The chat will start when you send the first message.
1Na wewe, mwanadamu, tabiri juu ya Gogu, useme, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Gogu, mkuu wa Roshi, Mesheki, na Tubali;[#Eze 38:2]
2nami nitakugeuza na kukuongoza, nami nitakupandisha toka pande za mwisho za kaskazini; nami nitakuleta juu ya milima ya Israeli;
3nami nitaupiga upinde wako, utoke katika mkono wako wa kushoto, na mishale yako nitaiangusha, itoke katika mkono wako wa kulia.
4Utaanguka juu ya milima ya Israeli, wewe, na vikosi vyako vyote, na watu wa kabila nyingi walio pamoja nawe; nami nitakutoa na kuwapa ndege wa kila namna walao nyama, na wanyama wa pori, uliwe na wao.[#Isa 34:2-8; Yer 15:3; Eze 32:4,5; Ufu 19:17-21]
5Utaanguka katika uwanda; kwa maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU.
6Nami nitapeleka moto juu ya Magogu; na juu ya watu wote wakaao salama katika visiwa; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.[#Amo 1:4; Zab 72:10]
7Na jina langu takatifu nitalifanya kuwa limejulikana kati ya watu wangu Israeli; wala sitaliacha jina langu takatifu kutiwa unajisi tena; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, na Aliye Mtakatifu katika Israeli.[#Law 18:21; Eze 38:16]
8Tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU; hii ndiyo siku ile niliyoinena.[#Eze 7:3-8; 38:17]
9Hao wakaao katika miji ya Israeli watatoka, nao watafanya mioto kwa silaha za vita na kuziteketeza, ngao, na vigao, na pinde, na mishale, na mafumo, na mikuki, nao watazitumia kama kuni kwa muda wa miaka saba;
10hata hawataokota kuni mashambani, wala hawatakata kuni msituni; maana watafanya mioto kwa silaha zile; nao watawateka nyara watu waliowateka wao, na kuwapora watu waliowapora wao, asema Bwana MUNGU.[#Isa 14:2]
11Tena, itakuwa katika siku hiyo, nitampa Gogu pa kuzikia katika Israeli, bonde la wapitao, upande wa mashariki wa bahari; nalo litawazuia wapitao; na huko watamzika Gogu na jamii ya watu wake wote; nao wataliita, Bonde la Hamon-Gogu.
12Na kwa muda wa miezi saba, nyumba ya Israeli watakuwa wakiwazika, wapate kuitakasa nchi.[#Kum 21:23]
13Naam, watu wote wa nchi hiyo watawazika; itakuwa ni sifa kwao katika siku ile nitakapotukuzwa, asema Bwana MUNGU.[#Zab 126:2]
14Nao watawachagua watu wa kufanya kazi ya daima, watakaopita kati ya nchi, ili kuwazika waliosalia juu ya uso wa nchi, ili kuisafisha; miezi saba itakapokwisha kupita watachunguza.
15Na hao wapitao kati ya nchi watachunguza; na mtu yeyote aonapo mfupa wa mtu, ndipo atakapoweka alama karibu nao, hadi wazikaji watakapouzika katika bonde la Hamon-Gogu.
16Tena, Hamona litakuwa jina la mji. Hivyo ndivyo watakavyotakasa nchi.
17Na wewe, mwanadamu, Bwana MUNGU asema hivi; Sema na ndege wa kila namna, na kila mnyama wa porini, Jikusanyeni, mje; jikusanyeni pande zote mwijie karamu yangu ya kafara ninayoandaa kwa ajili yenu, naam, karamu kuu ya kafara juu ya milima ya Israeli, mpate kula nyama na kunywa damu.[#Isa 18:6; Ufu 19:17-18]
18Mtakula nyama yao walio hodari, na kunywa damu ya wakuu wa dunia, ya kondoo dume na ya wana-kondoo, na ya mbuzi, na ya ng'ombe, wote na wanono wa Bashani.[#Eze 29:4; Kum 32:14; Zab 22:12]
19Nanyi mtakula mafuta na kushiba, mtakunywa damu na kulewa, katika karamu yangu ya kafara ninayoiandaa kwa ajili yenu.
20Nanyi mtashibishwa mezani pangu kwa farasi, na magari ya vita, na mashujaa, na watu wote wa vita, asema Bwana MUNGU.[#Zab 76:6; Eze 38:4; Ufu 19:18]
21Nami nitauweka utukufu wangu kati ya mataifa, na mataifa wote wataiona hukumu yangu niliyoitekeleza, na mkono wangu niliouweka juu yao.[#Kut 9:16; 7:4; Isa 26:11; Eze 36:23; Mal 1:11]
22Basi, nyumba ya Israeli watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wao, tangu siku hiyo na baadaye.
23Nao mataifa watajua ya kuwa nyumba ya Israeli walihamishwa, na kwenda kifungoni, kwa sababu ya uovu wao; kwa sababu waliniasi, nami nikawaficha uso wangu; basi nikawatia katika mikono ya adui zao, nao wote wakaanguka kwa upanga pia.[#Kum 31:17; Law 26:25]
24Kwa kadiri ya uchafu wao, kwa kadiri ya makosa yao, ndivyo nilivyowatenda, nami nikawaficha uso wangu.[#Eze 36:19]
25Kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU asema hivi, Sasa nitawarejesha watu wa Yakobo waliohamishwa, nitawahurumia nyumba yote ya Israeli; nami nitalionea wivu jina langu takatifu.[#Yer 30:3; Hos 1:11]
26Nao watachukua aibu yao, na makosa yao yote waliyoniasi, watakapokaa salama katika nchi yao wenyewe, wala hapana mtu atakayewatia hofu;[#Dan 9:16; Law 26:5]
27nitakapokuwa nimewaleta tena kutoka makabila ya watu, na kuwakusanya kwa kuwatoa katika nchi za adui zao, na kutakaswa kati yao mbele ya macho ya mataifa mengi.[#Eze 28:25; 36:23]
28Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wao, kwa kuwa niliwahamisha, waende utumwani kati ya mataifa, na mimi nikawakusanya, na kuwaingiza katika nchi yao wenyewe; wala sitawaacha tena huko kamwe, hata mmojawapo;[#Eze 34:30; Hos 2:20]
29wala sitawaficha uso wangu tena; kwa maana nimemwaga roho yangu juu ya nyumba ya Israeli, asema Bwana MUNGU.[#Isa 54:8; Yoe 2:28]