Ezekieli 7

Ezekieli 7

Maafa yajayo

1Tena neno la BWANA likanijia, kusema,

2Na wewe, mwanadamu, Bwana MUNGU aiambia hivi nchi ya Israeli; Ni mwisho; mwisho umezijia pembe nne za nchi.[#Kum 32:20; Omb 4:18; Amo 8:2; Mt 24:6]

3Sasa mwisho huu unakupata, nami nitakuletea hasira yangu, nitakuhukumu kulingana na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote.

4Jicho langu halitakuachilia, wala sitaona huruma; bali nitakupatiliza njia zako, na machukizo yako yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.[#Eze 5:11; 6:7]

5Bwana MUNGU asema hivi; Ni jambo baya, jambo baya la namna ya peke yake; angalia, linakuja.

6Mwisho umekuja, mwisho huu umekuja; unaamka ukupate; angalia, unakuja.

7Ajali yako imekujia, wewe ukaaye katika nchi hii; majira yamewadia, siku ile inakaribia; siku ya fujo, wala si ya shangwe milimani.[#Isa 13:22; 1 Pet 4:17; Eze 12:23-25]

8Basi hivi karibu nitamwaga ghadhabu yangu juu yako, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote.[#Zab 79:6; Isa 42:25; Yer 7:20; Eze 20:8]

9Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga.

10Angalia, siku hiyo; angalia, inakuja; ajali yako imetokea; fimbo imechanua, kiburi kimechipuka.

11Udhalimu umeinuka, ukawa fimbo ya uovu; hapana mtu atakayesalia miongoni mwao, wala katika jamii yao, wala kitu katika utajiri wao; wala hakutakuwa kutukuka kati yao.[#Yer 6:7; 16:5]

12Majira yamewadia, siku ile inakaribia; huyo anunuaye asifurahi, wala asihuzunike auzaye; maana ghadhabu imewapata watu wote.

13Kwa maana auzaye hatakirudia kilichouzwa, wajapokuwa wangali hai; kwa sababu maono haya yawahusu watu wote; hapana mmoja atakayerudi; wala hapana mtu atakayejitia nguvu katika uovu wa maisha yake.

14Wamepiga tarumbeta, wametayarisha vitu vyote; lakini hapana aendaye vitani; maana ghadhabu yangu imewapata umati wote.

15Upanga uko nje, na tauni na njaa zimo ndani; yeye aliye nje mashambani atakufa kwa upanga; na yeye aliye ndani ya mji, njaa na tauni zitamla.[#Kum 32:25]

16Lakini watakaokimbia watakimbia, nao watakuwa juu ya milima kama hua wa bondeni, wote wakilia, kila mmoja katika uovu wake.[#Eze 6:8]

17Mikono yote itakuwa dhaifu, na magoti yote yatalegea kama maji.[#Isa 13:7]

18Tena watajifungia nguo za magunia, na utisho utawafunika; na aibu itakuwa juu ya nyuso zote, na upaa juu ya vichwa vyao vyote.[#Yer 6:26; Zab 55:5]

19Watatupa fedha yao katika njia kuu za mji, na dhahabu yao itakuwa kama kitu cha unajisi; fedha yao na dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa siku ya ghadhabu ya BWANA; hawatajishibisha roho zao, wala hawatajijaza matumbo yao; kwa sababu zilikuwa kwazo la uovu wao.[#Mit 11:4; Sef 1:18; Eze 44:12]

20Na uzuri wa pambo lake, yeye aliuweka katika enzi, lakini wao walifanya sanamu za machukizo yao, na vitu vyao vichukizavyo, ndani yake; ndiyo maana nimeifanya kuwa kama kitu cha unajisi kwao.[#Yer 7:30]

21Nami nitapatia katika mikono ya wageni pawe mateka yao, na katika mikono ya waovu wa duniani pawe mawindo yao, nao watapanajisi.

22Tena nitaugeuza uso wangu usiwaelekee, nao watapatia unajisi mahali pangu pa siri; na wanyang'anyi wataingia humo na kupatia unajisi.

23Ufue mnyororo; kwa maana nchi hii imejaa hukumu za damu, nao mji umejaa udhalimu.[#Mwa 9:6; 2 Fal 21:16; Zab 10:8]

24Kwa sababu hiyo nitawaleta watu wa mataifa walio wabaya kabisa, nao watazimiliki nyumba zao; tena nitakikomesha kiburi chao wenye nguvu; na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi.[#Hab 1:6]

25Uharibifu utakapokuja; nao watatafuta amani, lakini haitapatikana.

26Madhara yatakuja juu ya madhara, na habari ya shari juu ya habari ya shari; nao watakwenda kwa nabii kutaka maono; lakini hiyo sheria itampotea kuhani, na mashauri yatawapotea wazee.[#Kum 32:23; Zab 74:9; Omb 2:9; Mal 2:7-9]

27Mfalme ataomboleza, na mkuu atavikwa ukiwa, na mikono ya watu wa nchi itataabika; nitawatenda kulingana na njia yao; nami nitawahukumu kulingana na kustahili kwao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania