The chat will start when you send the first message.
1Neno la BWANA likanijia tena, kusema,
2Mwanadamu, uujulishe Yerusalemu machukizo yake,[#Eze 20:4]
3useme, Bwana MUNGU auambia Yerusalemu hivi; Asili yako na kuzaliwa kwako kwatoka katika nchi ya Mkanaani; Mwamori alikuwa baba yako, na mama yako alikuwa Mhiti.
4Na kuhusu habari za kuzaliwa kwako, siku ile uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuoshwa kwa maji usafishwe; hukutiwa chumvi hata kidogo, wala hukutiwa katika nguo kabisa.[#Hos 2:3]
5Hakuna jicho lililokuhurumia, ili kukutendea lolote la mambo hayo kwa kukuhurumia; lakini ulitupwa nje uwandani, kwa kuwa nafsi yako ilichukiwa, katika siku ile uliyozaliwa.
6Nami nilipopita karibu nawe, nikakuona ukigaagaa katika damu yako, nilikuambia, Ulipokuwa katika damu yako, uwe hai; naam, nilikuambia, Ulipokuwa katika damu yako, uwe hai.
7Nilikufanya kuwa maelfu, kama mimea ya mashamba, ukaongezeka, na kuzidi kuwa mkubwa, ukapata kuwa na uzuri mno; matiti yako yakaumbwa, nywele zako zikawa zimeota; lakini ulikuwa uchi, bila mavazi.
8Basi, nilipopita karibu nawe, nikakutazama; tazama, wakati wako ulikuwa wakati wa upendo; nikatandika upindo wa vazi langu juu yako, nikakufunika uchi wako; naam, nilikuapia, nikafanya agano nawe, asema Bwana MUNGU, ukawa wangu.[#Rut 3:9; Kut 19:5]
9Kisha nikakuosha kwa maji; naam, nilikuosha kabisa damu yako, na kukupaka mafuta;
10nikakuvika nguo ya taraza, nikakupa viatu vya ngozi ya pomboo, nikakufunga nguo ya kitani safi kiunoni mwako, nikakufunika kwa hariri.
11Nikakupamba kwa mapambo pia, nikatia vikuku mikononi mwako, na mkufu shingoni mwako.[#Mwa 24:22; 41:42; Wim 1:10; Isa 13:19; Mit 1:9; Dan 5:7,16,29]
12Nikatia kishaufu puani mwako, na hereni masikioni mwako, na taji zuri juu ya kichwa chako.
13Hivyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha; na mavazi yako yalikuwa ya kitani safi, na hariri, na kazi ya taraza; ulikula unga mzuri, na asali, na mafuta; nawe ulikuwa mzuri mno, ukafanikiwa hata kufikia hali ya kifalme.[#Kum 32:13; Zab 48:2]
14Sifa zako zikaenea kati ya mataifa kwa sababu ya uzuri wako; kwa maana ulikuwa mkamilifu, kwa sababu ya utukufu wangu niliokutia, asema Bwana MUNGU.[#Omb 2:15]
15Lakini uliutumainia uzuri wako, ukafanya mambo ya kikahaba kwa sababu ya sifa zako, ukamwaga mambo yako ya kikahaba juu ya kila mtu aliyepita; ulikuwa wake.[#Kum 32:15; Mik 3:11; Yer 7:4; 2:20; Isa 1:21; 57:8; Hos 1:2]
16Ukatwaa baadhi ya mavazi yako, ukajifanyia mahali palipoinuka, palipopambwa kwa rangi mbalimbali, ukafanya mambo ya kikahaba juu yake; mambo kama hayo hayatakuja wala hayatakuwako.[#2 Fal 23:7; Eze 7:20; Hos 2:8]
17Pia ulivitwaa vyombo vyako vya uzuri, vya dhahabu yangu na vya fedha yangu, nilivyokupa, ukajifanyia sanamu za wanaume, ukafanya mambo ya kikahaba pamoja nazo;
18ukatwaa nguo zako za kazi ya taraza, ukawafunika, ukaweka mafuta yangu na uvumba wangu mbele yao.
19Mkate wangu niliokupa, unga mzuri, na mafuta, na asali, nilivyokulisha, ukaviweka mbele yao viwe harufu ya kupendeza; na ndivyo vilivyokuwa; asema Bwana MUNGU.[#Kum 32:13]
20Pamoja na hayo uliwatwaa wana wako na binti zako, ulionizalia, ukawatoa sadaka kwao ili waliwe. Je! Mambo yako ya kikahaba ni kitu kidogo tu,[#2 Fal 16:3; Isa 57:5; Yer 7:31; Eze 20:26]
21hata ukawaua watoto wangu, na kuwatoa kwa kuwapitisha motoni kwa hao?[#Mwa 17:7,11; Kut 13:2]
22Na katika machukizo yako yote, na mambo yako ya kikahaba, hukuzikumbuka siku za ujana wako, ulipokuwa uchi, bila mavazi, ukawa ukigaagaa katika damu yako.[#Yer 2:2; Hos 2:3]
23Tena, imekuwa baada ya uovu wako wote, (ole wako! ole wako! Asema Bwana MUNGU,)
24ulijijengea mahali palipoinuka, ukajifanyia mahali palipoinuka katika kila njia kuu.[#Law 26:30; Zab 78:58; Isa 57:5; Yer 2:20]
25Umejenga mahali pako palipoinuka penye kichwa cha kila njia, ukaufanya uzuri wako kuwa chukizo, ukatanua miguu yako kwa kila mtu aliyepita karibu, ukaongeza mambo yako ya kikahaba.[#Mit 9:14; Yer 6:15]
26Tena umezini na Wamisri, jirani zako, wakuu wa mwili; ukaongeza mambo yako ya kikahaba, ili kunikasirisha.[#Eze 8:10; 20:7]
27Basi, tazama, kwa ajili ya hayo nimenyosha mkono wangu juu yako, nami nimelipunguza posho lako, na kukutoa kwa mapenzi yao wanaokuchukia, binti za Wafilisti, walioyaonea haya mambo yako ya uasherati.
28Pia umefanya mambo ya kikahaba pamoja na Waashuri, kwa sababu ulikuwa huwezi kushibishwa; naam, umefanya mambo ya kikahaba pamoja nao, wala hujashiba bado.[#Amu 10:6; 2 Fal 16:7; Yer 2:18,29; Eze 23:14]
29Pamoja na hayo umeongeza mambo yako ya kikahaba katika nchi ya Kanaani, mpaka Ukaldayo, wala hujashibishwa kwa hayo.
30Jinsi moyo wako ulivyokuwa dhaifu, asema Bwana MUNGU, ikiwa unafanya mambo hayo yote, kazi ya mwanamke mzinzi,[#Mit 30:20]
31apendaye kutawala watu; kwa kuwa wajijengea mahali pako pakuu penye kichwa cha kila njia, na kufanya mahali pako palipoinuka katika kila njia kuu; lakini hukuwa kama kahaba, kwa maana ulidharau kupokea ujira.
32Mke wa mtu, aziniye! Akaribishaye wageni badala ya mumewe!
33Watu huwapa makahaba wote zawadi, bali wewe unawapa wapenzi wako wote zawadi zako, na kuwapa rushwa ili waje kwako pande zote, kwa ajili ya mambo yako ya kikahaba.[#Isa 30:3]
34Tena, katika mambo yako ya kikahaba, wewe na wanawake wengine ni mbalimbali, kwa kuwa hapana akufuataye katika mambo yako ya kikahaba; tena kwa kuwa unatoa ujira, wala hupewi ujira; basi, njia yako na njia yao ni tofauti.
35Kwa sababu hiyo, Ewe kahaba, lisikie neno la BWANA;
36Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu uchafu wako umemwagwa, na uchi wako umefunuliwa, kwa njia ya uzinzi wako pamoja na wapenzi wako; na kwa sababu ya vinyago vyote vya machukizo yako; na kwa sababu ya damu ya watoto wako, uliyowapa;[#Zab 106:38; Yer 2:34]
37basi, tazama, nitawakusanya wapenzi wako wote ambao umejifurahisha pamoja nao, nao wote uliowapenda, pamoja na watu wote uliowachukia; naam, nitawakusanya juu yako pande zote, na kuwafunulia uchi wako, wapate kuuona uchi wako wote.[#Isa 47:2,3; Yer 13:22; Omb 1:8; Eze 23:9; Hos 2:10; Nah 3:5]
38Nami nitakuhukumu, kama wahukumiwavyo wake walioolewa wazinio, na kumwaga damu, nami nitakupatiliza damu ya ghadhabu na wivu.[#Mwa 9:6; Kut 21:12; Law 24:17; Mt 26:52; Ufu 13:10]
39Tena nitakutia katika mikono yao, nao watapaangusha mahali pako pakuu, na kupabomoa mahali pako palipoinuka, nao watakuvua nguo zako, na kutwaa vyombo vyako vya uzuri, nao watakuacha uchi, bila mavazi.[#Eze 23:26]
40Tena wataleta mkutano wa watu juu yako, nao watakupiga kwa mawe, na kukuchoma kwa panga zao.[#Eze 23:10; Yn 8:5]
41Nao watazichoma moto nyumba zako, na kutekeleza hukumu juu yako mbele ya wanawake wengi, nami nitakulazimisha kuacha mambo ya kikahaba, wala hutatoa ujira tena.[#Kum 13:16; 2 Fal 25:9; Yer 39:8; Rum 2:8; Eze 5:8; 23:10,27]
42Hivyo ndivyo nitakavyoshibisha ghadhabu yangu juu yako, na wivu wangu utanitoka, nami nitatulia wala sitaona hasira tena.[#Eze 5:13]
43Kwa sababu hukuzikumbuka siku za ujana wako, bali umenikasirisha kwa mambo hayo yote; basi, tazama, mimi nami nitaleta matendo yako juu ya kichwa chako, asema Bwana MUNGU; wala hutafanya uasherati zaidi ya machukizo yako yote.[#Zab 78:42; Eze 9:10; 11:21]
44Tazama, kila mtu atumiaye mithali atatumia mithali hii kinyume chako, akisema, Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake.
45Wewe u binti ya mama yako, amchukiaye mume wake na watoto wake; nawe u dada wa dada zako, waliowachukia waume zao na watoto wao; mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako Mwamori.
46Na dada yako mkubwa ni Samaria, akaaye mkono wako wa kushoto, yeye na binti zake; na dada yako mdogo, akaaye mkono wako wa kulia, ni Sodoma na binti zake.
47Lakini hukuenda katika njia zao, na hukutenda kulingana na machukizo yao; lakini kwa kitambo kidogo ulikuwa umepotoka kuliko wao katika njia zako zote.[#2 Fal 21:9; Eze 5:6,7]
48Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, Sodoma, dada yako, yeye na binti zake, hawakutenda kama wewe ulivyotenda, wewe na binti zako.[#Mt 10:15; Mk 6:11; Lk 10:12]
49Tazama, uovu wa dada yako, Sodoma, ulikuwa huu; kiburi, na kushiba chakula, na kufanikiwa, hayo yalikuwa ndani yake na binti zake; lakini hukuwasaidia maskini na wahitaji.[#Mwa 13:10; Lk 16:20]
50Nao walijivuna, wakafanya machukizo mbele zangu; kwa sababu hiyo niliwaondoa hapo nilipoyaona.[#Mwa 13:13; 18:20; Ayu 18:18]
51Samaria naye hakutenda nusu ya dhambi zako; bali wewe umeyaongeza machukizo yako zaidi ya hao, nawe umewapa haki dada zako kwa machukizo yako yote uliyoyatenda.[#Mt 12:41]
52Wewe nawe, ichukue aibu yako mwenyewe, kwa kuwa umetoa hukumu juu ya dada zako; kwa dhambi zako ulizozitenda, zilizochukiza kuliko hao, wao wana haki kuliko wewe; naam, ufedheheke wewe nawe, ukaichukue aibu yako, kwa kuwa umewapa haki dada zako.
53Nami nitawarudisha watu wao waliofungwa; wafungwa wa Sodoma na binti zake, na wafungwa wa Samaria na binti zake na wafungwa wako waliofungwa kati yao;[#Isa 1:9; Rum 9:29; Yer 20:16]
54upate kuichukua aibu yako mwenyewe, na kutahayari, kwa sababu ya mambo yote uliyoyatenda, kwa kuwa umekuwa faraja kwao.[#Eze 14:22,23]
55Na dada zako, Sodoma na binti zake, watairudia hali yao ya kwanza, na Samaria na binti zake watairudia hali yao ya kwanza, na wewe na binti zako mtairudia hali yenu ya kwanza.
56Kwa maana dada yako, Sodoma, hakutajwa kwa kinywa chako katika siku ya kiburi chako;
57kabla uovu wako haujafunuliwa bado, kama vile wakati ule walipokutukana binti za Shamu, na wale wote waliomzunguka, binti za Wafilisti wanaokudharau pande zote.[#2 Fal 16:5; 2 Nya 28:18; Isa 7:1]
58Yakupasa kupata adhabu ya uasherati wako, na machukizo yako, asema BWANA.
59Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitakutenda vile vile kama ulivyotenda, uliyekidharau kiapo kwa kulivunja agano.[#Kum 29:12-14; Eze 17:13,16]
60Walakini nitalikumbuka agano langu nililolifanya pamoja nawe, katika siku za ujana wako, nami nitaweka imara agano la milele pamoja nawe.[#Kut 2:24; Law 26:41,42; Zab 106:45; Hos 2:15; Yer 32:40]
61Hapo ndipo utakapozikumbuka njia zako, na kutahayarika, hapo utakapowakaribisha dada zako, walio wakubwa wako na wadogo wako; nami nitakupa hao wawe binti zako, lakini si kwa agano lako.[#Eze 20:43; Wim 8:8; Isa 2:2; 54:1; Gal 4:26]
62Nami nitaweka imara agano langu nawe; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi BWANA;[#Hos 2:19,20; Mdo 7:8; Ebr 8:6-10,13]
63upate kukumbuka, na kufadhaika, usifumbue kinywa chako tena, kwa sababu ya aibu yako; hapo nitakapokusamehe yote uliyoyatenda, asema Bwana MUNGU.[#Rum 3:19]