1]

22Utamla ndani ya malango yako; wasio tohara na wenye tohara pia watakula, kama unavyokula paa na kulungu.[#Kum 12:15,22]

23Pamoja na haya usile damu yake; uimwage chini kama maji.[#Mwa 9:4; Law 7:26-27; 17:10-14; 19:26; Kum 12:16,23]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania