Ezekieli 6

Ezekieli 6

Hukumu kwa Israeli kwa kuabudu sanamu

1Neno la BWANA likanijia, kusema,

2Mwanadamu, uelekeze uso wako uitazame milima ya Israeli, ukaitabirie,[#Eze 36:1]

3ukisema, Enyi milima ya Israeli, lisikieni neno la Bwana MUNGU; Bwana MUNGU aiambia hivi milima na vilima, na vijito na mabonde; Tazama, mimi, naam, mimi, nitaleta upanga juu yenu, nami nitapaharibu mahali penu palipoinuka,[#Law 26:30]

4Na madhabahu zenu zitakuwa ukiwa, na sanamu zenu za jua zitavunjika; nami nitawatupa wana wenu waliouawa mbele ya vinyago vyenu.[#Yer 44:28; Eze 5:2,12]

5Nami nitaiweka mizoga ya wana wa Israeli mbele ya vinyago vyao; nami nitaitawanya mifupa yenu pande zote za madhabahu zenu.

6Kila mahali mkaapo miji itaharibika, na mahali palipoinuka patakuwa ukiwa; ili madhabahu zenu ziharibiwe, na kufanywa ukiwa, na vinyago vyenu vivunjwe, na kukoma, na sanamu zenu za jua zikatwe, na kuangushwa, na kazi zenu zifutwe kabisa.

7Na hao waliouawa wataanguka katikati yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

8Lakini nitasaza mabaki; maana mtakuwa na baadhi ya watu watakaoukimbia upanga kati ya mataifa, mtakapokuwa mmetawanyika katika nchi za watu.

9Na hao wa kwenu watakaookoka watanikumbuka kati ya mataifa, watakakochukuliwa mateka, jinsi nilivyoiponda mioyo yao ya kikahaba, iliyoniacha, na macho yao, yaendayo kufanya uasherati na vinyago vyao; nao watajichukia nafsi zao machoni pao wenyewe, kwa sababu ya mabaya yao yote, waliyoyatenda kwa machukizo yao yote.[#Zab 78:40; Isa 7:13; Hes 15:39; Eze 20:7,43; Law 26:39; Ayu 42:6]

10Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA; sikusema bure kama nitawatenda mabaya hayo.

11Bwana MUNGU asema hivi; Piga kwa mkono wako, ipige nchi kwa mguu wako, ukaseme, Ole! Kwa sababu ya machukizo maovu yote ya nyumba ya Israeli; maana wataanguka kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni.[#Law 26:36; Eze 12:16; 5:12]

12Yeye aliye mbali sana atakufa kwa tauni; na yeye aliye karibu atakufa kwa upanga; na yeye atakayesalia, na kuhusuriwa katika mji, atakufa kwa njaa, hivyo ndivyo nitakavyoitimiza ghadhabu yangu juu yao.

13Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, watu wa kwao waliouawa watakapokuwa kati ya vinyago vyao, pande zote za madhabahu zao, juu ya kila kilima kirefu, juu ya vilele vya milima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, na chini ya kila mwaloni mnene, pale pale walipovifukizia uvumba mzuri vinyago vyao vyote.[#Yer 2:20; 15:2,3; Hos 4:13; Isa 57:5]

14Nami nitanyosha mkono wangu juu yao, na kuifanya nchi kuwa maganjo, tena ukiwa mbaya kuliko jangwa upande wa Dibla, katika makao yao yote; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.[#Isa 5:25; Hes 33:46]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania