Kumbukumbu la Torati 32

Kumbukumbu la Torati 32

1Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitanena;[#Zab 50:4; Isa 1:2; Yer 2:12; 6:19]

Na nchi isikie maneno ya kinywa changu.

2Mafundisho yangu yatadondoka kama mvua,[#2 Sam 23:4; Ayu 29:22,23; Isa 55:10; Hos 6:4; 14:5; 1 Kor 3:6,8; Ebr 6:7; Zab 72:6]

Maneno yangu yatatona-tona kama umande;

Kama manyunyu juu ya majani mabichi;

Kama matone ya mvua juu ya mimea.

3Maana nitalitangaza Jina la BWANA;

Mpeni ukuu Mungu wetu.

4Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu;[#2 Sam 22:31; Dan 4:37; Yer 10:10; Ayu 34:10]

Maana, njia zake zote ni haki.

Mungu wa uaminifu, asiye na uovu,

Yeye ndiye mwenye haki na adili.

5Wametenda mambo ya uharibifu,

Hawawi watoto wake, hii ndiyo ila yao;

Wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka.

6Je! Mnamlipa BWANA hivi,[#Zab 116:12; Isa 63:16; 2 Sam 7:23; Zab 74:2]

Enyi watu wapumbavu na ujinga?

Je! Yeye siye baba yako aliyekununua?

Amekufanya, na kukuweka imara.

7Kumbuka siku za kale,

Tafakari miaka ya vizazi vingi;

Mwulize baba yako, naye atakuonesha;

Wazee wako, nao watakuambia.

8Yeye Aliye Juu alipowapa mataifa urithi wao,[#Mdo 17:26; Zek 9:2; Mwa 11:8]

Alipowabagua wanadamu,

Aliweka mipaka ya watu

Kwa kadiri ya hesabu ya wana wa Israeli.

9Maana, sehemu ya BWANA ni watu wake,[#1 Sam 10:1]

Yakobo ni kura ya urithi wake.

10Alimkuta katika nchi ya ukame,[#Kum 4:36; Neh 9:20; Zab 32:7,10; 147:19,20; Rum 2:18; 3:2; Zab 17:8; Mit 7:2]

Na katika jangwa tupu litishalo;

Alimzunguka, akamtunza;

Akamhifadhi kama mboni ya jicho;

11Mfano wa tai ataharikishaye kiota chake;

Na kupapatika juu ya makinda yake,

Alikunjua mbawa zake, akawatwaa,

Akawachukua juu ya mbawa zake;

12BWANA peke yake alimwongoza,

Wala hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye.

13Alimpandisha mahali pa nchi palipoinuka,[#Isa 58:14; Ayu 29:6]

Naye akala mazao ya mashamba;

Akamnyonesha asali iliyotoka jabalini,

Na mafuta yaliyotoka katika mwamba wa gumegume;

14Siagi ya ng'ombe, na maziwa ya kondoo,[#Zab 147:14; Mwa 49:11; Mt 26:28,29; Yn 6:55,56]

Pamoja na mafuta ya wana-kondoo,

Kondoo dume wa Kibashani, na mbuzi,

Na unono wa ngano iliyo nzuri;

Ukanywa divai, damu ya mizabibu.

15Lakini Yeshuruni alinenepa, akapiga teke;[#Isa 1:4; Zab 89:26]

Umenenepa, umekuwa mnene, umewanda;

Ndipo akamwacha Mungu aliyemfanya,

Akamdharau Mwamba wa wokovu wake.

16Wakamtia wivu kwa miungu migeni,

Wakamkasirisha kwa machukizo.

17Walitoa sadaka kwa pepo, si Mungu,[#1 Kor 10:20]

Kwa miungu wasiyoijua,

Kwa miungu mipya iliyotokea siku zilizo karibu,

Ambayo baba zenu hawakuiogopa.

18Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa,

Mungu aliyekuzaa umemsahau.

19BWANA akaona, akawachukia,

Kwa sababu ya kukasirishwa na wanawe na binti zake.

20Akasema, Nitawaficha uso wangu,[#Mt 17:17]

Nitaona mwisho wao utakuwaje;

Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi,

Watoto wasio na imani ndani yao.

21Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu;[#1 Kor 10:22; Rum 10:19; 1 Sam 12:21]

Wamenikasirisha kwa ubatili wao;

Nami nitawatia wivu kwa wasio watu,

Nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo.

22Maana, moto umewashwa kwa hasira yangu,[#Omb 4:11]

Unateketea hata chini ya kuzimu,

Unakula dunia pamoja na mazao yake,

Unaunguza misingi ya milima.

23Nitaweka madhara juu yao chungu chungu;

Nitawapiga kwa mishale yangu hata ikaishe;

24Watakonda kwa njaa, wataliwa na makaa ya moto,

Na uharibifu mkali;

Nitawapelekea meno ya wanyama wakali,

Pamoja na sumu ya wadudu watambaao mavumbini.

25Nje upanga utawafisha[#Omb 1:20]

Na ndani ya vyumba, utisho;

Utaangamiza mvulana na msichana,

Anyonyaye pamoja na mwenye mvi,

26Nilisema, Ningewatawanyia mbali,

Ningekomesha kumbukumbu lao kati ya wanadamu;

27Isipokuwa niliogopa makamio ya adui,[#Zab 140:8]

Adui zao wasije wakafikiri uongo,

Wasije wakasema, Mkono wetu umetukuka,

Wala BWANA hakuyafanya haya yote.

