Waefeso 4

Waefeso 4

Umoja katika mwili wa Kristo

1Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa;[#Kol 1:10]

2kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo;[#Kol 3:12-13]

3na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.[#Kol 3:14,15]

4Kuna mwili mmoja, na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.[#Rum 12:5]

5Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.[#Yn 10:16; 1 Kor 8:6]

6Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.[#1 Kor 12:6]

7Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo.[#Rum 12:3,6; 1 Kor 12:11]

8Hivyo husema,[#Zab 68:18; Kol 2:15]

Alipopaa juu aliteka mateka,

Akawapa wanadamu vipawa.

9Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi?[#Yn 3:13]

10Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote.

11Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;[#1 Kor 12:28; Mdo 21:8]

12kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;[#1 Pet 2:5; 2 Tim 3:17]

13hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;[#Kol 1:28]

14ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.[#1 Kor 14:20; Ebr 13:9]

15Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.[#Efe 1:22; 5:23; Kol 1:18]

16Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.[#Kol 2:19]

Maisha ya zamani na mapya

17Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msiende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao;[#Rum 1:21; Kol 2:4,6]

18ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wametengwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao;[#Efe 2:12; Kol 1:21; 1 Pet 1:14]

19ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani.[#Kol 3:5]

20Bali ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Kristo;

21ikiwa kwa hakika mlisikia habari zake na kufundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika Yesu,

22mvue mwenendo wenu wa kwanza, utu wa zamani unaoharibika, kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya;[#Kol 3:9; Rum 8:13; Gal 6:8]

23na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu;[#Rum 12:2]

24na mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.[#Mwa 1:26; Kol 3:10]

Amri za maisha mapya

25Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.[#Zek 8:16; Kol 3:8]

26Muwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;[#Zab 4:4; Yak 1:19,20]

27wala msimpe Ibilisi nafasi.

28Mwizi asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akifanya kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji.[#1 The 4:11]

29Neno lolote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.[#Efe 5:4; Kol 3:16,17; 4:6]

30Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa mhuri hata siku ya ukombozi.[#Efe 1:13; Isa 63:10]

31Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matusi yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;[#Kol 3:8]

32tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.[#Kol 3:13; Mt 6:14; 18:22-35]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania