The chat will start when you send the first message.
1Hii ndiyo baraka ya Musa, huyo mtu wa Mungu, aliyowabarikia wana wa Israeli kabla ya kufa kwake.[#Mwa 49:28; Lk 24:50; Yn 14:27; 16:33]
2Akasema,[#Kut 19:18; Amu 5:4; Hab 3:3; Dan 7:10; Mdo 7:53; Gal 3:19; Ebr 2:2]
BWANA alitoka Sinai,
Akawajia kutoka Seiri;
Aliangaza katika kilima cha Parani,
Akaja Meribath-kadeshi.
Upande wa mkono wake wa kulia
Palikuwa na sheria ya motomoto kwao.
3Hakika ayapenda hayo makabila ya watu;[#Hos 11:1; Mal 1:2; 1 Sam 2:9; Zab 50:5; Lk 10:39; Mdo 22:3]
Watakatifu wake wote wamo mkononi mwako;
Nao waliketi miguuni pako;
Watapokea kila mmoja katika maneno yako.
4Musa alituagiza torati,[#Yn 7:19]
Ni urithi kwa mkutano wa Yakobo.
5Akawa mfalme katika Yeshuruni,[#Ayu 29:25]
Walipokutanika wakuu wa watu,
Makabila yote ya Israeli pamoja.
6Reubeni na aishi, asife;
Lakini watu wake na wawe wachache.
7Na baraka ya Yuda ni hii; akasema,[#Mwa 49:8]
Isikize, Ee BWANA, sauti ya Yuda,
Umlete ndani kwa watu wake;
Alijitetea kwa mikono yake;
Nawe utakuwa msaada juu ya adui zake.
8Akamnena Lawi,[#Kut 17:7; 28:30; Hes 20:13; 27:21; Law 8:8]
Thumimu yako na Urimu yako vina mtakatifu wako,
Uliyemjaribu huko Masa;
Ukateta naye kwenye maji ya Meriba.
9Aliyemtaja baba yake na mama yake, Mimi sikumwona;[#Kum 13:6; Mt 10:37; 12:48; Mk 10:29; Lk 14:26; Kut 32:26; Yer 18:18; Mal 2:5]
Wala nduguze hakuwakubali;
Wala hakuwajua watoto wake mwenyewe;
Maana wameliangalia neno lako,
Wamelishika agano lako.
10Watamfundisha Yakobo hukumu zako,[#Law 10:11; Kut 30:7,8; Zab 51:19]
Na Israeli torati yako,
Wataweka uvumba mbele zako,
Na sadaka nzima za kuteketezwa madhabahuni pako.
11Ee BWANA, ubariki mali zake,[#Zab 20:3]
Utakabali kazi ya mikono yake;
Uwapige viuno vyao waondokao juu yake,
Na wenye kumchukia, wasiinuke tena.
12Akamnena Benyamini,
Mpenzi wa BWANA atakaa salama kwake;
Yuamfunika mchana kutwa,
Naye hukaa kati ya mabega yake.
13Na Yusufu akamnena,[#Mwa 49:25; 27:28]
Nchi yake na ibarikiwe na BWANA;
Kwa vitu vya thamani vya mbinguni, kwa huo umande,
Na kwa kilindi kilalacho chini,
14Na kwa vitu vilivyo bora vya matunda ya jua,
Na kwa vitu vilivyo bora vya mavuno ya miezi,
15Na kwa vitu viteule vya milima ya kale,[#Hab 3:6]
Na kwa vitu vilivyo bora vya vilima vya milele,
16Na kwa vitu vilivyo bora vya nchi, na kujaa kwake,[#Kut 3:2,4; Mdo 7:30]
Na uradhi wake aliyekaa ndani ya kile kichaka;
Na ije baraka juu ya kichwa chake Yusufu,
Juu ya utosi wa kichwa chake aliyetengwa na nduguze.
17Mzaliwa wa kwanza wa ng'ombe wake dume, enzi ni yake;[#1 Fal 22:11; Zab 44:5]
Na pembe zake ni pembe za nyati;
Kwa hizo atayasukuma mataifa yote, hata ncha za nchi;
Nao ni makumi ya maelfu ya Efraimu,
Nao ni maelfu ya Manase.
18Na Zabuloni akamnena,
Furahi Zabuloni, katika kutoka kwako;
Na Isakari, katika hema zako.
19Watayaita mataifa waje mlimani;[#Isa 2:3; Yer 50:4,5; Zab 4:5]
Wakasongeze huko sadaka za haki;
Kwa kuwa watanyonya wingi wa bahari,
Na akiba zilizofichamana za mchangani.
20Na Gadi akamnena,[#Yos 13:10; 1 Nya 12:8]
Na abarikiwe amwongezaye Gadi;
Yeye hukaa kama simba jike,
Hurarua mkono, naam, na utosi wa kichwa.
21Akajichagulia sehemu ya kwanza,[#Hes 32:16,21; Yos 4:12]
Kwani ndiko lilikowekwa fungu la mtoa-sheria;
Akaja pamoja na wakuu wa watu,
Akaitekeleza haki ya BWANA,
Na hukumu zake kwa Israeli.
22Na Dani akamnena,[#Yos 19:47; Amu 18:27]
Dani ni mwanasimba,
Arukaye kutoka Bashani.
23Na Naftali akamnena,[#Yos 19:32]
Ee Naftali, uliyeshiba fadhili,
Uliyejawa na baraka ya BWANA;
Umiliki magharibi na kusini.
24Na Asheri akamnena,[#Ayu 29:6]
Na abarikiwe Asheri kwa watoto;
Na akubaliwe katika nduguze,
Na achovye mguu wake katika mafuta.
25Makomeo yako yatakuwa ya chuma na shaba;
Na kadiri ya siku zako ndivyo zitakavyokuwa nguvu zako.
26Hapana aliyefanana na Mungu, Ee Yeshuruni,[#Kut 15:11; Zab 86:8; Yer 10:6; Zab 68:4,33,34; 104:3; Hab 3:8]
Ajaye amepanda juu ya mbingu ili akusaidie.
Na juu ya mawingu katika utukufu wake.
27Mungu wa milele ndiye makazi yako,[#Zab 90:1]
Na mikono ya milele i chini yako.
Na mbele yako amemsukumia mbali adui;
Akasema, Angamiza.
28Na Israeli anakaa salama,[#Hes 23:9; Yer 23:6; 33:16]
Chemchemi ya Yakobo peke yake,
Katika nchi ya ngano na divai;
Naam, mbingu zake zadondoza umande.
29U heri, Israeli.[#Zab 144:15; 2 Sam 7:23]
Ni nani aliye kama wewe, taifa lililookolewa na BWANA!
Ndiye ngao ya msaada wako,
Na upanga wa utukufu wako;
Na adui zako watajitiisha chini yako,
Nawe utapakanyaga mahali pao pa juu.