The chat will start when you send the first message.
1BWANA, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali hayo mataifa yenye nchi akupayo BWANA, Mungu wako, nawe ukawafuata, na kukaa katika miji yao, na katika nyumba zao;[#Yos 20:1-9]
2itenge miji mitatu iwe kwako katikati ya nchi yako, akupayo BWANA, Mungu wako, kuimiliki.[#Yos 20:2]
3Itengeneze njia, igawanye na mipaka ya nchi yako, akurithishayo BWANA, Mungu wako, iwe mafungu matatu, ili kwamba kila mwenye kuua mtu apate kukimbilia huko.
4Na hii ndiyo hukumu ya mwenye kuua mtu, atakayekimbilia huko awe hai; atakayemwua mwenziwe pasipo kukusudia, wala hakumchukia tangu hapo mwanzo;
5kama aingiapo mtu na mwenziwe mwituni kwenda kukata kuni, akapeleka mkono wake na shoka ili kukata mti, likatoka shoka katika mpini, likampiga yule mwenziwe hata akafa; basi na akimbilie katika miji hii mmojawapo awe hai;
6asije akaandamwa mwuaji na mwenye kulipiza kisasi cha damu, moyo wake ukali na hasira, akampata kwa njia kuwa ndefu, akamwua; wala hana haki ya kuuawa, kwa kuwa hakumchukia tangu hapo.
7Kwa sababu hii ninakuamuru, na kukuambia, Ujitengee miji mitatu.
8Na kama BWANA, Mungu wako, akiueneza mpaka wako kama alivyowaapia baba zako, akakupa na nchi yote aliyoahidi kwamba atawapa baba zako;[#Mwa 15:18]
9nawe ukiyashika maagizo haya yote nikuagizayo leo, na kuyafanya, kumpenda BWANA, Mungu wako, na kwenda siku zote katika njia zake, ndipo ujiongezee miji mitatu tena, pamoja na mitatu ile;[#Yos 20:7]
10isije ikamwagika damu ya asiye makosa kati ya nchi yako akupayo BWANA, Mungu wako, iwe urithi, ikawa na damu juu yako.
11Lakini mtu awaye yote akimchukia mwenziwe na kumwotea na kumwinukia, akampiga hata akafa; naye akakimbilia miji hii mmojawapo;[#Kut 21:12; Hes 35:16; Mit 28:17; 29:10; 1 Yoh 3:15]
12ndipo wazee wa mji wake wapeleke ujumbe kumtwaa huko, na kumwua katika mkono wa mwenye kulipiza kisasi cha damu, apate kufa.
13Jicho lako lisimhurumie, lakini uondoe damu ya asiye makosa katika Israeli, ili upate kufanikiwa.[#1 Fal 2:31]
14Usiiondoe alama ya mpaka wa jirani yako, waliouweka watu wa kale katika urithi wako, utakaorithi ndani ya nchi akupayo BWANA, Mungu wako, uimiliki.[#Kum 27:17; Ayu 24:2; Mit 22:28; Hos 5:10]
15Shahidi mmoja asimwinukie mtu awaye yote kumshuhudia kwa uovu wowote, wala kwa dhambi yoyote, katika makosa akosayo yoyote; jambo na lithibitishwe kwa vinywa vya mashahidi wawili, au watatu.[#Hes 35:30; Kum 17:6; Mt 18:16; Yn 8:17; 19:31; 2 Kor 13:1; 1 Tim 5:19; Ebr 10:28]
16Shahidi mdhalimu akimwinukia mtu yeyote na kushuhudia juu yake ya upotovu;[#Zab 27:12; 1 Fal 21:13]
17ndipo wale watu washindanao kwa mambo yale na wasimame wote wawili mbele za BWANA, mbele ya makuhani na waamuzi watakaokuwapo siku hizo;
18nao waamuzi na watafute kwa bidii; na tazama, yule shahidi akiwa shahidi wa uongo, naye ametoa ushahidi wa uongo juu ya nduguye;
19ndipo mtamfanyia kama alivyodhani kumfanyia nduguye; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.[#Mit 19:5; Dan 6:24]
20Na watakaosalia watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako.[#Kum 17:13; 21:21]
21Wala jicho lako lisiwe na huruma; uzima kwa uzima, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu.[#Kut 21:23-25; Law 24:19-20; Mt 5:38]