The chat will start when you send the first message.
1Sikiliza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita, miji mikubwa iliyojengewa kuta hadi mbinguni,[#Kum 4:38; 7:1; 11:23; 1:28]
2watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki?[#Hes 13:22]
3Basi jua siku hii ya leo kuwa BWANA, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia BWANA.[#Kum 31:3; Yos 3:11; Mik 2:13; Ufu 19:11-15; Kum 4:24; Isa 30:27; 33:14; Nah 1:5,6; 2 The 1:8; Ebr 12:29; Kut 23:31; Kum 7:24]
4Usiseme moyoni mwako, BWANA, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia BWANA niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya BWANA anawafukuza nje mbele yako.[#Kum 8:11,17; Eze 36:32; Rum 11:6; 1 Kor 4:4; Mwa 15:16; Law 18:24; Kum 18:12]
5Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya BWANA, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno BWANA alilowaapia baba zako Abrahamu, na Isaka, na Yakobo.[#2 Tim 1:9; Tit 3:5; Mwa 12:7; 13:15; 15:7; Kut 32:13; Lk 1:54,55; Mdo 13:32,33; Rum 15:8]
6Basi jua ya kuwa BWANA, Mungu wako, hakupi nchi hii nzuri uimiliki kwa ajili ya haki yako, kwa maana u taifa lenye shingo ngumu.
7Kumbuka, usisahau ulivyomtia BWANA, Mungu wako, kasirani jangwani; tangu siku uliyotoka nchi ya Misri hadi mlipofika mahali hapa, mmekuwa na uasi juu ya BWANA[#Kut 14:11; 16:2; 17:2; Hes 11:4; 14:1; 20:2]
8Tena mlimkasirisha BWANA katika Horebu, BWANA akakasirika hadi akataka kuwaangamiza.[#Kut 32:4; Zab 106:19]
9Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano BWANA alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji.[#Kut 24:18; 34:28; Lk 4:1]
10BWANA akanipa vile vibao viwili vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu; na juu yake yameandikwa maneno mfano wa yote aliyosema nanyi BWANA mle mlimani kutoka kati ya moto siku ya mkutano.
11Ikawa mwisho wa siku arobaini usiku na mchana, BWANA alinipa zile mbao mbili za mawe, nazo ni mbao za agano.
12BWANA akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu.[#Kut 32:7; Kum 31:29; Amu 2:17]
13Tena BWANA akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu;[#Kut 32:9; Kum 10:16; 31:27; 2 Fal 17:14]
14niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuliko wao.[#Kum 29:20; Zab 9:5; 109:13]
15Basi nikageuka nikashuka mle mlimani, mlima ukawaka moto; na vile zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu miwili.
16Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wenu; mmefanya ndama ya ng'ombe ya kusubu; mmepotoka punde katika njia aliyowaamuru BWANA.
17Nikazishika zile mbao mbili, nikazitupa kutoka katika mikono yangu miwili, nikazivunja mbele ya macho yenu.[#Zab 69:9; 119:139]
18Nikaanguka chini mbele za BWANA siku arobaini usiku na mchana, kama pale kwanza; sikula chakula wala kunywa maji; kwa sababu ya makosa yenu yote mliyofanya, kwa kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, kwa kumkasirisha.[#Kut 34:28; Zab 106:23]
19Kwa kuwa niliogopa hasira na makamio aliyowakasirikia BWANA kutaka kuwaangamiza. Lakini BWANA alinisikiza wakati huo nao.[#Ebr 12:21,29; Kut 32:10,11,14; 33:17; Kum 10:10; Zab 106:23; Yak 5:15; Amo 7:1-6]
20BWANA akamkasirikia sana Haruni akataka kumwangamiza; nikamwombea Haruni naye wakati huo.
21Kisha nikaitwaa ile dhambi yenu, huyo ndama mliyemfanya, nikamteketeza kwa moto, nikamponda, nikamsaga tikitiki, hata akawa laini kama vumbi; nikalitupa vumbi lake katika kijito kilichoshuka kutoka mlimani.[#Kut 32:20; Isa 2:18-21; 30:22; 31:7; Hos 8:11]
22Tena huko Tabera, na Masa, na Kibroth-hataava mlimtia BWANA hasira.[#Hes 11:3,34; Kut 17:7]
23Na wakati alipowatuma BWANA kutoka Kadesh-barnea, akiwaambia, Kweeni mkaimiliki nchi niliyowapa; ndipo mkaasi juu ya maagizo ya BWANA, Mungu wenu, hamkumsadiki wala hamkusikiliza sauti yake.[#Hes 13:3,17; 14:1; Zab 78:22; 106:24; Kum 1:21,26; Ebr 3:16; 4:2]
24Mmekuwa na uasi juu ya BWANA tokea siku nilipowajua ninyi.[#Kum 31:27]
25Ndipo nikaanguka chini mbele za BWANA siku zile arobaini usiku na mchana nilizokuwa nimeanguka chini; kwa kuwa BWANA alisema atawaangamiza.
26Nikamwomba BWANA, nikasema, Ee Bwana Mungu, usiwaangamize watu wako, urithi wako, uliowakomboa kwa ukuu wako, uliowatoa Misri kwa mkono wa nguvu.[#Kut 32:11; 1 Sam 7:9; Mit 15:29; Yer 15:1]
27Wakumbuke watumishi wako, Abrahamu, na Isaka, na Yakobo; usiangalie ukaidi wa watu hawa, wala uovu wao, wala dhambi yao;
28isije nchi uliyotutoa ikasema, Ni kwa sababu BWANA hakuweza kuwaleta katika nchi aliyowahidi, tena ni kwa kuwa aliwachukia, aliwatoa nje ili kuwaua jangwani.[#Mwa 41:57; 1 Sam 14:25; Kut 32:12; Hes 14:16; Kum 32:26,27; Yos 7:7-9; Zab 115:1,2; Isa 48:9-11]
29Nao ni watu wako, urithi wako, uliowatoa kwa nguvu zako kuu na mkono wako ulionyoka.[#Kum 4:20; 1 Fal 8:51; Neh 1:10; Zab 95:7]