28Maana hawa ni taifa wasio shauri,

Wala fahamu hamna ndani yao.

29Laiti wangekuwa na akili, hata wakafahamu haya,[#Zab 81:13]

Ili watafakari mwisho wao.

30Mmoja angefukuzaje watu elfu,[#Yos 23:10; Zab 44:12]

Wawili wangekimbizaje elfu kumi,

Kama Mwamba wao asingaliwauza,

Kama BWANA asingaliwatoa?

31Maana, Mwamba wao si kama Mwamba wetu,[#1 Sam 4:8; Yer 40:3]

Hata adui zetu wenyewe ndivyo wahukumuvyo.

32Maana, mzabibu wao ni mzabibu wa Sodoma,

Nao ni wa mashamba ya Gomora;

Zabibu zao ni zabibu za uchungu,

Vichala vyao ni vichungu.

33Mvinyo yao ni sumu ya majoka,

Uchungu mkali wa nyoka.

34Je! Haya hayakuwekwa akiba kwangu?[#Ayu 14:17]

Na kutiwa mhuri kati ya hazina yangu?

35Kisasi ni changu mimi, na kulipa,[#Rum 12:19; 13:4; Ebr 10:30; Zab 94:1]

Wakati itakapoteleza miguu yao;

Maana siku ya msiba wao imekaribia,

Na mambo yatakayowapata yatafanya haraka.

36Kwa kuwa BWANA atawaamua watu wake,[#Zab 135:14; Amu 2:18; Zab 90:13; 105:45; Yer 31:20; Yoe 2:14]

Atawahurumia watumwa wake,

Aonapo ya kuwa nguvu zao zimeondoka,

Na ya kuwa habaki mtu, aliyefungwa wala asiyefungwa,

37Naye atasema, Iko wapi miungu yao,[#Amu 10:14; 2 Fal 3:13; Yer 2:28]

Mwamba ule walioutumaini;

38Uliokula shahamu za sadaka zao,

Na kunywa divai ya sadaka zao za kinywaji?

Na waondoke na kuwasaidia ninyi;

Na wawe hao himaya yenu.

39Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam, Mimi ndiye,[#Isa 41:4; 45:5; 46:4; 1 Sam 2:6; 2 Fal 5:7; Ayu 5:18; Zab 68:20; Isa 43:13; Hos 6:1]

Wala hapana Mungu mwingine ila Mimi;

Naua Mimi, nahuisha Mimi,

Nimejeruhi, tena naponya;

Wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu,

40Maana, nainua mkono wangu mbinguni,[#Kut 6:8]

Na kusema, Kama Mimi niishivyo milele,

41Nikiunoa upanga wangu wa umeme,

Mkono wangu ukishika hukumu,

Nitawatoza kisasi adui zangu,

Nitawalipa wanaonichukia.

42Nitailevya mishale yangu kwa damu,[#Ayu 13:24]

Na upanga wangu utakula nyama;

Pamoja na damu ya waliouawa na waliotekwa nyara,

Katika vichwa vya wakuu wa adui.

43Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake;[#Rum 15:10; Ufu 19:2; 6:10; Zab 85:1]

Kwa maana atatwaa kisasi kwa damu ya watumwa wake,

Atawatoza kisasi adui zake,

Tena atafanya kafara kwa nchi yake, na watu wake.

44Musa akaja akasema maneno haya yote ya wimbo huu masikioni mwa watu, yeye na Yoshua, mwana wa Nuni.

45Musa akamaliza kuwaambia Israeli wote maneno haya yote;

46akawaambia, Yawekeni mioyoni mwenu maneno yote ambayo nashuhudia kwenu hivi leo; nayo waamuruni watoto wenu, wayatunze na kuyafanya maneno yote ya torati hii.

47Kwa maana si jambo lisilofaa kwenu; maana, ni maisha yenu, na kwa jambo hili mtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi mwivukiayo Yordani kuimiliki.[#Mit 3:2; Rum 10:5]

Utabiri wa kifo cha Musa

48BWANA akasema na Musa siku hiyo hiyo, akamwambia,[#Hes 27:12-14; Kum 3:23-27]

49Kwea katika mlima huu wa Abarimu, mpaka kilima cha Nebo, kilicho katika nchi ya Moabu, kuelekea Yeriko; ukaangalie nchi ya Kanaani niwapayo wana wa Israeli kuimiliki;

50ukafe katika kilima, huko ukweako, ukusanywe uwe pamoja na jamaa zako; kama alivyokufa nduguyo Haruni katika mlima wa Hori, akakusanywa awe pamoja na watu wake;

51kwa sababu mlinikosa ninyi juu yangu katikati ya wana wa Israeli katika maji ya Meriba huko Kadeshi, katika bara ya Sini; kwa kuwa hamkunitakasa katikati ya wana wa Israeli.[#Hes 20:11]

52Kwani utaiona hiyo nchi mbele yako, lakini hutakwenda huko kuingia hiyo nchi niwapayo wana wa Israeli.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania