The chat will start when you send the first message.
1Tena uwaombolezee wakuu wa Israeli,[#Eze 26:17]
2useme, Mama yako alikuwa nini? Simba mke; alijilaza kati ya simba, kati ya wanasimba aliwalisha watoto wake.
3Akamlea mtoto mmoja katika watoto wake, akawa mwanasimba, akajifunza kuwinda mawindo, akala watu.[#2 Fal 23:31]
4Mataifa nao wakapata habari zake, akanaswa katika rima lao, wakamchukua kwa kulabu mpaka nchi ya Misri.[#2 Fal 23:33; 2 Nya 36:4; Yer 22:11]
5Basi mamaye alipoona kwamba amemngoja, na tumaini lake limepotea, akatwaa mtoto mwingine katika watoto wake, akamfanya mwanasimba.[#2 Fal 23:34]
6Naye akaenda huku na huko kati ya simba, akawa mwanasimba, akajifunza kuwinda mawindo, akala watu.[#Yer 22:13]
7Akayajua majumba yao, akaiharibu miji yao; nchi ikawa ukiwa, na vyote vilivyomo, kwa sababu ya mshindo wa kunguruma kwake.
8Ndipo mataifa wakajipanga juu yake pande zote toka nchi zote; wakaunda wavu wao juu yake; akanaswa katika rima lao.[#2 Fal 24:2]
9Wakamtia katika tundu kwa kulabu, wakamleta kwa mfalme wa Babeli wakamtia ndani ya ngome, sauti yake isisikiwe tena juu ya milima ya Israeli.[#2 Nya 36:6; Yer 52:3-11; Eze 6:2]
10Mama yako alikuwa kama mzabibu, katika damu yako, uliopandwa karibu na maji; akazaa sana na kujaa matawi, kwa sababu ya maji mengi.[#Eze 15:2; Zab 80:8; Kum 8:7]
11Naye alikuwa na vijiti vya nguvu, kwa fimbo za enzi zao watawalao, na kimo chao kiliinuka kati ya matawi manene, wakaonekana kwa urefu wao, pamoja na wingi wa matawi yao.[#Dan 4:11]
12Lakini aling'olewa kwa ghadhabu, akaangushwa chini, upepo wa mashariki ukakausha matunda yake; vijiti vyake vya nguvu vikavunjika, vikakauka; moto ulivila.[#Hos 13:15]
13Na sasa umepandwa jangwani, katika nchi kavu, ya ukame.[#Kum 28:48]
14Na moto umetoka katika vijiti vya matawi yake, umekula matunda yake, hata hana tena kijiti cha nguvu kifaacho kwa fimbo ya enzi ya kutawala. Na hayo ni maombolezo, nayo yatakuwa maombolezo.[#Amu 9:15]